Imewekwa na Hamed Mazrouy

Rais wa Zanzibar akizungumza na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania aliefika Ikulu Zanzibar
Rais wa Zanzibar akizungumza na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania aliefika Ikulu Zanzibar

MAREKANI imeeleza kuvutiwa kwake na mafanikio yaliopatikana katika miradi inayoiendesha hapa Zanzibar na kuahidi kuunga mkono miradi mengine ikiwemo miradi mipya ya Changamoto ya Milenia (MCC) awamu ya pili  baada ya   Tanzania kufanikiwa katika awamu hiyo ambapo Zanzibar nayo itafaidika.

Maelezo hayo yametolewa leo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe. Alfonso Lenhardt akiwa na ujumbe wake wakati walipokuwa na mazungumzo na Rais wa   Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar .

Balozi huyo alieleza kuwa Marekani inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Zanzibar na kusisitiza kuwa itaendelea kuiunga mkono katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inayoisimamia ukiwemo mradi mkubwa wa umeme inafanikiwa.

Katika maelezo yake, Balozi huyo alisifu juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kupambana na Malaria pamoja na kuimarisha sekta zake za maendeleo huku akieleza jinsi hatua zinazochukuliwa na Ubalozi wake katika kuitangaza Zanzibar nchini mwake kutokana na amani na utulivu uliopo ikiwa ni miongoni mwa hatua za kuutangaza utalii wa Zanzibar .

Katika mazungumzo hayo, Balozi  Lenhardt alitoa nafasi kwa wajumbe aliofuatana nao ambao ni Wakurugenzi wa Miradi mbali mbali inayoendeshwa na Marekani nchini Tanzania kutoa ufafanuzi wa miradi wanayoisimamia hapa nchini.

Kwa upande wa mradi wa MCC, Mkurugenzi Mkaazi wa Mradi huo nchini Tanzania Bwana Karl Fickenscher, alieleza maendeleo yaliofikiwa katika  mradi mpya wa umeme kutoka Ras Kiromoni hadi Fumba ambapo tayari ulazaji waya umeshakamilika na uwekaji nguzo pamoja na uwekaji waya kutoka Fumba hadi mtoni umefikia hatua nzuri na kueleza mategemeo ya kazi za mradi huo kumalizika mwishoni mwa mwezi ujao.

Aidha, Mkurugenzi huyo alieleza maendeleo yaliofikiwa katika ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 35 huko kisiwani Pemba na kusisitiza kuwa suala la ubora wa barabara hizo limezingatiwa sana ili ziweze kutumika kwa muda mrefu.

Pia, alisisitiza kuwa hivi sasa ni wakati muwafaka kwa Zanzibar kuunda timu iliyoimara kwa kushirikiana na ndugu zao wa Tanzania Bara katika kutekeleza miradi ya awamu ya pili ya MCC baada ya kufanikiwa kutokana na vigezo vilivyowekwa na MCC.

Nae Mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Marekani USAID, Bi Sharon Cromer alieleza kuwa  Shirika hilo limeweza kupata maendeleo makubwa katika kuiunga mkono Tanzania ikiwemo Zanzibar katika kusimamia na kuendesha shughuli mbali mbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo uzazi wa mpango, Malaria, uundaji wa Sera, Kilimo, Utumiaji wa Raslimali, Elimu, Lishe,Uhifadhi wa Mazingira pamoja na Utalii.

Alieleza kuwa hivi sasa Shirika hilo limo katika kutekeleza mikakati ya miaka mitano katika kuimarisha misaada juu ya sekta hizo wanazozishughulikia ambapo pia wana dhamira ya kuendeleza mafunzo ya uongozi kwa sekta mbali mbali.

Nae Mkurugenzi Mkaazi wa Huduma za kujitolea za Wamarekani “US Peace Corps- Tanzania’, Bi Elizabeth O’ Malley, alielezea maendeleo yaliofikiwa katika sekta mbali mbali ambazo Marekani imekuwa ikisaidia kwa kuleta wafanyakazi wa kujitolea na kushiriki katika kutoa misaada kwenye sekta za maendeleo ikiwemo elimu.

Kwa upande wa sekta ya elimu Mkurugenzi huyo alieleza kuwa hivi sasa tayari wako walimu wane kisiwani Pemba wanafundisha lugha ya Kiengereza na bado ameahidi kuleta wafanyakazi wa kujitolea wakiwemo walimu wa sayansi hasa hisabati katika skuli mbali mbali za Unguja na Pemba .

Mwakilishi wa Mpango wa Rais wa Marekani wa Dharura kwa Maradhi ya Ukimwi (PEPFAR), Bwana  Brian Rettmann alisifu jitihada za Tanzania ikiwemo Zanzibar katika kupambana na Ukimwi pamoja na Malaria.

Kutokana na juhudi hizo, Mwakilishi huyo alieleza haja ya kuongeza jitihada katika maeneo ambayo wanasaidia ikiwemo miradi ya kifua kikuu, uendeshahji wa tafiti kwa miradi mbali mbali. Aidha, alieleza kuwa Mpango huo utaimarishwa zaidi ili uweze kuleta mafanikio kupitia hospitali Kuu ya MnaziMmoja.

Nae Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Moahmed Shein  kwa upande wake alimueleza Balozi huyo pamoja na ujumbe aliofuatana nao kuwa Zanzibar inathamini sana ushirikiano kati yake na Marekani pamoja na juhudi zake za kuunga mkono miradi ya Zanzibar.

Aidha, Dk. Shein alimpongeza Balozi huyo wa Marekani nchini Tanzania kwa juhudi  anazozichukua katika kuhakikisha Zanzibar inaendelea kuungwa mkono na nchi hiyo.

Dk. Shein pia, aliwapongeza wajumbe hao aliofuatana nao kwa usimamiazi mzuri wa miradi mbali mbali pamoja na shughuli za maendeleo wanazozitekeleza hapa nchini pamoja na zile ambazo wameahidi kuzitekeleza.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliahuidi kuwa Zanzibar itaendelea kuiimarisha miradi yote inayoungwa mkono na Marekani na kuahidi kuunda timu iliyoimara na uzoefu katika kusimamia kwa umakini zaidi miradi ya awamu ya pili ya MCC nchini.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.