Julius Nyerere akiwa Kiongozi wa Bunge la Tanganyika.
Julius Nyerere akiwa Kiongozi wa Bunge la Tanganyika.

KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya, pamoja na mambo mengine, tuliona jinsi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulivyofikiwa kwa dharura kutokana na kushindwa kwa juhudi za Mwalimu Nyerere kuratibu kuanzishwa kwa Shirikisho la nchi za Afrika Mashariki – Tanganyika, Kenya, Uganda na Zanzibar; chini ya Azimio la pamoja la Viongozi wa nchi hizo Kumb: Na. 13/931/63/PDT/1/1 la Juni 5, 1963.

Hivi karibuni, Mwanazuoni mahiri nchini, Profesa Issa Shivji,ambaye pia ni Mwenyekiti mstaafu wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alihoji kwenye Kongamano la Kigoda hicho, Juni 21, 2013; juu ya uhalali wa Mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, akisema “Hati ya Mkataba wa Muungano ndiyo nguzo kuu inayotawala Katiba” na pia kwamba Muundo wa Muungano wetu, kwa mujibu wa Mkataba huo, ni wa Serikali mbili.

Profesa Shivji ambaye ni msomi mwenye kuheshimika nchini, ni mfuasi na mtetezi mkubwa (kama nilivyo mimi), wa falsafa, sera na fikra za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alikuwa mtetezi mkubwa wa Muundo wa Serikali mbili kwa sababu ambazo tutaziona baadaye.

Muundo wa Muungano wetu uko dhahiri kwa mujibu wa Mkataba, na Mwalimu Nyerere, kama Mwanasiasa, anaweza kusamehewa kwa kushindwa kutafsiri kwa usahihi hati hiyo ya kisheria iliyoandaliwa na Mwanasheria wake Mkuu, Roland Brown kwa “Muundo wa uhusiano kati ya Serikali ya Uingereza na Serikali ya Ireland Kaskazini”, kuwa ndio Muundo wa Muungano wa Tanzania.

Lakini si Profesa Shivji yeye kama Msomi na Mwanasheria mzamifu wa Sheria za Katiba, na ambaye ameliandikia kwa kirefu jambo hili,anayeweza kusamehewa kwa kutoa tafsiri tofauti na kinzani kwenye Kongamano, kama nitakavyochambua katika makala haya.

Na hii ni hatari kubwa kwa nchi, kwa wasomi wanaotegemewa na jamii kujiambatisha na hisia (sentiments) za kisiasa ndani ya ombwe la uongozi na kukosa dira, linalopashwa kuzibwa na wasomi hao.

Niharakishe kutamka mapema hapa kwamba, pamoja na ushujaa, ushupavu na uongozi bora wa Mwalimu Nyerere enzi za utawala wake, lakini kwa hili la Muungano nasema hakufanya vyema; na ni kwa sababu tu aliachwa kucheza namba zote uwanjani bila ushauri wala kuzingatia matakwa ya Muungano, na matokeo yake ameacha Muungano ukiwa umeghubikwa na kero tele, ukipiga miayo kutaka tafsiri sahihi ya Muundo.

Mmoja wa Waasisi wa Muungano, Abeid Amani Karume, aliamini kwamba, aliingia Mkataba wa kuunda Shirikisho la nchi na Serikali tatu.  Na pale alipobaini utekelezaji tofauti, hakutaka tena kuundwa Tume ya kupendekeza Katiba ya Muungano, na mara nyingi alitaka kuona Muungano unavunjwa kwa kile alichoita “Muungano ni kama koti, likikubana unalivua”.  Matokeo yake ni kwa Muungano huo kuendeshwa kwa Katiba ya Muda kwa miaka 13 hadi mwaka 1977 wakati yeye alikuwa amekwishatangulia mbele ya haki.

Vivyo hivyo kadhalika, Rais wa awamu ya pili Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, mwaka 1984 alihoji mantiki ya dhana ya Serikali mbili kinyume cha Mkataba wa Muungano, kufuatia mapendekezo ya CCM ya mabadiliko zaidi ya Katiba ya Muungano na Katiba ya Zanzibar, kwa Katiba hiyo ya Muungano kutaka kutwaa mambo zaidi ya Muungano kutoka Zanzibar.

Jumbe hakusalimika, alivuliwa ngazi zote za uongozi za Muungano na Visiwani. Tutaona baadaye, kwanini CCM bado inatetea Muundo wa Serikali mbili, licha ya kupingwa na sehemu zote za Muungano.

Sasa tuendelee na sehemu ya tatu ya makala hii, ambayo kwa bahati nzuri itakuwa inajibu pia hoja ya Profesa Shivji, na kwa sehemu kubwa kwa kutumia baadhi ya maandiko yake mwenyewe ya nyuma kuthibitisha kwamba Muundo asilia wa Muungano unaotakiwa ni wa Shirikisho.

Sote tunakubaliana na Prof. Shivji, kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifikiwa kwa kutiwa sahihi kwa Mkataba wa Kimataifa (International Treaty) na Wakuu wa nchi hizo mbili; ujulikanao kama HATI YAMUUNGANO (Articles of Union), na kuridhiwa na taasisi za kutunga Sheria za nchi hizo na kuwa sehemu ya Sheria za nchi hizo kwa jina la “SHERIA ZA MUUNGANO”  (Acts of Union).

Prof. Shivji anaandika kwa usahihi kabisa katika kitabu chake “The Legal Foundations of the Union” (Misingi ya Kisheria ya Muungano) ukurasa tano, kwamba:“Sheria za Muungano ni Hati ya Kikatiba na aina ya Sheria mama.  Ndiyo msingi mkuu wa Muungano ambao Kanuni zingine zote kuhusiana na Muungano zinapata nguvu za Kisheria na uhalali wake”.

Anaendelea kusema (uk. 14) kwa usahihi pia kwamba, “Sheria ya Muungano (namba 22, ya 1964) ndiyo Katiba ya maandishi [written Constitution] ya Muungano”, na kwamba, “ikitokea mgongano kati ya Katiba ya Muungano au Katiba ya Zanzibar na Mkataba wa Muungano (Sheria ya Muungano), Mkataba wa Muungano utashinda”.

Kama hivyo ndivyo, na kweli ndivyo ilivyo; Mkataba wa Muungano, kama ulivyoridhiwa kuwa Sheria ya Muungano Namba 22, 1964, ndiyo muhimili mama wa kufuatwa na Katiba zote katika Muungano.

Tume ya Warioba imetamka bayana kuongozwa na Mkataba wa Sheria ya Muungano.

Na kwa sababu hiyo, tuangalie ibara ya 5 ya Sheria ya Muungano (ibara ya 4, Mkataba wa Muungano), inasema nini kuhusu Muundo sahihi wa Muungano.

Ibara 5 (1) (a), inataja mambo 11 tu yatakayoshughulikiwa na Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano; na kwa mujibu wa ibara ya 5 (2), Katiba ya Tanganyika itarekebishwa (ilirekebishwa) na kutumika pia kama Katiba ya Muungano, kwa njia ya Amri ya Rais, kwa kuingiza mambo yote 11 ya Muungano hadi hapo Jamhuri ya Muungano (kwa mujibu wa ibara ya 7 ya Mkataba na ibara ya 9 ya Sheria ya Muungano) itakapopata Katiba yakekwa utaratibu uliowekwa na Sheria hizo.

Makala ya Joseph Mihangwa kwenye gazeti la Raia Mwema la tarehe 10 Julai 2013

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.