ASKARI  walioshiriki katika operesheni ya kusambaratisha mkutano wa Chadema mkoani Iringa na kusababisha kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi, wanalalamika kwamba hawajalipwa posho zao zinazofikia Sh12,150,000.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana, zilisema  kiasi hicho cha fedha kilipaswa kulipwa kwa askari 27 waliotokea mkoani Dodoma kwa malipo ya Sh45,000 kwa siku kwa kila askari. Askari hao walikaa Iringa kwa muda wa siku kumi. Mmoja wa askari hao alisema hadi kufikia jana  askari wote waliotoka mkoani Dodoma,  walikuwa hawajalipwa posho zao za operesheni hiyo iliyofanyika Septemba mwaka jana. “Kutoka hapa tulienda (Iringa) askari 27, askari wa kawaida 24, masajenti wawili na inspekta mmoja. Wakati tunaondoka tuliambiwa kwamba posho zetu ambazo ni Sh45,000 kwa siku wangetutumia,” alisema askari huyo na kuongeza;

“Tulikaa Iringa kwa siku kumi, hivyo kila askari aliyekwenda kwenye operesheni ile, alipaswa kulipwa Sh450,000. Lakini bahati mbaya sana, baada ya kutokea mauaji yale hakuna mtu aliyelipwa mpaka sasa. Vocha zimeendikwa lakini hazijatolewa.”

Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema hana taarifa kuhusu  malipo hayo hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni mgeni mkoani humo.

“Hapa Dodoma mimi nimekuja siku za hivi karibuni na hilo suala la askari kutolipwa posho zao silijui na sifahamu kama kweli walikwenda huko ulikosema,” alisema Kamanda huyo na kuongeza: “ Naomba nipe muda zaidi nifuatilie ili kujua ukweli wake. Lakini pia nikuombe uwasiliane na mwandishi mwenzako aliyeko hapa Dodoma ili iwe rahisi mie kuwasiliana naye kuliko kuzungumza kwa simu tu.”

Mwangosi aliuawa kwa bomu Septemba 2, mwaka jana wakati polisi hao waliodaiwa pia kutoka Mikoa ya Morogoro na Mbeya, wakiwatawanya wafuasi wa Chadema, waliokuwa kwenye mkutano wa ndani katika Kijiji cha Nyololo mkoani Iringa.
Askari hao walikwenda mkoani Iringa kushirikiana na wenzao katika kudhibiti,  mikutano ya Chadema.

Mwangosi aliuawa kwa bomu alipokuwa akiwajibika katika kazi zake za kutafuta habari wakati wa ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kufanya mikutano ya ndani ya kuimarisha chama.

Ripoti ya kamati iliyoundwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuchunguza kifo hicho, ilisema Mwangosi aliuawa kwa makusudi na polisi chini ya usimamizi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.

CHANZO MWANANCHI

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.