Profesa Issa Shivji akitoa mhadhara chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Profesa Issa Shivji akitoa mhadhara chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Kati ya maneno yaliyonasa katika vichwa vya wasikilizaji na watazamaji wa mhadhara wa Prof. Shivji ni Maelewano (Compromise) na Mapatano (Concensus). Hakuna shaka kuwa Prof. Shivji aliyatumia vizuri sana kufikisha ujumbe wake. Kwa mujibu wa Prof. Shivji, katika majadiliano ndani ya Tume, Wajumbe wa Tume ya Warioba walilazimika kuelewana (na sio kupatana) kuhusu ibara mbalimbali za Rasimu ya Katiba ili kutokwamisha maamuzi na hatimaye Rasimu ikatoka.

Katika kujenga hoja hii, Prof. Shivji anasema kwa kawaida Maelewano huzaa maamuzi legelege wakati Mapatano ni matokeo ya hoja bora na huzaa maamuzi bora na baada ya mwafaka kila mmoja hutoka ndani akiwa ameridhika na amefurahi.

Bila shaka, katika hali ya kawaida, hili la mapatano (concensus) ni jambo jema zaidi ukilinganisha na maelewano (compromise) kama ilivyofafanuliwa na Prof. Shivji. Kama inawezekana kwa wajumbe kukaa mezani, kuongea kwa kina na uwazi na kupatana kwa kuridhika, sote tungeshukuru. Lakini kwa maoni yangu, hili ni gumu kwa suala nyeti kama Katiba Mpya.

Pamoja na Prof. Shivji kujaribu kujenga hoja yake vizuri, lazima nikiri kuwa bado naona ugumu. Nasema kuna ugumu kwa kuwa sikumbuki ni nchi gani hapa duniani wananchi wake waliandika Katiba yao bila kuelewana (compromise). Prof. Shivji katika mhadhara wake ulichapishwa katika kitabu cha kurasa 43 ametaja nchi kama Marekani na Australia kuwa zina Ibara zinazotoa ukuu wa Katiba ya Shirikisho, lakini ameshindwa kututajia hata nchi moja iliyoandika Katiba bila maelewano (compromise).

Dhana ya Maelewano inatekelezeka Tanzania?

Anachozungumzia Prof. Shivji ni dhana tu ambayo kwa maoni yangu, naamini haitekelezeki. Mosi, Tume yenyewe imeundwa na watu kutoka Tanzania Bara na Visiwani na ambao wanatoka katika makundi yenye itikadi, mitizamo na maslahi mbalimbali ambayo wakati mwingine yanakinzana.

Kati ya makundi haya, ambayo ni muhimu tukumbuke kuwa yanawakilisha maoni ya wananchama wao, yapo yanayotaka Serikali moja na mengine mbili. Pia yapo yanayotaka tatu au nne huku mengine yakitaka Muungano wa Mkataba. Unafikiaje mapatano (concensus) katika mazingira kama haya? Ni wazi kuwa kutakuwa na maelewano (compromise).

Mimi binafsi, na nadhani wengi wa wasomaji, hatutegemei wajumbe wote 32 wapatane (concensus) kama inavyotokea kwa wale wanafunzi wa Chuo Kikuu wanapopatana (tena sio wote) kugoma ili kushinikiza maslahi yao ya posho ya chakula iongezewe kwa kuwa wote wana maslahi nayo.

Historia inakubaliana na mapatano (concensus)?

Jambo jingine la kuangalia hapa ni historia ya mijadala hii ya Katiba na muundo wa Muungano. Kwa kuangalia historia ya mijadala ya Muungano kwa miongo kadhaa sasa, nashawishika kuamini kuwa hili la mapatano (concensus) ni gumu. Nitajaribu kufafanua.

Kutoka kuchafuka kwa hali ya kisiasa Zanzibar mwaka 1984 na kusababisha ‘kujiuzulu’ kwa Mzee Abood Jumbe wakati wadau wa Zanzibar wakidai mamlaka zaidi hadi kuundwa kwa Kundi la Wabunge, Maarufu kama G55 likidai Serikali ya Tanganyika mwanzoni mwa miaka ya 1990, umuhimu wa kuwepo kwa maelewano (compromise) ili tusonge mbele kama Taifa unaonekana hauepukiki.

Aidha, Tume mbili kubwa, ile ya Jaji Mkuu Mstaafu Francis Nyalali ya mwaka 1992 na ile Kamati ya Jaji Robert Kisanga iliyotoa taarifa yake mwaka 1998, zote zilipendekeza uwepo wa Serikali Tatu. Kikubwa cha kukumbuka hapa ni kuwa, Tume hizi nazo zilizunguka nchi nzima na kukusanya maoni ya wananchi ya watu wenye maslahi tofauti kama ilivyo hii ya Jaji Warioba. Kwa maoni yangu, Tume hizi mbili, nazo zilikutana na maoni yanayokinzana na ilibidi kutoa mapendekezo yatakayowafanya watanzania waelewane (wa-compromise).

Nimalizie kwa kusema kuwa kufikia mwafaka kwa kutumia hii dhana ya mapatano (compromise) haiepukiki kwa binadamu tunatoka katika mazingira tofauti yenye masalhi tofauti. Kama alivyosema Jenerali Ulimwengu tarehe 24 Agosti mwaka 1993 alipokuwa akichangia Bungeni, lazima tuwe na kitu kinaitwa spirit of give and take, ili tupate ushindi ambao kwangu mimi ni Katiba Mpya ambayo, angalau kila kundi linahisi sehemu ya maslahi yake yameguswa. Kwa kweli, hata wanandoa, ambayo ni taasisi ndogo kabisa katika jamii, hulazimika ku-compromise katika mambo mengi sana ili kuishi pamoja!

Hatutarajii, kwa mfano, mwanandoa akakimbilia kuomba talaka au kujitenga ati kwa sababu mwenzake anakoroma kwa sauti kubwa akiwa usingizini. Hili linapaswa liwe suala la kuvumiliana. Kwa wanandoa wenzake, pengine wenye matatizo makubwa kuliko lake, hii itakua sababu feki kwa kuwa inawezekana kabisa, kukoroma huko kulivumilika wakiwa wachumba.

Katika hili la Katiba Mpya, mtu au kundi lolote, liwe linalotaka Serikali moja, mbili, tatu, nne au mkataba, linapaswa kukubali kuwa ndani ya Tanzania kuna makundi na watu wengine ambao nao wana haki kama ilivyo kwake. Kwa hiyo, wamkumbuke Jenerali Ulimwengu.


Sehemu ya makala “Prof. Shivji, hata wanandoa wana-compromise” ya Simon Mwalwimle kwenye Raia Mwema la tarehe 10 Julai 2013

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.