Imewekwa na Hamed Mazrouy

 

ASKARI wa Idara ya Maliasili katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, wamechoma moto na kuharibu nyumba za familia zaidi ya 200 katika kijiji cha Namalandula kata ya Namonge wilayani Bukombe mkoani Geita.

 

Katika tukio hilo wananchi wa kijiji hicho wakiongozwa na Diwani wao, Patrick Kaburusi walisema askari hao waliingia kijijini hapo juzi na kuanza kuwashambulia na kuwafukuza kwa kupiga risasi hewani wakiwatuhumu kuishi kwenye hifadhi ya halmashauri hiyo kinyume cha sheria.

 

Diwani wa kata hiyo iliyopo mpakani mwa Wilaya ya Biharamulo na Bukombe, alisema pamoja na askari hao kuendesha Operesheni ya wiki mbili ya kuwaondoa wavamizi wa maeneo ya hifadhi, kijiji hicho hakihusiki na uvamizi huo kwani kiko kihalali na  wananchi wake wameishi kwa siku nyingi katika maeneo hayo.

 

Alisema wananchi hao waliingia katika maeneo hayo kwa kununua kutoka Serikali ya kijiji ambayo iliwapimia kupitia kamati yake ya ugawaji wa ardhi na kuongeza kuwa ni hali ya kushangaza kuona askari hao  wanawafanyia unyama wa kuwaondoa kwa nguvu katika maeneo hayo.

 

Kufuatia hali hiyo wananchi hao pamoja na familia zao hawana mahala pa kuishi baada ya makazi yao kuchomwa moto na mengine kuharibiwa  na askari hao kutoka wilayani Biharamulo mkoani Kagera wakidai walikuwa wakiishi kwenye eneo la hifadhi ya halmashauri ya wilaya hiyo.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo,Richard Mbeho alisema operesheni hiyo ina lengo la kuwaondoa wavamizi haramu wa maeneo ya Serikali ambao waliingia kwenye hifadhi hiyo kwa ulaghai wa viongozi wa Serikali ya kijiji hicho ambao walikuwa wakiwauzia.

 

Imedaiwa kuwa wananchi hao waliingia kwenye eneo hilo kwa kuuziwa na viongozi wa Serikali ya kijiji cha Namalandula kwa gharama ya kati ya Sh1 hadi  Sh2 milioni kwa eneo lenye ukubwa wa hekari moja au mbili na wameishi kwa kipindi kirefu.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Amani Mwenigoha alisema suala hilo analo na analifanyia kazi kwa kuwasiliana na viongozi wa Wilaya ya Biharamulo ili kuona mipaka ya hifadhi hiyo na kijiji cha Namalandula kinachodaiwa kuwa ndani ya hifadhi  hiyo.

 

Mkuu huyo wa  wilaya aliyeongea kwa njia ya simu kutoka Dodoma alisema mara tu atakaporejea wilayani kwake atalishughulikia suala hilo ikiwa ni pamoja na kwenda kuwaona wananchi hao wanaodaiwa kuishi  msituni bila kuwa na nyumba za kuishi.

 

CHANZO MWANANCHI

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.