WATU 21 wanahofiwa kufa maji katika Ziwa Tangayika baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kutoka katika Kijiji cha Kirando wilayani Nkasi, Mkoa wa Rukwa kuelekea Rumonge nchini Burundi kupasuka na kuzama katika eneo la Kijiji cha Herembe.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari katika eneo la tukio, nahodha wa boti na abiria walionusurika katika ajali hiyo, Kilimali Sefu na Muhamed Said walisema kuwa ajali hiyo imetokea jana majira ya saa saba usiku.

Walisema jumla ya abiria 85 walikuwemo katika boti hiyo inayojulikana kwa jina la Yarabi Salama na kati yao 64 wameokolewa na 21 wamefariki dunia. Maiti tisa zimepatikana na 12 hazijulikani zilipo.

Kwa mujibu wa mashuhuda hao, chanzo cha ajali hiyo ni upepo mkali uliotokea katika eneo hilo la Herembe na kusababisha mashine ya boti kushindwa kufanya kazi.

Boti hiyo ilikuwa imebeba idadi kubwa ya abiria na tani 45 za mihogo, dagaa na samaki, waliokuwa wakisafirishwa kwenda Rumonge, nchini Burundi.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Herembe, Joka Mpapi na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Adam Makuka wamelalamika kukosekana vifaa vya uokoaji, lakini waliwashukuru wananchi kwa jitihada walizofanya za kusaidia kuokoa.

Akizungumza na wananchi katika eneo la ajali, Mkuu wa Mkoa Kigoma, Luteni Kanali mstaafu Issa Machibya, aliwataka wananchi kuwa makini na usafiri wa majini na kuchukua tahadhari ya kupakia mizigo na abiria kulingana na uwezo wa boti.

“Hivi sasa kuna mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa imebadilika sana, lazima mchukue tahadhari mnaposafirisha bidhaa zenu, mbebe abiria na mizigo kulingana na uwezo wa boti husika,” alisema Machibya.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Maweni.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.