Imewekwa na Hamed Mazroy

 

WATOTO wawili wa familia moja wamefariki dunia baada ya kuunguzwa na kuteketezwa na moto wakiwa ndani ya nyumba yao, iliyopo kwenye Kijiji cha Lemkuna Kata ya Ngorika Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Manyara.

Akithibitisha kutokea kwa vifo hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi, Akili Mpwapwa alisema tukio hilo lilitokea Januari 24 mwaka huu saa 5:49 asubuhi kijijini hapo.

Kamanda Mpwapwa aliwataja watoto hao waliofariki dunia kuwa ni Manase Mathayo (6) na Henlyghty Mathayo mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu ambao waliungua kwenye nyumba yao wakiwa peke yao.

“Baada ya tukio hilo nilimuagiza Mkuu wa Kituo cha Polisi Mirerani, Mrakibu wa Polisi Ally Mohamed Mkalipa afuatilie na kuchunguza tukio hilo ili kubaini chanzo cha moto huo na namna ajali ilivyotokea,” alisema Kamanda Mpwapwa.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni moto uliokuwa unawaka ulichoma majani nje ya nyumba kushika kasi na kuchoma nyumba hiyo ya nyasi ambayo kwa muda huo ilikuwa na watoto hao wawili peke yao.

Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha Manase alikuwa nje ya nyumba na baada ya moto huo kuchoma nyumba ulimkuta mdogo wake aliyekuwa amelala ndani kwenye chandarua na yeye aliingia ndani wakakutwa wamekumbatiana.

“Baadhi ya watu waliokuwa jirani na eneo hilo walifika mara moja kwa ajili ya kutoa msaada kwenye nyumba hiyo, lakini walishindwa na kukuta watoto hao na mali zilizokuwepo zimeteketezwa kwa moto,” alisema Kamanda Mpwapwa.

Alisema wakati ajali hiyo ikitokea, baba wa watoto hao, Samwel Mathayo na mama yao walikuwa wamekwenda kulima shamba la mahindi lililopo pembeni ya Mto Ruvu uliopita katika kijiji hicho.

CHANZO MWANANCHI

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.