walemavu

WATU wenye ulemavu, wanayonafasi kubwa ya kuielimisha jamii juu ya kukabiliana na majanga mbali mbali yanayojitokeza na yanayotarajiwa kutokezea ndani ya jamii iliowazunguka.

Akizungumza na watu wenye ulemavu, huko Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais mjini Chake Chake Pemba, Afisa Ufuatiliaji na Tathimini kutoka Idara ya Kukabiliana na Maafa, Khamis Abdurazaki Khamis, alisema suala la maumbile yao halihusiani na kukosa kuwaelimisha wengine.

Alisema taaluma walioipata katika mkutano huo wa siku moja, kama wataifanyia kazi wanaweza kuwa mabalozi wazuri ndani ya jamii, kwani suala la kupashana habari juu ya kujikinga na kukabiliana na maafa linamgusa kila mmoja.

Afisa huyo alieleza kuwa watu wenye ulemavu wanaweza kuielekeza jamii kuchana na kujenga maeneo ya mabondeni, kufuata kanuni za usafi wa mazingira, kuhifadhi misitu pamoja na kufuata kanuni za ujenzi mambo ambayo hayo wanayaweza.

‘’Yako mengi ya kuwaeleza ambao hapa hawapo, kwani majanga unayakuta katika sura mbili kuu, kundi moja likiwa lile tunalolisababisha sisi wanaadamu na mengine yale ya maumbile’’,alifafanua Arazaki.

Akifungua mkutano huo, Afisa Mdhamini Afisi ya Makamu wa pili wa rais Pemba Amran Massoud Amran alisema, kwa vile Idara ya kukabiliana na maafa haiwezi kukutana na watu wote wenye ulemavu, hivyo wao wachache wawe mabalozi kwa wenzao.

Katika hatuba yake hiyo iliosomwa na Mtaribu wa Shughuli za Serikali Pemba, Mohamed Mbarouk Haji, Amran alilitaka kundi hilo kuitumia vyema fursa ya ushiriki wao ili taaluma walioipata waisambaaze.

Akitoa mada kuhusu kuzima moto na uakozi, Afisa kutoka Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Mkubwa Hamad Khamis alisema, moto unaotokana na aina ya mafuta hasa ya petroli wasijaribu kuzima kwa kutumia maji kwani ni kuuongezea nguvu.

Kwa upande wao washiriki wa mkutano huo, ambao ni watu wenye ulemavu kutoka Wilaya za Chake chake na Mkoani, walielezea kufarajika kwao kutokana na Idara ya Kukabiliana na Maafa kuwapa taaluma hiyo.

Afisa wa watu wenye ulemavu Pemba, Maryam Mohamed Salim ameehidi taaluma hiyo walioipata kuwasambaazia wenzao ili nao waweze kujua njia mbali mbali za kujikinga na kukabiliana na majanga katika maeneo yao.

Mkutano huo wa siku moja ulioandaliwa na Idara ya Kukabiliana na Maafa Pemba , ambapo ni mfululizo wa kuyapa taaluma makundi maalum juu ya kujikinga, kuyatambua na kukabiliana na maafa endapo yatatokezea katika maene yao.

Na Haji Nassor, Pemba

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.