MAKAMU wa Kwanza wa rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiondoa pazia kuashiria ufunguzi wa skuli mpya ya Sekondari ya inayoitwa Dk. Omar Ali Juma, ilipo Wawi Chake chake Pemba, ambayo ina vyumba kumi na mbili, vyumba vitatu vya maabara na ukumbi wa mkutano ikiwa ni mkopo kutoka benki ya Dunia
MAKAMU wa Kwanza wa rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiondoa pazia kuashiria ufunguzi wa skuli mpya ya Sekondari ya inayoitwa Dk. Omar Ali Juma, ilipo Wawi Chake chake Pemba, ambayo ina vyumba kumi na mbili, vyumba vitatu vya maabara na ukumbi wa mkutano ikiwa ni mkopo kutoka benki ya Dunia

MAKAMU wa Kwaza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, ameuagiza uongozi wa Skuli mpya ya Sekondari ya ‘Dk Omar Ali Juma’ kuanzisha kamati maalum za utunzaji wa skuli hiyo, ili iweze kuwa endelevu na kudumu kwa muda mrefu.

Alisema, imekuwa ni kawaida mara majengo kama hayo yanapokabidhiwa kwa taasisi husika, kukaa bila ya kushughulikiwa, hivyo kwa skuli hiyo na jina iliopewa, ni vyema suala la matunzo likapewa umuhimu wa pekee.

Makamu huyo wa Kwanza wa rais wa Zanzibar , aliyaeleza hayo jana huko Skuli ya Wawi Wilaya ya Chake chake Pemba , mara baada ya kuifungua skuli hiyo ya ‘Dk Omar Ali Juma’ yenye vyumba kumi na mbili, vitatu vya maabara na ukumbi wa mkutano ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi Zanzibar

Alisema kuwa jina la Dk. Omra Ali Juma, ni kubwa katika taifa hili, hivyo haiwi busara skuli hiyo baada ya mwaka ikaanza kuchakaa na kupoteza haiba na uzuri wake, jambo ambalo halitoleta sura nzuri kwa wenyeji na wageni.

Alisema ni vyema uongozi wa skuli hiyo kwa kushirikiana na kamati ya Skuli, uongozi wa shehia za Wawi na Mgogoni na wananchi wote, kukaa pamoja ili kuweka mikakati ya kuilinda skuli hiyo kwa maslahi yao na kizazi kijacho.

MAKAMU wa Kwanza wa rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akipanda Mnazi, mara baada ya kuifungua skuli mpya ya Sekondari ya inayoitwa Dk. Omar Ali Juma, ilipo Wawi Chake chake Pemba, ambayo ina vyumba kumi na mbili, vyumba vitatu vya maabara na ukumbi wa mkutano ikiwa ni mkopo kutoka benki ya Dunia (picha na Haji Nassor, Pemba)
MAKAMU wa Kwanza wa rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akipanda Mnazi, mara baada ya kuifungua skuli mpya ya Sekondari ya inayoitwa Dk. Omar Ali Juma, ilipo Wawi Chake chake Pemba, ambayo ina vyumba kumi na mbili, vyumba vitatu vya maabara na ukumbi wa mkutano ikiwa ni mkopo kutoka benki ya Dunia (picha na Haji Nassor, Pemba)

“Kabla ya uzio mlioombwa kujengwa ili kuizungurishia skuli hii haujaja, ni vyema kwanza mkakaa pamoja na kuona mnafanya nini katika kuilinda skuli hiyo na kuitunza hasa kwa vile mamilioni ya fedha yametumika’’, alieleza Maalim Seif.

Aidha amesema, kwa vile wafugaji wa shehia za Wawi na Mgogoni wanajulikana, na uongozi wa shehia upo, kusiwe na sababu ya mfugaji atakaefunga Ng’ombe wake katika eneo hilo kuonelewa haya kwa vile anaharaibu mali ya umma.

Makamau huyo Kwanza alizidi kueleza kuwa, hadhi ya jengo hilo pamoja na vifaa vilivyomo ndani yake, haiwi busara kuanza kuliacha bila ya kulitunza hasa kwa vile wanaotarajiwa kufaidika kwanza, ni vijana wa Wawi na Mgogoni.

Akizungumzia kuhusu elimu, aliwataka wazazi na walezi kuendelea kujenga ‘utatu’ wa ushirikiano unaohusisha mwanafunzi, mwalimu pamoja na wazazi hao katika kuendeleza mbele elimu.

‘’Wazazi msiwaachie waalimu peke yao , na nyinyi mnapoitwa mje skuli kwani kumtengeneza mwanafunzi, kunahitajika nguvu za pamoja na sio waalimu peke yake’’,alifafanua Makamu huyo wa Kwanza wa rais Zanzibar .

Kuhusu Dkahalia, alisema hata Serikali haijaridhika kwa skuli hiyo na nyengine kukosekana kwakwe, na bado inaendelea kutafuta wafadhili, ili kuondoa kero hiyo iliopo kwa muda mrefu.

Hata hivyo amewataka wananchi kuelewa dhana ya elimu bure, ambayo iliasisiwa na mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Amani Abeid Karume na kuona umuhimu wake na wasisite kuchangia pale panaopohitajika.

Kwa upande wake Naibu Ktaibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Amali, Abdalla Mzee, alisema skuli hiyo pekee, imegharimu jumla ya shilingi Bilion moja, ikiwa ni fedha za mkopo kutoka benki ya dunia (WB).

Alisema benki hiyo, ilikubali kuikopesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , jumla ya dola za Marekani 42 milion, sawa na shilingi 55 bilion, kwa ajili ya ujenzi wa skuli 25 za Unguja na Pemba na chuo kimoja cha ualimu

Mzee alifafanua kuwa kati ya dola hizo 42 milion, baada ya kutumia dola 32.9 bakaa ambayo inaendelea kutumiwa ni dola milion 9. 4, huku mazungumzo ya awali yakiwa yameshafanyika bina ya benki ya dunia na Serikali juu kupatiwa mradi mwengine utakaohusisha ujenzi wa dakhalia

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Juma Kassim Tindwa, alielezea wasiwasi wake juu ya utunzaji wa majengo hayo, ambayo mara baada ya wafadhili kuondoka huanza kupoteza hadhi yake.

Akisoma risala katika hafka hiyo, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Wawi Said Mohamed ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia gari skulini hapo, hasa kutokana na kuwa mbali na barabara kuu.

Jumla ya wanafunzi 480 watafaidika ndani ya madarasa hayo 12 kwa wakati mmoja katika skuli hiyo mpya ya sekondari ya Dk. Omar Ali Juma, ambayo pia ina vyumba vitatu vya maabara, chumba kimoja cha kompyuta, ukumbi wa mkutano, afisi za mwalimu mkuu na msaidizi wake.

Na Haji Nassor, Pemba

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.