Imewekwa na Hamed Mazrouy

Nahodha wa Jahazi ya Sun Rise  iliyozama kati ya Tanga na Mkokotoni Bwana Abdulla Saleh akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mkasa uliowapata wa kuzama baada ya chombo chao kupatwa na dhoruba kali.

Nahodha na abiria mmoja wakiwa miongoni mwa  watu 32 waliokuwa wakisafiri ndani ya  Jahazi lililopata ajali na kuzama liitwalo Sun Rise likitokea Mkoani Tanga kuja Mkokotoni Unguja wanaendelea kupatiwa  huduma za matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kaskazini A iliyopo Kivunge.

Jumla ya abiria 21 wameokolewa katika ajali hiyo na kupelekwa Kivunge kwa ajili ya kupatiwa huduma za matibabu ambapo hadi sasa abiria saba watoto wakiwa watatu na watu wazima wane  bado hawajapatikana kutokana na ajali hiyo.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Viongozi wa Juu wa Ofisi yake ambayo ndio inayoratibu masuala ya maafa walifika Hospitali ya Kivunge kuwapa pole majeruhi hao waliobakiwa wakipatiwa huduma za Matibabu.

Nahodha wa Jahazi hiyo Bwana Abdulla Saleh akiwa pamoja na Majeruhi mwenzake Bwana Ali Juma Jaku alimueleza Balozi Seif kwamba ajali hiyo ilitokea kutokana na kuchafuka mara Moja hali ya Bahari.

Nahodha Abdulla alisema chombo chao chenye uwezo wa kubeba abiria 50 kiliondoka bandarini Tanga salama Majira ya Saa nane za Usiku  na walianza kupata mitihani na kuzama mara baada ya kuchafuka kwa bahari majira ya saa 11 za alfajiri.

Akiwapa pole majeruhi hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maafa Zanzibar Balozi Seif alisema juhudi alizoonyesha Nahodha huyo katika kusaidia uokozi huo zinastahiki kupongeza na Jamii yote.

Balozi  Seif aliwaombea majeruhi hao kupoa haraka na kuungana na familia zao na kuutaka Uongozi wa Hospitali ya Kivunge kuendelea kuwachunguza Mareruhi hao kutokana na juhudi kubwa waliyoifanya ya kusaidia harakati za uokozi wa wenzao uliopelekea kupoteza nguvu nyingi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimfariji Abiria Juma Ali Jaku wa Jahazi ya Sun Rise iliyopata ajali na kuzama  kati ya Tanga na Mkokotoni ikiwa imebeba Abiria 32 kati ya hao 21 wameokolewa na saba hadi sasa hawajapatikana.

Jahazi hilo la Sun Rise lililokuwa likitokea Tanga kuja Mkokotoni mbali ya kuchukuwa abiria pia lilibeba sanduku nne za maziwa pamoja na  Polo zipatazo 30 za Mkaa.

Othmna Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

31/1/2013.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.