HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR,

MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI KATIKA UFUNGAJI WA MKUTANO WA KUMI WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR,
TAREHE 29 JANUARI, 2013

1.                    Mheshimiwa Spika, nianze hotuba yangu hii kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu mwingi wa Rehema, kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha kukutana katika Mkutano huu wa Kumi wa Baraza la Wawakilishi, mkutano ambao umefanyika kwa maelewano makubwa sana. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuiweka nchi yetu katika hali ya amani, salama na utulivu na kutuwezesha kupiga hatua kubwa za kimaendeleo ya kijamii na kiuchumi.

 

2.                    Mheshimiwa Spika, nakupongeza kwa dhati wewe Mwenyewe pamoja na wasaidizi wako wakuu, ambao ni Naibu Spika na Wenyeviti wa Baraza kwa kuendelea kuliongoza Baraza letu kwa busara, hekima, umakini, na ufanisi mkubwa na kufuata vyema misingi ya kidemokrasia na Kanuni za Baraza. Nachukua fursa hii pia kuwapongeza Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati mbali mbali za kudumu za Baraza kwa kutekeleza majukumu yao kwa hekima kubwa, na kwa haki na uadilifu lengo likiwa kuliwezesha Baraza lako Tukufu kutekeleza majukumu yake ya kusimamia shughuli za Serikali na kuona kwamba shughuli hizo zinaendeshwa vizuri na kwa uadilifu.

 

3.                    Mheshimiwa Spika, kwa aina ya kipekee, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuendelea kuiongoza nchi yetu kwa umakini mkubwa, hekima, busara na uadilifu.  Uongozi wa Mheshimiwa Rais ndio chachu ya maendeleo tunayoendelea kuyapata katika nyanja za kijamii na kiuchumi.  Sote ni mashahidi jinsi Rais Shein anavyoonyesha kwa vitendo utendaji bora katika Serikali na kuhimiza watendaji kubadilika na kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea, ingawa bado kwa baadhi ya watendaji tabia hii inawapa taabu kuiacha.  Nawaomba sana waiache tabia hiyo.  Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na tunamuomba Mwenyezi Mungu amzidishie hekima, afya njema na uwezo wa kuiongoza nchi yetu.  Amin.

 

4.                    Mheshimiwa Spika, pia nampongeza sana Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad kwa kumsaidia vizuri Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mashirikiano makubwa anayompa katika kuiendesha nchi yetu.  Natoa shukrani nyingi kwa Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi kwa namna wanavyotekeleza majukumu yao ya msingi ya kuwasilisha mawazo ya wananchi waliowachagua na pia kwa kusimamia vyema utendaji wa Serikali yetu ili kuona utendaji bora wa Serikali katika kukuza uchumi wa nchi na kutoa huduma kwa jamii ya Wazanzibari.  Vile vile, nawapongeza sana Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya na Watendaji wote wa Serikali kwa kuendelea kuchapa kazi na kuiletea maendeleo nchi yetu.

 

5.                    Mheshimiwa Spika, nina kila sababu ya kuvipongeza na kuvishukuru Vyombo vya Habari vyote hapa Zanzibar, hasa Shirika la Habari la Zanzibar (ZBC) kupitia Redio na Televisheni ambavyo viliendelea kurusha moja kwa moja maendeleo ya shughuli za Baraza yalivyokuwa yanakwenda na kuwawezesha wananchi wetu kufuatilia kwa makini hoja, michango na mijadala iliyoendeshwa Barazani. Kwa furaha kubwa nawapongeza na kuwashukuru wakalimani wa lugha ya alama kwa kazi zao nzuri walizozifanya kutafsiri mijadala kwa ishara ili wananchi wetu wenye ulemavu wa kutokusikia, nao waweze kufuatilia mijadala ya Baraza.

 

 

MASUALA MUHIMU YALIYOJIRI NCHINI:

6.                    Mheshimiwa Spika, kama sote tunavyoelewa nchi yetu imo katika harakati za mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tume ya Maoni ya Mabadiliko ya Katiba tayari imemaliza kazi yake ya kukusanya maoni kutoka kwa wananchi na Taasisi mbali mbali hapa Zanzibar na Tanzania Bara na pia imeshakamilisha zoezi hilo kwa upande wa Viongozi. Nachukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza sana wananchi wote Unguja na Pemba kwa kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao. Sasa ni kazi ya Tume kufanya uchambuzi wa maoni ya wananchi na naamini kabisa kwa uwezo wa Wajumbe wa Tume hiyo nchi yetu itapata Katiba mpya yenye kukidhi matakwa ya wananchi walio wengi na ambayo itaendeleza umoja na mshikamano wetu na kudumisha muungano wa nchi yetu. Wakati Tume inaendelea na kazi zake za kuandaa rasimu ya Katiba, nawasihi wananchi wote tuwe wastahamilivu na tuendelee kuchapa kazi ili tuweze kuiletea nchi yetu maendeleo kwa faida ya wananchi wetu na kwa faida ya vizazi vyetu vijavyo.

 

7.                    Mheshimiwa Spika, katika mwezi wa Agosti, 2012 nchi yetu ilikuwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makaazi, zoezi ambalo limefanyika kwa mafanikio makubwa licha ya kujitokeza changamoto katika baadhi ya maeneo. Matokeo ya Awali ya Sensa hiyo yalitangazwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 31 Disemba, 2012 katika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam. Matokeo hayo yanaonyesha kwamba Tanzania hivi sasa tupo watu 44,929,012 na Zanzibar tumefikia watu 1,303,560.  Kwa upande wa Zanzibar, idadi hii ya watu ni kubwa na kwa kweli tunahitaji kuwa na mipango madhubuti ya kudhibiti ongezeko la kasi la idadi ya watu.  Sasa inatulazimu kuongeza bidii katika kufanya kazi na kuzalisha kwa wingi bidhaa zitakazokidhi mahitaji yetu ya ndani na kupata ziada ya kuuza nje. Vile vile, tutahitajika kuimarisha huduma za jamii, ikiwemo elimu, afya, upatikanaji wa maji safi na salama na makaazi. Nawasihi Viongozi wote katika ngazi zote na  wananchi kwa ujumla tuzidishe mashirikiano na tuzidishe ari ya kujituma na kuwajibika zaidi katika maeneo yetu ya kazi katika sekta ya umma na sekta binafsi.

 

8.                    Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sensa ya 2002, Zanzibar ilikuwa na watu wapatao 980,000.  Katika Sensa ya 2012, miaka kumi baadae, Zanzibar inayo watu 1,303,560.  Ongezeko la watu 323,560.  Hili ni ongezeko kubwa sana.  Hatuna budi sasa tufanye maarifa ya kupunguza kasi ya kuzaliana ili watoto wetu tuwalee vizuri zaidi.

 

9.                    Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Januari, 2013, nchi yetu iliadhimisha miaka 49 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Katika maadhimisho hayo, miradi 53 ya maendeleo iliwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa. Miradi hiyo inathamani ya wastani wa Shilingi bilioni 97 na ilikuwa katika sekta ya elimu, maji safi na salama, afya, kilimo, uvuvi na miundombinu ya habari, mawasiliano na barabara. Hii ni hatua kubwa ya maendeleo ambayo nchi yetu imepiga katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Nachukua nafasi hii kuwashukuru kwa dhati Viongozi katika ngazi zote na wananchi wote kwa kushirikiana katika kufanikisha sherehe zetu hizi adhimu ambazo zilifana sana.

 

10.               Vile vile, nawashukuru makamanda na askari wa vikosi vyetu vya ulinzi, Wajumbe wa Kamati ya Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho na Wanafunzi walioshiriki katika halaiki na maandamano na Wanahabari kwa kazi nzuri waliyoifanya ambayo imetuletea mafanikio makubwa katika maadhimisho ya Mapinduzi yetu.  Hivi sasa tunakabiliwa na maandalizi ya maadhimisho ya Mapinduzi ya kutimiza miaka 50 (nusu karne) ifikapo tarehe 12 Januari, 2014. Ni imani yangu viongozi sote na wananchi tutaendelea kushirikiana ili kuzifanya sherehe zetu hizo kuwa za mfano na za hadhi ya juu kulingana na umuhimu na hadhi ya Mapinduzi yetu.

 

11.               Mheshimiwa Spika, hivi karibuni nilipata fursa ya kuzindua utekelezaji wa Mradi wa TASAF Awamu ya Tatu hapa Zanzibar. Mradi huu unatekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar na una jumla ya Shilingi Bilioni 470 ambazo zitatumika kusaidia kaya masikini kwa kipindi cha miaka mitano (5) ijayo. Naomba niwaelekeze watendaji wote watakaohusika na utekelezaji wa mradi huu kufanya kazi kwa makini, bidii na uadilifu ili kuhakikisha malengo na matarajio ya mradi huu yanafikiwa. Viongozi kwa upande wao hawana budi kuwahamasisha wananchi katika maeneo yao kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huu, ikiwa ni pamoja na kubuni miradi mbali mbali itakayokuwa na manufaa kwao.

 

12.               Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali zetu kuandaa mradi huu ni kutekeleza kwa vitendo ahadi zake kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015 ya kuwawezesha wananchi kiuchumi na kupunguza makali ya umasikini. Nachukua nafasi hii kuwapongeza sana wananchi wa Unguja na Pemba na viongozi na watendaji wote walioshiriki katika utekelezaji wa TASAF Awamu ya Pili kwa kazi nzuri walizofanya na kupelekea kupata mafanikio makubwa ya mradi huu ambayo yamewafurahisha Wahisani wetu ambao ni Benki ya Dunia, Shirika la Misaada la Uingereza (DFID) na USAID na kufikia maamuzi ya kutusaidia tena katika Awamu hii ya tatu. Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, nawashukuru kwa dhati Wahisani hao kwa misaada yao mikubwa kwa Tanzania na kwa Zanzibar.

  

 MAMBO MUHIMU YALIOJITOKEZA BARAZANI:

13.               Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu wa 10 wa Baraza lako Tukufu, Waheshimiwa Mawaziri wamewasilisha miswada minne (4) ya sheria ambayo ina umuhimu mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu. Miswada iliyowasilishwa na kupitishwa na Baraza lako tukufu ni:

                                           i.            Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ruzuku kwa Vyama vya Siasa Nam. 6 ya mwaka 1997.

                                         ii.            Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Usafiri Nam. 5 ya mwaka 2006.

iii.            Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Shirika la Utangazaji Zanzibar Kazi, Majukumu na Utawala wake pamoja na Mambo mengine Yanayohusiana na Hayo.

iv.            Mswada wa Sheria ya Kuanzishwa kwa Shirika la Meli Zanzibar Kazi, Uwezo na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.

 

14.               Mheshimiwa Spika, Mswada wa kwanza uliojadiliwa ni Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ruzuku kwa Vyama vya Siasa na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo Nam. 6 ya mwaka 1997. Marekebisho ya Sheria hii yana lengo la kuimarisha demokrasia nchini mwetu pamoja na kuviongezea uwezo vyama vya siasa kushiriki katika chaguzi zote zinazoendeshwa nchini.  Mgawanyo wa ruzuku hiyo kwa Vyama vya Siasa utafanywa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa baada ya Mheshimiwa Rais kuweka saini sheria hiyo.

 

15.               Mheshimiwa Spika, Mswada wa Pili uliojadiliwa na Baraza lako Tukufu ni Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Usafiri wa Baharini Nam. 5 ya mwaka 2006. Mswada huu unakusudia kuweka mazingira bora ya udhibiti wa masuala ya usafiri wa baharini na kuhakikisha kuwa yanatekelezwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria hii. Marekebisho ya Sheria hii yamezingatia maeneo mbali mbali ikiwemo suala la umri wa meli kutumika kwake tangu ilipoundwa ambayo itaruhusiwa kuingia nchini. Aidha, suala jengine lililozingatiwa ni kutobadilisha uasili wa meli kutoka kwenye uasili wa meli ya kubeba mizigo na kuwa meli ya abiria.  Lengo hasa la Mswada huu ni kuwalinda wananchi kutokupoteza maisha yao kutokana na ajali zisizo na sababu.

 

16.               Mheshimiwa Spika, pia marekebisho ya sheria hii yana lengo la kuweka uwiano na mashirikiano mazuri kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha usalama wa usafiri baharini kutokana na kwamba meli zinasafiri pande zote mbili za Muungano. Haya yote ni maudhui yaliyozingatiwa kwenye marekebisho ya Sheria ya Usafiri wa Baharini.

 

17.               Mheshimiwa Spika, marekebisho ya sheria hii pia yanalenga kuweka utaratibu mzuri wa usafiri wa abiria na mizigo kwa vyombo vya baharini na hivyo kuondoa sababu za kibinadamu zinazosababisha ajali.

18.                Mheshimiwa Spika, Mswada mwengine uliowasilishwa na kujadiliwa kwenye Baraza lako Tukufu ni Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Shirika la Utangazaji Zanzibar, Kazi, Majukumu na Utawala wake pamoja na Mambo mengine yanayohusiana na hayo. Mswada huu unakusudia kufuta Tangazo la Sheria Nam. 111/2011 la kuanzisha Shirika la Utangazaji Zanzibar pamoja na kazi na majukumu yake.

Umuhimu wa kuanzisha upya Shirika hilo umekuja kutokana na haja ya kuwa na chombo kimoja tu kitakachosimamiwa na kuendeshwa na uongozi wa aina moja tu ambao ni Mkurugenzi Mkuu mmoja, Mhariri Mkuu mmoja, Mhandisi Mkuu mmoja na Meneja wa Vipindi. Utaratibu huu wa sheria hii utaliimarisha Shirika pamoja na kuleta ufanisi zaidi.

 

19.               Mheshimiwa Spika, Wajumbe wa Baraza lako wakati wakijadili mswada huu walisisitiza sana umuhimu wa kuwepo na wataalamu wa fani mbali mbali watakaoweza kuliendesha Shirika letu la Utangazaji kwenye mazingira yaliopo sasa ya kiushindani kwa lengo la kuwavutia wananchi.

 

20.               Mheshimiwa Spika, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako pamoja na wananchi kwamba Serikali imejipanga vyema katika kuliimarisha shirika kimajengo, vifaa na wataalam, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu hao.

 

21.               Mhesimiwa Spika, Serikali imo kwenye hatua zake za mwisho za kuondoka kwenye matumizi ya analogia na kwenda kwenye dijitali. Ni dhahiri kwamba matumizi ya mfumo wa dijitali yanahitaji utaalamu wa hali ya juu unaoendana na ubunifu ili Shirika hili liweze kusonga mbele kwa kutoa habari za kisiasa, kiuchumi na kijamii za ndani na nje ya nchi. Serikali itayazingatia sana maslahi na marupurupu ya wafanyakazi wa Shirika ili kuwajengea mazingira mazuri ya kuweza kuwajibika ipasavyo na kuweza kulibadilisha kwa kuimarisha huduma zake ili ziwe nzuri na za haraka zaidi.  Serikali pamoja na wananchi kwa ujumla wana mategemeo makubwa ya kuona Shirika hili linabadilika sana na kuondokana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea. Huu sasa ni wakati wa kutoa huduma za kiushindani, kutafuta wateja na kubuni mambo mbali mbali ili kuweza kukidhi mahitaji ya walengwa.

 

22.               Mheshimiwa Spika, tunakusudia Shirika hili lijiendeshe kibiashara, hivyo kila atakayetumia huduma zake, ikiwa ni pamoja na Baraza la Wawakilishi, itawalazimu kuzilipia huduma hizo.

 

23.               Mheshimiwa Spika, Mswada wa Nne uliojadiliwa katika Mkutano huu wa 10 wa Baraza lako ni Mswada wa Sheria ya Kuanzishwa kwa Shirika la Meli Zanzibar Kazi, Uwezo na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.

 

24.               Mheshimiwa Spika, Shirika la Meli hapo awali liliundwa kwa mujibu wa Amri ya Rais iliyotolewa mwaka 1983 chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma Nam. 4 ya mwaka 1978 ambayo imeshafutwa na kwa sasa Mashirika yote ya Umma yanasimamiwa na Sheria ya Mitaji ya Umma Nam. 4 ya mwaka 2004. Mswada uliopitishwa na Baraza lako unakusudia kutekeleza Sera ya Usafiri ya Zanzibar pamoja na Mpango Mkuu wa Usafiri wa mwaka 2008 na kuliwezesha Shirika jipya la Meli kutoa huduma za usafiri zilizo bora na zinazoendana na matwaka ya viwango vya ushindani wa Kitaifa na Kimataifa.

 

25.               Mheshimiwa Spika, Serikali ina lengo la kuwa na usafiri wa baharini ulio bora zaidi na endelevu hapa Zanzibar. Sote tunaelewa jinsi nchi yetu ilivyokumbwa na misiba mikubwa kutokana na kukosa usafiri wa baharini wa uhakika. Nchi yetu ni ya visiwa ambapo usafiri mkubwa unaotumiwa na wananchi walio wengi ni kwa njia ya bahari. Serikali yetu imeanza kuchukua jitihada za hali na mali za kuweza kuagiza meli kubwa, ya uhakika na itakayoweza kuchukua abiria wengi na mizigo kwa usalama. Kwa mantiki hiyo, Serikali imekusudia kuanzisha Shirika la Meli litakaloimarisha huduma za meli kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kijamii, kiuchumi na kibiashara. Aidha, Shirika litasimamia uendeshaji wa meli zetu kitaalamu na kibiashara ili ipatikane tija na faida ya kuliimarisha shirika hilo. Serikali itachukua hatua za kuhakikisha kwamba Shirika hili linapatiwa wataalamu na kuendeshwa kwa ufanisi

.

26.               Mheshimiwa Spika, Sheria hizi zote zimetungwa na Baraza lako Tukufu kwa nia ya kuwatumikia wananchi.  Ningependa kuwasihi watekelezaji wa sheria hizo wazisimamie na kuhakikisha kuwa zinatekelezwa ipasavyo, bila ya kumuonea haya au aibu mtu yoyote atakayezikiuka sheria hizi.

 

27.               Mheshimiwa Spika, mara nyingi Wajumbe wa Baraza lako Tukufu wamekuwa wakilalamika kuwa sheria nyingi zimetungwa lakini kumekuwa na udhaifu wa kusimamia utekelezaji wake.  Nakubaliana na malalamiko hayo.  Hii ni kwa sababu wasimamizi wa sheria zinazotungwa hawawajibiki ipasavyo.  Kwa mfano, tuangalie, usimamizi wa Sheria ya Usalama Barabarani.  Hausimamiwi vizuri na wahusika.  Utaona waendesha baiskeli wakiendesha baiskeli zao usiku bila taa, magari yanaendeshwa usiku bila namba (Number plates), hatujui madhumuni yake ni nini, wapanda mapiki piki hawavai kofia za kinga (helmet), wanaosimamia sheria hizi wapo lakini wanaangalia tu.  Nawaomba sasa watekelezaji na wasimamizi wa sheria hizi watimize wajibu wao.  Huu ni mfano mmoja tu.

28.               Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuimarisha uchumi na kuimarisha shughuli za uwakala, Serikali inaendelea na juhudi zake za kutafuta Washirika wa Maendeleo na wawekezaji watakaochangia ujenzi wa bandari mpya ya kibiashara ya Mpiga Duri, ili Serikali iweze kuongeza mapato yake kutokana na meli kubwa zitakazotumia bandari hiyo.

 

29.                Mheshimiwa Spika, Baraza lako Tukufu liliunda Kamati Teule ya Kuchunguza utendaji wa Shirika la Umeme na Kamati Teule ya Kuchunguza Utendaji wa Baraza la Manispaa. Nawapongeza kwa dhati Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati hizi kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kufuatilia kwa kina masuala mbali mbali kwa mujibu wa hadidu rejea walizopewa na kuwasilisha ripoti zao katika Baraza hili.  Nawashukuru Wenyeviti wa Kamati hizo kwa umakini wao na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu utendaji katika Taasisi hizo.

 

30.               Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Baraza lako Tukufu kwamba Serikali imepokea ripoti hizo za Kamati Teule zilizowasilishwa katika Baraza na itazifanyia kazi taarifa hizo pamoja na mapendekezo yake kwa umakini mkubwa na kuchukua hatua kadri itakavyoonekana inafaa. Nirudie kuwapongeza Viongozi na Wajumbe wote wa Kamati hizi kwa kazi kubwa waliyoifanya, ambayo Serikali inathamini sana kazi yao hiyo yenye lengo la kuimarisha utendaji na uwajibikaji Serikalini.  Ningependa kuwahakikishia Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwamba wale wote waliotajwa kwenye ripoti hiyo watashughulikiwa vipasavyo kwa kuzingatia haki na utawala bora.  Kama baadhi ya Wajumbe walivyosema, aliyekuwemo hatoki na asiyekuwamo hataingia.

 

31.               Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, jumla ya maswali 72 ya msingi na maswali ……… ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wawakilishi na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri husika. Nawapongeza sana Waheshimiwa Wajumbe kwa kuja na maswali mazuri yenye lengo la kujenga zaidi na kuimarisha uwajibikaji wa watendaji wa Serikali. Aidha, nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa majibu yao ya kina ambayo hatimaye yaliwaridhisha Waheshimiwa Wajumbe.

32.               Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako na wananchi wote wa Zanzibar kwamba Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa, inayoongozwa na kiongozi makini, Dkt. Ali Mohamed Shein inafanya kazi kubwa ya kuiletea nchi yetu maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha huduma za jamii.  Katika kufanikisha hayo, Serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha sekta za uzalishaji, zikiwemo za kilimo, mifugo na uvuvi, kuimarisha sekta ya viwanda, utalii na biashara na kuendeleza sekta ya miundombinu nchini. Vile vile, Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya elimu, afya na kuhakikisha wananchi wote wa mijini na mashamba wanapata maji safi na salama kwa kuimarisha afya zao na kuwa na nguvu kazi bora itakayoshiriki katika kukuza uchumi wetu. Lengo kuu la jitihada hizi ni kukuza uchumi na kupunguza umasikini katika nchi yetu.

 

33.               Mheshimiwa Spika, ili tuweze kufanikiwa katika jitihada zetu hizi, ni lazima sote tuwajibike katika kutunza mazingira yetu. Hatuna budi sote kwa pamoja kushiriki kikamilifu katika upandaji wa miti, utuzanji wa misitu yetu ya asili na kuachana na tabia ya kuchimba mawe na mchanga ovyo bila ya vibali na kutupa taka ovyo. Aidha, nawataka wafanya biashara ambao bado wanaendelea na tabia ya kuingiza mifuko ya plastiki nchini waachane na tabia hiyo mara moja kwani kuendelea kufanya hivyo ni kuhatarisha afya zetu na vizazi vyetu. Uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kutunza mazingira kwa manufaa ya nchi yetu.

 

 

UNUNUZI WA MELI:

34.               Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu wakati wa kufunga Mkutano wa Nane wa Baraza lako Tukufu nilieleza juhudi inayofanywa na Serikali za kununua meli mpya, kubwa ya abiri itakayokidhi mahitaji ya usafiri wa baharini katika Visiwa vyetu na katika maeneo ya mwambao wa nchi jirani.  Napenda kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba Serikali imekwisha chukua hatua hizo na hivi karibuni Serikali itatiliana saini mkataba na Kampuni ya Damen ya Uholanzi itakayotengeneza meli hiyo.  Mheshimiwa Spika, meli hiyo itakuwa na uwezo wa kuchukua abiria wapatao1,200 na mizigo yenye uzito wa tani 200.  Meli hiyo itachukua miezi 18 kutengenezwa baada ya mkataba kuwekwa saini na pande mbili hizo.  Hivyo, wananchi wa Zanzibar wategemee, kama mambo yote yatakwenda sawa, kupata meli mpya mnamo robo ya mwisho ya 2014, ingawa inawezekana ikawa zaidi kabla ya hapo.

 

35.               Mhesimiwa Spika, kwa mara nyengine tena naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, Wajumbe wa Baraza lako, Waandishi wa Habari na wananchi wote kwa mashirikiano makubwa katika kuliendesha Baraza letu kwa mafanikio. Kadri siku zinavyoendelea mbele, wananchi wanazidi kujenga matumaini makubwa na Baraza hili na Serikali yao na hii ndio ishara ya kukua kwa utawala wa demokrasia nchini.

 

36.               Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba kutoa hoja ya kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi siku ya Jumatano, tarehe 3 April, 2013 saa 3.00 barabara za asubuhi panapo majaaliwa.

 

37.               Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.