Kituo cha stendi ya Abiria wanaosafiri kwa gari Chake chake Pemba
Kituo cha stendi ya Abiria wanaosafiri kwa gari Chake chake Pemba

MADEREVA wanaotumia barabara ya Mkoani – Chake chake, wamelalamikia vitendo vya baadhi ya waosha Gari, kufanya shughuli hiyo karibu na madaraja jambo ambalo linaweza kusababisha ajali zisizokuwa za lazima.

 

Madereva hao walisema, tabia hiyo imekuwa ikiwapa usumbufu na tabu wakati wanapofika maeneo hayo, kwa vile huwepo msururu wa gari zinazooshwa na kuwaziba wenzao wanapotaka kupishana.

 

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa wakati tofauti, madereva hao walisema, hali hiyo ambayo walishaipigia kelele kwa muda mrefu, bado haijapatiwa dawa na kuhatarisha usalama wao.

 

Walisema kuwa wajenzi wa barabara, wameweka maeneo maaluma karibu na daraja hizo ili kuzipa nafasi gari kupishana, ambapo sehemu hiyo ndio inayotumiwa na waosha gari jambo ambalo sio shahihi

 

Mmoja kati ya madereva hao Ali Mohamed Kombo alisema hali hiyo imekuwa ikiwababaisha hasa kwa vile zipo alama zinazowapa fursa dereva mmoja kumpisha mwenzake.

 

‘’Eneo ambalo dereva mmoja anapaswa kumpa nafasi mwenzake apite, ndio waosha gari wanapokaa kufanya hivyo, sasa huyu amabae nafasi yake imechukuliwa na muosha gari akae wapi’’,alihoji dereva huyo.

 

Nae Hassan Ali Said alisema hata wanapowaelekeza waosha gari hudai kua barabara ni ya watu wote, hivyo huwepo kutupiana maneno na kuendelea kazi yao hiyo jambo ni hatari kuwepo katika maeneo hayo.

 

Akizungumza kwa njia ya simu mmoja kati ya waosha gari ambae hakupenda jina lake lichapishwe gazetini alikiri kufanya hivyo na kueleza kuwa wamekuwa wakiacha nafasi kwa ajili ya gari kupishana.

 

Aliendeleza kueleza kuwa, pia huwa hawaweki zaidi ya gari mbili kwa wakati mmoja, na hata hivyo mmoja wao huwepo kwa ajili ya kuruhusu gari ama kuisimamisha ili kuondoa uwezekano wa kutokezea ajali.

 

Kwa upande wake Mhandisi Ujenzi wa barabara kutoka Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Pemba Khamis Massoud, alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kusema kuwa changamoto hiyo na nyengine katika maeneo hayo zipo.

 

Alisema kila daraja hujengewa eneo hilo (pass bay) la kumpa nafasi dereva ili kusita na kumruhusu mwengine ili kuepusha uwezekano wa kutokezea ajali zisizokuwa za lazima katika maeneo hayo.

 

Alieleza kuwa karibu na daraja huwepo alama mbili kubwa, moja ikiwa rangi nyekundu na upande mwengine rangi nyeupe, ambapo mwenye rangi nyengukundu kisheria ndie anaepaswa kusimama.

 

‘’Hilo la waosha gari ni tatizo, lakini hata kama hawapo madereva wenyewe hawaziheshimu alama za barabarani na hupishana katikati ya daraja, kama vile hakuma alama inayompa fursa mwengine’’,alieleza Mhandisi huyo.

 

Katika hatua nyengine alisema wanatarajia hivi karibuni, kukutana na waosha gari katika madaraja ya Mkata maini, meli mbili na maeneo mengine Kisiwani Pemba ili kuwaelimisha juu tabia hiyo mbaya.

 

Hata hivyo alisema, iwapo madareva watazifuata kikamilifu alama za barabarani hakuna sababu ya kutokeza ajili ya barabarani, kwani kila hatua ipo lama inayoelekeza usalama wa jambo fulani.

 

Maeneo ambayo ambayo waosha gari wamekua wakiendesha kazi hiyo na kulalamikiwa na madereva ni pamoja na Kigope Mtambile, Kimbuni, Mkatamaini Kipapo naMeli mbili Chake chake.

Na Haji Nassor, Pemba

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.