
Benki ya damu Zanzibar inategemea kuanzisha zoezi la uchangiaji damu wa hiari kwa kupita maskuli pamoja na vyuo vinavyotoa elimu mbali mbali kwa lengo la kuichangia benki hiyo kutokana na upungufu wa damu kwa benki hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Afisa uhamasishaji wa benki ya damu wa jumuiya ya wachangiaji damu kwa hiari Bw Bakari Magarawa huko ofisini kwake amesema kua zoezi hilo ambalo litaanza mwishoni mwa mwezi ujao litasaidia kupunguza ukosefu wa huduma hiyo kwa ajili ya wagonjwa pamoja na mama wajawazito ambao hupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua.
Aidha amesema kua kupitia zoezi hilo la kupita skuli mbali mbali za sekondari kwa Unguja na Pemba pamoja na vyuo vya hapa Zanzibari kutasaidia kwa kiasi kikubwa ongezeko la damu katika benki ya damu ambayo inaonekana kuongezeka kwa watu wanaohitaji huduma hiyo siku hadi siku.
Hata hivyo amesema kua zaidi ya asilimia 95 ya damu zilizo kusanywa ni za wachangiaji wa hiari na kuwatoa wasiwasi wachangiaji wa damu kuwa itatolewa bila malipo kwa wagonjwa wote wanaohitaji huduma hiyo .
Bw Magarawa amewataka wanafunzi wa vyuo pamoja na skuli za hapa Zanzibar kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo ili kuweza kusaidia uchangiaji wa damu kwa lengo la kuokoa maisha ya wananchi.