SIKU chache baada ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kufanya maandamano, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleman Kova, amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englbert Kiondo, kusimamia usalama wa hosteli za wanafunzi hao zilizoko Kigamboni.

Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Kova alisema amelazimika kutoa agizo hilo baada ya kuwepo kwa mvutano kati ya Kiondo na wanafunzi hao ambao walidai taarifa zote za uhalifu walizofanyiwa na kundi la vibaka kwenye hosteli zao zimeripotiwa katika kituo kidogo cha polisi Kigamboni.

Naye msimamizi wa hosteli mojawapo, aliyefahamika kwa jina la Sanfroza alieleza wazi kuwa anashangazwa na ripoti ya polisi kuwa matukio ya vitendo hivyo hayako katika orodha kwa sababu yote yameripotiwa ipasavyo.

“Tunachotaka sisi kwa sasa ni jeshi la polisi kuwajibika katika vitendo vyote vya uhalifu vilivyotokea hosteli, kwa sababu majina ya vibaka wote yameripotiwa polisi Kigamboni, iweje leo warushiane mpira wenyewe kwa wenyewe?” alihoji Sanfroza.

Wanafunzi hao walifanya maandamano Januari 14, mwaka huu, ambapo Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kiliingilia kati kwa kuwatawanya kwa mabomu ya machozi.

Pamoja na hilo, Kova aliahidi kutoa ufafanuzi wa matukio hayo wakiwemo vibaka waliohusika wawe ndani ya Dar es Salaam au nje ifikapo Januari 30, mwaka huu.

CHANZO TANZANIADAIMA

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.