Imewekwa na Hamed Mazrouy

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharib Abdalla Mwinyi
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharib Abdalla Mwinyi

Kamati ya kutathmini zoezi la uondoshaji wa bandari ya forodha mchanga imekabidhi ripoti ya kamati hiyo kwa mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Mh, Abdallah Mwinyi Khamis ili iweze kufanyiwa kazi na kufikie malengo yaliyokusudiwa.

Akitoa maelezo kuhusu ripoti hiyo mwenyekiti wa kamati hiyo Nd, Ayoub Mohammed Mohammed amesema kuwa kamati hiyo ilipewa kazi ya kutathmini na kutoa mapendekezo kufuatia ziara ya Mh, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi aliyoifanya kwenye eneo hilo na kuona hali mbaya ya bandari hiyo.

Amesema kamati imewashirikisha wadau mbalimbali katika kupata taarifa wakiwemo wananchi kupitia shehia, wafanya biashara wa meli za mizigo na taasisi za serikali na hatimae kupata mapendekezo 10 yaliyomo katika ripoti hiyo.

Akieleza baadhi ya mapendekezo yaliyomo katika ripoti hiyo amesema ni pamoja na kusitishwa kwa shughuli zote zinazofanyika kwenye eneo hilo la forodha mchanga na kupendekeza eneo mbadala kuwa ni bandari ya Mtoni, na shughuli nyengine zinazofanywa kwenye eneo hili zirejeshwe katika ripoti hiyo.

Nae mkurugenzi wa mamlaka ya Mji mkongwe ambae pia ni mjumbe wa kamati hiyo Nd, Issa Sarboko Makarani amesisitiza kufuatwa sheria na taratibu zilizowekwa juu ya mpango mzuri wa mtumizi ya njia za Mji mkongwe ili kurejesha hadhi ya Mji wa Zanzibar .

Akizungumza mara baada ya kupokea ripoti hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mjini magharibi Mh, Abdallah Mwinyi Khamis aliipongeza kamati hiyo kwa kazi nzuri na kuahidi kuwa serikali ya mkoa wake itasimamia utekelezaji wa ripoti hiyo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa manufaa ya taifa.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.