MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Taifa Philip Mangula jana alionja machungu aliyowahi kupata Waziri Mkuu Mizengo Pinda baada ya msafara wake kuzomewa jijini Mwanza.

Msafara huo wa Mangula ulizomewa jana muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wake katika uwanja wa michezo Nyamagana.
Katika msafara huo mbali na Mangula pia walikuwapo Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri wa Ujenzi, Grayson Lwenge na Katibu Itikati na Uenezi, Nape Nnauye.

Mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo, baadhi ya wananchi waliokuwa katika mkutano huo ambao hawakuwa wamevalia sare za CCM, walijipanga kando ya barabara ya Posta na wakati viongozi hao wakipita waliwazomea huku wakionyesha ishara ya vidole viwili.

Kutokana na hali hiyo, vijana wa CCM maarufu kama Green Guard walianza kuvamia wazomeaji hao na kuanza kutembeza kipigo ambapo vijana wawili ambao majina yao hayakufahamika walijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili.

Septemba 17, mwaka jana, ndani ya uwanja wa Sahara, Pinda alizomewa na wananchi wakati akihitimisha ziara yake jijini Mwanza, kutokana  na kero nyingi zinazowakabili wakazi wa jiji hilo, huku kiongozi huyo akiwataka waachane na ushabiki wa kisiasa.

Awali, akihutubia mkutano huo, Mangula alisema pamoja na kwamba wapinzani wamekuwa wakibeza mafanikio ya ya CCM lakini ukweli utabaki palepale kwamba katika kipindi cha miaka 50 ya utawala huo nchi imepiga hatua za maendeleo.

Mangula alitoa mfano kuwa wakati wa miaka ya nyuma kulikuwa na ghorofa moja la hospitali ya Bugando na sasa yapo ‘mabugando’ mengi.

Mbali na kuelezea mafanikio hayo pia aliwataka wanachama wa CCM kutumia vikao katika mashina kuzungumza na wanachama kubainisha matatizo yanayowakabili badala ya kuzungumza nje ya vikao, jambo ambalo limekuwa likikigawa chama.

Hata hivyo, Mangula ambaye alikuwa akisubiriwa kwa hamu katika mkutano huo, tofauti na matarajio ya wengi hakuzungumza zaidi ya dakika tano.
Wakati akiondoka baadhi ya wananchi hao walisikika walilalamika kuwa walitarajia kusikia mengi lakini hakuna walichosikia.

Kutokana na hali hiyo wananchi hao waliamua kukaa kando ya barabara ya Posta, nje ya uwanja huo na kuanza kuwazomea viongozi waliokuwa wakipita.

CHANZO MWANANCHI

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.