Na Hamed Mazrouy

Wananchi wa Shangani Lebanon wilaya ya Mjini Unguja walalamikia kikosi cha zima moto Zanzibar kwa kuchelewa kwao kufika katika eneo ambalo nyumba moja imeunguwa moto na kusababisha uharibifu wa mali kadhaa ndani ya nyumba hio.
Kwa mujibu wa watu waliofika mwanzo na kushuhudia tukio hilo likiwa ndio kwanza linaanza wameiambia Zanzubardaima kuwa kutokea kwa moto huo kumesababishwa na hitilafu ya umeme ilitotokea ndani ya nyumba hio katika ghorofa ya pili.
Watu hao wamesema kuwa kupata kwao ya tukio hilo kumekuja kutokana na wakaaazi wa nyumba hio kupiga kelele wakiomba kupatiwa msaada kutoka kwa wasamaria wema ili waweze kuuzima moto huo ambao ulikuwa unawaka kwa kasi kubwa, nao waliweza kufanikiwa kwa kushirikiana na Polisi Jamii na badae walipata nguvu zaidi kutoka kwa kikosi cha zima moto waliofika hapo.
Aidha wamesema kuwa moto uliotokea ndani ya nyumba hio umeharibu vitu kadhaa ndani ya nyumba hio vikiwemo nguo,kuta za nyumba hio na baadhi ya vitu vyengine ambavyo mpaka sasa haijajuulikana ni hasara ya kiasi gani.

Kwa upande wao maafisa wa kikosi cha zima moto waliofika hapo wamesema kuwa wao hawakuchelewa kufika hapo isipokuwa kutokana na tukio hilo kutokea katikati ya majumba pahala ambapo kuna ugumu wa kupita gari ni moja ya mambo yaliosababisha kuchelewa kuzimwa kwa moto huo,lakini pia walifanikiwa kuzuia moto huo kuendelea zaidi.
