Imeweka na Mhammed khamis

Mkurugenzi Mkuu wa Unesco Irina Bokova akizungumza na Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huko katika Hoteli ya Serena ikiwa ni muendelezo wa Ziara yake ya Siku mbili Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa Unesco Irina Bokova akizungumza na Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huko katika Hoteli ya Serena ikiwa ni muendelezo wa Ziara yake ya Siku mbili Zanzibar.

Shirika la Umoja wa Matifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika juhudi zake za kuimarisha ustawi wa wananchi kupitia sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya Elimu.

Akizungumza na baadhi ya Mawaziri wa Serikali ambao Wizara zao zinapata misaada  kupitia UNESCO, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Bi. Erina Bokova amesema juhudi zinazochukuliwa na Serikali zimepelekea mabadiloko makubwa ya maendeleo visiwani humo.

Amesema UNESCO itaendelea kusaidia sekta ya Elimu kwani inafahamu  kwamba kuimarika kwa sekta hiyo ni muelekeo mzuri wa kuimarika kwa sekta nyengine za maendeleo ikiwemo kilimo, utalii na masuala ya Utamaduni nchini.

Ameipongeza Wizara ya Elimu kwa hatua kubwa  iliyofikia ya kuwasomesha watoto wote waliofikia umri wa kusoma na ameeleza matumaini yake kwamba sera mpya ya Elimu ya Zanzibar itazidi kuimarika kwa sekta hiyo.

Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk kushoto akipokeya Zawadi kutoka kwa  Mkurugenzi Mkuu wa Unesco Irina Bokova walipomaliza Mazungumzo hapo katika Hoteli ya Serena ikiwa ni muendelezo wa Ziara yake ya Siku mbili Zanzibar.

Bi. Erina amesema suala la kuijengea uwezo Wizara ya Elimu na kuwaongezea ujuzi watendaji wake ni miongoni mwa masuala yatakayoendelea  kupewa kipaumbele na UNESCO.

Akizungumzia  kuimarishwa  Mji Mkongwe wa  Zanzibar, ambao ni moja kati ya miji iliyopata heshma ya kuwa ya Urithi wa Kimataifa, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO amesema hatua ya Serikali kuendelea kuuhifadhi mji huo ni hatua ya kupigiwa mfano.

Amesema mabadiliko madogo madogo aliyoyaona  katika baadhi ya majengo ya Mji Mkongwe hayaonyeshi kuondosha mandhari ya asili ya mji huo bali yanalenga zaidi kubuni vianzio vya ajira kwa wananchi wanaoishi ndani ya  mji huo.

Amesisitiza kwa Taasisi zinazosimamia Mji huo kuhakikisha kwamba malengo ya kuufanya mji huo kuwa mji wa urithi wa Kimataifa linaendelezwa na linasimamiwa vizuri zaidi.

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO amefurahishwa na uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukubali kuanzishwa kwa vituo vya  Redio Jamii Micheweni na  Mtegani Makunduchi na amesema hiyo ni moja ya hatua ya kuwapelekea maendeleo wananchi wa vijiji hivyo.

Amesema UNESCO itaendelea kusaidia utaalamu na vifaa mbali mbali kwa vituo hivyo na vituo vyengine vya aina hiyo ambavyo jamii za vijijini zitaamua kuvianzisha.

Akizungumza  katika mkutano huo ulioshirikisha wajumbe wa UNESCO na viongozi wa ngazi za juu wa Serikali katika Hoteli ya Serena Shangani, Waziri wa Habari, Utamduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk alisema vituo vya Redio Jamii vimekuwa na mchango mkubwa katika kusukuma mbele maendeleo ya wanajamii wenyewe.

Amesema vituo hivyo vimekuwa tegemea kubwa kwa wanajamii na vimeleta mabadiliko makubwa ya maisha  yao hasa katika masuala ya kupunguza umaskini na kukuza sekta ya Utalii ambayo imekuwa tegemeo kubwa kwa wananchi wa vijijini.

Mkurugenzi Mkuu wa Unesco Irina Bokova katikati akiwa katika Picha ya  pamoja na Mawaziri wa Serikali ya Zanzibar na Viongozi mbalimbali baada ya kumaliza kwa Mazungumzo yao katika Hoteli ya Serena ikiwa ni muendelezo wa Ziara yake ya Siku mbili Zanzibar.

Katika ziara yake ya siku mbili hapa Zanzibar, Ujumbe  wa UNESCO, ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, ulitembelea sehemu mbali mbali za Mji Mkongwe wa Zanzibar zikiwemo sehemu za kihistoria na baadhi ya vivutio vya Utalii vilivyomo ndani ya mji huo. 

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIB

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.