Viongozi wakuu wa serikali za Tanzania na Zanzibar wanapinga serikali tu
Viongozi wakuu wa serikali za Tanzania na Zanzibar wanapinga serikali tu

GAZETI hili toleo la Julai 3, mwaka huu lilichapisha makala iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Walaaniwe wanaolilia serikali tatu na Tanganyika”, iliyoandikwa na mwandishi aliyejiita “Mwandishi Maalumu”.

Makala hiyo ilikuwa ikijibu makala yangu iliyochapishwa na gazeti hili hili toleo la Juni 26, mwaka huu, ambayo kwa ufupi ilijibu hoja za watu wanaopinga pendekezo la Tume ya Mabadiliko ya Katiba la kutaka muundo wa Muungano uwe serikali tatu.

Nilisema katika makala hiyo kuwa hoja za watu wanaopinga muundo wa serikali tatu kwamba utasababisha kuvunjika kwa Muungano hazina nguvu kwa sababu Watanzania wa Tanganyika na Zanzibar wengi wameonyesha bado wanautaka Muungano uendelee kuwepo isipokuwa wanataka muundo mpya ili kuondoa manung’uniko na malalamiko makubwa ya sasa.

Wengi wanataka Muungano wa serikali tatu badala ya mbili za sasa. Kwa maneno mengine Watanzania wengi wanataka kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika iliyofutwa kinyemela mwaka 1964 baada ya kufikiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Niliandika kuwa hoja ya wahafidhina kwamba kuwepo serikali tatu itasababisha kuvunjika kwa Muungano ni maneno matupu yasiyofanana na hali halisi. Nilisema kuwa wapinzani wa mabadiliko ya muundo wa Muungano wamevaa miwani ya mbao kwa kutotaka kuuona ukweli, hawazisomi alama za nyakati na wameshindwa kwenda na kasi ya wakati na mabadiliko ya dunia ya kisasa.

Nilibainisha kuwa muundo wa sasa wa serikali mbili wanaoung’ang’ania wahafidhina ndiyo utakaoupeleka kaburini Muungano wetu kwa sababu ni muundo usio wa haki na usiozingatia hali halisi ya nchi zetu mbili, Tanganyika na Zanzibar. Ni muundo unaojenga chuki na uhasama kati ya wananchi wa pande zote mbili za Muungano ambapo kila upande unahisi kuonewa.

Kuhusu gharama, niliandika kuwa hiyo si hoja ya kutiliwa uzito katika mjadala wa serikali tatu kwa sababu hakuna ushahidi madhubuti wa kuithibitisha. Nilisema kuwa hoja ya gharama ni kama kichaka wanachokitumia wahafidhina kuficha nia yao mbaya. Nilisema huo ni ujanja wa watawala kutaka kulinda maslahi yao.

Haiwezekani kuwepo ongezeko la gharama za uendeshaji kwa sababu tutaunda serikali ndogo sana ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Tanganyika. Kwa mfano, nilisema kuwa Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano litakuwa na mawaziri na naibu mawaziri wasiozidi 10 tu. Aidha, hata idadi ya watumishi wa kada mbalimbali katika Serikali ya Muungano hawatakuwa wengi kwa sababu haitakuwa na kazi nyingi.

Nilisema serikali kubwa kidogo itakuwa Serikali ya Tanganyika, ambayo nayo nilipendekeza iwe na mawaziri na naibu mawaziri wasiozidi 25 tu. Hatuhitaji serikali yenye mawaziri 60 kama ya Rais Jakaya Kikwete.

Katika kuhakikisha tunapunguza zaidi matumizi, nilipendekeza tusiwe na wakuu wa wilaya, badala yake wenyeviti na mameya wa halmashauri tuwafanye kuwa watendaji. Aidha, nilipendekeza Bunge la Tanganyika liwe na wajumbe wachache wasiozidi 200.

Sasa huyu jamaa aliyejiita Mwandishi Maalumu amejaribu kufurukuta kunijibu. Nampongeza sana kwanza kwa kuwa msomaji wa gazeti hili, na pili kwa kuisoma na kuguswa na makala yangu, naamini ujumbe nilioukusudia umefika kwake na kwa wengine wenye mtazamo kama huo.

Kabla sijaanza kuchambua majibu yake, naomba nianze kwa kutolea ufafanuzi neno “walaaniwe” nililolitumia katika makala yangu na ambalo linaonekana kumkwaza Mwandishi Maalumu.

Anasema hakuna haja ya kulaaniana kutokana na kutofautiana kimtazamo kuhusu muundo wa Muungano.

Mimi nasisitiza kuwa wanapaswa kulaaniwa wale wote wanaopinga kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika. Ninasema hivyo kwa sababu kukataa kurejeshwa kwa Tanganyika ni sawa na mtu kumkana mzazi wake. Hivi dhambi ya kumkana mzazi wako adhabu yake nini? Bila shaka ni laana tu.

Tanganyika ni mama yetu, hivyo laana ndiyo adhabu pekee inayowafaa wanaopinga kurejeshwa Tanganyika. Mtu yeyote anayemkana mzazi wake anastahili kulaaniwa na Mwenyezi Mungu. Anayeikana Tanganyika alaaniwe, na siwezi kubadili msimamo wangu wala kuomba radhi katika hilo.

Ama kuhusu hoja nilizoandika katika makala yangu ya kwanza, nasikitika kwamba jamaa huyu ameshindwa kuzijibu. Makala yake imejaa maneno matupu yasiyo na hoja ndani yake. Ameendeleza wimbo kwamba serikali tatu zitaongeza gharama za uendeshaji bila kutoa mchanganuo wenye kuthibitisha hoja hiyo, bila shaka madai ya gharama yanabaki kuwa porojo na maneno matupu.

Anasema kuwa muundo wa serikali tatu utawaongezea mzigo Watanganyika kwa hoja kuwa ndio watakaobeba mzigo mkubwa zaidi wa kuiendesha Serikali ya Muungano. Hii siyo hoja yenye mashiko kwa sababu hata sasa Tanganyika inaendesha Serikali ya Muungano.

Pengine ndugu yangu Mwandishi Maalumu hajui kuwa serikali ya sasa ya Muungano ni mbili katika moja, kwa maana kuna mambo ya Muungano na yale ya Tanganyika ambayo yote yanasimamiwa na Serikali ya Muungano. Rais wa Jamhuri ya Muungano anasimamia pia mambo ya Tanganyika.

Kwahiyo, tutakachofanya ni kutenganisha tu utendaji. Na hili ndiyo msingi wa malalamiko ya ndugu zetu Wazanzibari ambao wanasema Tanganyika imejigeuza kuwa Muungano. Tunafanya hivi ili kuondoa malalamiko hayo na kuimarisha Muungano wetu.

Halafu jamaa huyu anasema kuwa hata kwa muundo wa sasa Watanganyika wanabeba mzigo mzito kwa hoja eti wanagharamia uendeshaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ambayo anadai haiwezi kujiendesha kwa sababu haina vyanzo vya uhakika vya mapato!

Haya ni matusi mabaya; ni dharau iliyopindukia dhidi ya Wazanzibari. Na kwa hakika ni kauli kama hizi zinazowafanya baadhi ya Wazanzibari wadai kujitenga na Muungano. Kama Wazanzibari ni mzigo, kwanini tunawang’ang’ania? Acheni matusi na dharau. Wazanzibari wanaendesha serikali yao kwa pesa zao wenyewe.

Kwahiyo, huyu Mwandishi Maalumu ameshindwa kutoa hoja madhubuti kuunga mkono madai yake kuwa serikali tatu zitaongeza gharama za uendeshaji. Pia ameshindwa kuvunja hoja zangu kuwa serikali tatu haziwezi kuongeza gharama za uendeshaji.

Hakuna popote katika makala yake alipozungumzia mapendekezo yangu ya kubana matumizi kwa kuwa na serikali ndogo kama hayawezekani, kwa maneno mengine amekubaliana nami, hivyo hoja ya kuongezeka gharama inakufa kifo cha asili.

Sasa nataka nijibu hofu yake kuwa Muungano utavunjika.

Anadai eti Muungano utavunjika kwa sababu kutakuwa na Watanganyika na Wazanzibari. Huu ndiyo udhaifu wa hoja za wapinzani wa serikali tatu. Hawana cha kushika ili kutetea upinzani wao. Hivi kwa sasa hakuna Watanganyika?

Watanganyika wapo ila hawana serikali yao. Tunachotaka ni kurejesha mamlaka ya utendaji ya Watanganyika mikononi mwao badala ya kumwachia Rais wa Muungano.

Marekani wana serikali 53, za majimbo 52 na moja ya shirikisho. Serikali za majimbo ya Marekani zina nguvu kubwa kikatiba, kisheria na kiutendaji. Majimbo ya Marekani yana Bunge, mahakama na serikali zao, na yanajitegemea kiuchumi. Lakini wana nchi moja tu ya Shirikisho la Marekani.

Halafu huyu jamaa anachekesha kweli, anadai kuwa kuwepo serikali tatu eti ni kwenda kinyume na dhana na dhamira ya Muungano ambao anadai ulilenga kuwa na serikali mbili kuelekea moja. Huu ni uongo wa kitoto na inaonyesha jinsi gani jamaa huyu asivyo na ufahamu wa kutosha kuhusu Muungano wetu.

Muungano wetu ulilenga kuwa na serikali tatu tangu mwanzo. Ndiyo maana Katiba ya Muungano inasema wazi kuwa yapo mambo ya Tanganyika ambayo imesema yatasimamiwa na Rais wa Muungano. Itakumbukwa kuwa baada ya kuungana mwaka 1964, Katiba ya Tanganyika ilirekebishwa kidogo na kuifanya kuwa ya Muungano ambayo ingetumika kwa kipindi cha mpito cha mwaka mmoja tu.

Baada ya kipindi hicho, Rais wa Muungano na Rais wa Zanzibar wangeunda Kamati ya Katiba ambayo ingekusanya maoni ya wananchi wa pande zote mbili ili kupata katiba mpya ya Muungano. Mchakato uliharibiwa na Mwalimu Julius Nyerere baada ya kuanza kufanya ujanja wa kutumia tamko la kisheria (decree) kurefusha muda wa kipindi cha mpito, na yaliharibika zaidi baada ya kifo cha Abeid Karume.

Inawezekana kabisa kuwa kama Karume angeendelea kuwa hai, Katiba ya Muungano isingeendelea kumpa Rais wa Muungano mamlaka ya kuwa pia msimamizi wa mambo ya Tanganyika. Inawezekana kabisa Serikali ya Tanganyika ingeundwa. (Soma kitabu cha mzee Abdul Jumbe; “The Partinership-Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Miaka Thelathini ya Dhoruba”).

Kuna uzushi mwingine huyu jamaa ameusema, eti serikali tatu zitasababisha utoroshaji mali za Watanganyika kwenda Zanzibar. Huu ni uzushi usio na msingi, ni mwendelezo wa matusi kwa Wazanzibari, ni kauli inayoongeza nguvu katika madai ya Wazanzibari wanaotaka kujitenga na Muungano.

Ama maoni kwamba serikali tatu zitadhoofisha uchumi wetu na kuongeza utegemezi kwa wafadhili, haya ni madai matupu yasiyoungwa mkono na hoja za kiuchumi. Mwandishi huyu hajatuambia kwa namna gani serikali tatu zitasababisha kudhoofika kwa uchumi wetu, tunapaswa kumpuuza.

Mfumo kama huu upo Ujerumani, Afrika Kusini, Ethiopia na Kenya. Kama hawa wameweza, kwanini sisi tushindwe? Tatizo ni kwamba watu wanajadili mambo kwa kuongozwa na hofu ya kuvunjika Muungano. Watu hawa wanapaswa kuelewa kuwa muundo wanaoung’ang’ania umeshindwa, na hauwezi kuendelea halafu tukabaki salama.

Chanzo: Makala ya George Maziku kwenye gazeti la Tanzania Daima la tarehe 10 Julai 2013

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.