Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Chakula na Lishe Zanzibar ambae pia ni Makamu wa Pili wa  Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Chakula na Lishe Zanzibar ambyae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi

Wakati umefika kwa  Jamii Nchini kuanza kubadilika  kwa haraka kat ika matumizi bora ya chakula kwa lengo la kuziwezesha familia zao kujenga afya bora inayokubalika kitaalamu.

Hayo yameelezwa kwenye Mkutano wa kwanza wa Baraza la uhakika wa chakula na lishe uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View Migombani Mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Wakitoa mada katika Mkutano huo Wataalamu wa Sekta ya Kilimo Bwana Ali Ramadhan, Bwana Mzee Rajab na Bibi Mastura Kassim walisema tabia ya watu kupenda matumizi makubwa ya mchele mbali ya kupoteza fedha nyingi za kigeni kwa uagizaji wa bidhaa hiyo lakini pia yanaukosesha mwili kupata virutubisho vinavyohitajika.

Walisema ili uhakika wa chakula upatikane nguvu za uzalishaji wa mazao mbali mbali zinahitajika kwa lengo la kuondokana na utegemezi wa chakula kimoja tu cha mchele.

“ Asilimia 41% ya chakula kinachotumika Nchini huagizwa nje ya Zanzibar. Mfano bidhaa ya mchele Zanzibar huzalisha Tani 13,000 wakati uagizaji bidhaa hiyo nje ya nchi hufikia Tani 46,000 mwaka 2007 na Tani 50,000 kwa mwaka 2011”. Alifafanua Bwana Ali Ramadhan.

Hata hivyo Bwana Ali Ranadhan alielezea kwamba  zao la Muhogo kwa sasa ndio pekee linalofikia hatua ya kutosheleza mahitaji ya ndani wakati zao la mpunga  ambalo ndio chakula kikuu nchini linaendelea kuwa la kubahatisha.

Bwana Mzee Rajab kwa upande wake alisema  udumavu wa watoto hapa  Zanzibar unaonekana kupanda  kutoka Asilimia 11% hadi Asilimia 30%.

Alisema udumavu huu wa watoto ambao huanzia tumboni mwa mama unatokana na wananachi wengi hapa Zanzibar kubadilisha mfumo wa matumizi ya chakula ambao umejikita  zaidi katika vyakula vya mafuta.

Mapema akiufungua Mkutano huo wa kwanza wa Baraza la Taifa la uhakika wa chakujla na lisheZanzibar, Mwenyekiti wa Baraza hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uwajibikaji, mshikamano pamoja na uratibu wa uhakika ndio mambo ya msingi yatakayoliwezesha Taifa kuwa na uhakika wa chakula.

Balozi Seif alisema jukumu la Taifa kuwa na uhakika wa chakula si la Wizara ya Kilimo pekee bali kila Taasisi, ambapo uzoroteshaji wa kazi kwa Taasisi moja unaweza kusababisha utekelezaji mbovu wa mambo yaliyopangwa.

Alifahamisha kwamba Taifa lisilokuwa na uhakika wa chakula na lishe usalama wake unakuwa mashakani jambo ambalo wananchi wanaweza kupoteza utu wao na hili si vyema kwa Wajumbe wa Baraza hilo wakaliachia kuendelea ndani ya dhamana yao.

“ Zanzibar yenye uhakika wa chakula na lishe inawezekana iwapo kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake”. Alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Baraza la Taifa ya Uhakika wa Chakula na Lishe Zanzibar Balozi Seif.

Balozi Seif alielezea faraja yake kuona kwamba mada zilizojadiliwa katika Baraza hilo zimeelezea hali ya uhakika wa chakula na lishe Nchini ambayo sio nzuri jambo ambalo  ni changamoto zinazolikabili Taifa ambazo Baraza  hilo halinabudi kujipanga vizuri katika kukabiliana  nayo.

Alisema Baraza  la Taifa la Uhakika wa Chakula na Lishe Nchini linawajibika kusimamia utakelezaji wa Sera  ya uhakika wa chakula na lishe hapa Nchini kwani ndio chombo cha mwisho cha kufanya maamuzi katika kutekeleza masuala yoyote ya uhakika wa chakula na lishe.

“ Majukumu tuliyopewa na Taifa letu ambayo imani yangu kila Mjumbe anayafahamu ni makubwa mno na ili tufanikiwe vizuri kuyatekeleza majukumu hayo tunahitaji kuwajibika,kushikamana pamoja na kuwa na uratibu wa uhakika”. Alifafanua Balozi Seif.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

3/4/2013.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.