Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo

Mjadala kuhusu upatikanaji wa gesi mkoani Mtwara umezua mgawanyiko mkubwa, baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kusema haoni sababu ya wananchi wa mkoa huo kupinga gesi hiyo kusafirishwa kwenda mkoani Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja baada ya Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Asnan Murji, kutamka kwamba, yupo tayari kufa au kupona kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi wake wanaopinga hatua hiyo ya serikali.

Murji alitoa matamshi hayo juzi akiunga mkono msimamo wa umoja wa vyama vya siasa, walioandaa maandamano ya amani ya kupinga hatua hiyo inayotaka kuchukuliwa na serikali.

Wasiwasi kuhusu mgawanyiko kuhusu gesi hiyo, umeonyeshwa pia na Waziri Muhongo, ambaye katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, aliwataka Watanzania kutokubali kuruhusu hali hiyo nchini kwa kisingizio cha rasilimali.

Waziri Muhongo alisema hayo katika mkutano huo, alipokuwa akifafanua kuhusu miradi ya utafutaji na uvunaji wa gesi asilia nchini.

Alisema rasilimali zote za Tanzania ni mali ya Watanzania wote, hivyo akasema hakukuwa na sababu yoyote ya wananchi wa Mtwara na vyama vya siasa kufanya maandamano hayo.

Waziri Muhongo alisema haoni sababu za kufanyika kwa maandamano hayo kwa sababu asilimia kubwa ya gesi hiyo inapatikana katika kina kirefu cha bahari kuliko ile inayopatikana katika mikoa mingine.

Alisema gesi inayopatikana katika Mkoa wa Mtwara pekee ni asilimia 14, wakati inayopatikana mkoani Lindi ni asilimia saba na Pwani asilimia moja.

Waziri Muhongo alisema gesi inayopatikana katika kina kirefu cha bahari, ni asilimia 78 na kwamba, gesi nyingi inayotumika haitoki katika mikoa hiyo pekee.

Alisema gesi asilia iligunduliwa kwenye miamba tabaka katika miaka ya milioni 199.6 hadi 23.03 kipindi, ambacho alisema mipaka ya Bara la Afrika, ya Tanzania na ya mikoa hiyo haikuwapo.

“Raslimali za Tanzania ni za Watanzania wote. Tusikubali kuvunja nchi yetu vipande vipande kwa kisingizio cha rasilimali zilizopo mikoani mwetu. Wala tusikubali kuvunjavunja wilaya zetu, wala kata zetu kwa kisingizio cha rasilimali,” alisema Waziri Muhongo.

Alisema zipo rasilimali za aina tofauti zinazopatikana katika mikoa tofauti nchini, ambazo zimekuwa zikiwanufaisha Watanzania wote bila kubagua.

“Tokea uhuru, uchumi wa Tanzania umekuwa ukitegemea kilimo cha mazao ya biashara hasa katani, inayozalishwa Tanga na Morogoro, pamba inayopatikana Mwanza, Mara na Shinyanga.

Kahawa, inayopatikana Kilimanjaro, Kagera, Ruvuma na Mara. Zao la chai la kule Iringa, na Tumbaku inayopatikana Tabora. Lakini fedha za mazao hayo zimekuwa zikiwanufaisha wananchi wa mikoa yote,” alisema Waziri Muhongo na kuongeza:

“Mapato yatokanayo na uchimbaji wa dhahabu kutoka kule Geita, Mara, Shinyanga, Tabora, almasi inayopatikana Shinyanga na Tanzanite inayopatikana Manyara, pamoja na minofu ya samaki wa Ziwa Victoria kutoka kule Mara, Mwanza na Kagera yote ni kwa ajili ya wananchi wa mikoa yote bila ubaguzi.”

Alisema ipo pia mikoa inayozalisha mazao ya chakula kwa wingi kwa manufaa ya Watanzania wote, lakini hawajawahi kuandamana kudai rasilimali zao.

Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Rukwa, Ruvuma, Mbeya na Iringa kwa zao la mahindi, zao la sukari kutoka wilayani Kilombero na Mtibwa (mkoani Morogoro) na mkoani Kagera.

Alisema hata maji ya mto Ruvu yanatumiwa na wakazi wa Dar es Salaam na kwamba, hakuna manung’uniko yoyote kutoka kwa wakazi wa eneo la chanzo hicho. Mfano mwingine alisema ni umeme kutoka mabwawa ya Mtera, Kidatu na Kihansi, ambao unazalishwa mkoani Dodoma na Morogoro.

Pia umeme wa Hale kutoka mkoani Tanga, Nyumba ya Mungu kutoka mkoani Kilimanjaro, ambao unafuliwa na kusafirishwa kwenye gridi ya taifa. Kutokana na hali hiyo, aliwataka Watanzania wanaopinga ubaguzi kujiuliza sababu zilizofanya vyama vya siasa vya upinzani kuhamasisha na kushabikia maandamano ya Mtwara.

Alisema mitambo ya kufua umeme kutoka katika gesi asilia iliyopo Mtwara mjini ina uwezo wa kuzalisha Megawati 18 kwa ajili ya mikoa ya Lindi na Mtwara pekee, ambayo matumizi yake hayavuki Megawati 12.

“Ikumbukwe kwamba, gesi asilia iliyopo Mnazi Bay (Mtwara) inazalisha umeme peke yake kwa ajili ya mikoa ya Mtwara na Lindi. Gesi ya Songo Songo inayotumika  kuzalisha umeme kwa ajili ya gridi ya taifa na wananchi wa kisiwa hicho na katika viwanda vya Dar es Salaam tangu Oktoba 2004 hadi leo, kiasi cha gesi asilia kutoka katika kisiwa hicho kilichotumika ni asilimia saba tu. Hivyo, hata uchumi wa Jiji la Dar es Salaam hautumii gesi nyingi,”  alisema na kuongeza:

“Ikumbukwe kwamba, kati ya waajiriwa kwenye viwanda vya Dar es Salaam, wamo wenyeji wa Mtwara, ambako maandamano yalifanyika na vilevile wamo wafanyakazi wa vyama vya siasa vya upinzani vilivyopanga, kuratibu na kushabikia maandamano hayo.”

DAR KITOVU CHA UCHUMI
Alisema Jiji la Dar es Salaam ndiyo kitovu cha uchumi na kwamba, asilimia 80 ya mapato ya nchi yanazalishwa jijini humo. Waziri Muhongo alisema tayari jiji hilo lina jumla ya viwanda 34 vinavyotumia gesi asilia, ambavyo pia vinahitaji kupanua shughuli zao zaidi endapo gesi hiyo itapatikana kwa wingi.

Alisema takriban Dola za Marekani bilioni moja sawa na Trilioni 1.6 zitaokolewa kila mwaka kwa kutumia gesi asilia kuzalisha umeme na kuachana na kufua umeme huo kwa kutumia mitambo inayotumia mafuta.

Kwa jiji la Dar es Salaam pekee, alisema takriban Dola za Marekani milioni 202 zinatarajiwa kuokolewa kila mwaka iwapo jiji hilo litatumia gesi asilia badala ya mafuta.
Alisema jiji hilo ndilo lenye miundombinu mikubwa ya usafirishaji na usambazaji wa umeme kuliko mikoa mingine na kwamba, ndio sababu inayofanya kusafirisha gesi kutoka Lindi na Mtwara kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.

Alisisitiza kwamba rasilimali zilizopo nchini ni za Watanzania wote kwa mujibu wa Katiba na ndiyo maana zinatunzwa na kuzalishwa katika maeneo mbalimbali bila kujali maeneo zinakopatikana.

Kabla ya Waziri Muhongo kueleza hayo jana, Murji akiwa katika mkutano maalumu aliouandaa kwa kuwajumuisha viongozi wa umoja wa vyama vya siasa na wananchi uliofanyika katika ukumbi wa Pentekosti mjini Mtwara juzi, bila kificho, alisema anaungana bega kwa bega na uamuzi uliofanywa na umoja wa vyama vya siasa, kuandaa maandamano ya amani ya kupinga kusafirishwa gesi hiyo.

Murji alisema anapongeza kitendo hicho, kwa vile kimedhihirisha wananchi wa Mtwara, hawaungi mkono suala la serikali kusafirisha gesi bila kuwapo na sheria maalum ya kuwanufaisha.

Alisema anashangazwa na kitendo cha serikali kutangaza kusafirisha gesi, wakati hata rasimu, ambayo imeandaliwa kuhusu gesi haionyeshi wananchi watanufaika vipi.

“Najua kwa uamuzi huu, ninaochukua kukaa meza moja na umoja huu wa vyama vya siasa, unaweza kuniletea athari na madhara makubwa kwa upande wangu, hasa kwa uongozi wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec). Nasisitiza niko tayari kwa lolote litakalotokea kwa sababu mimi ni mbunge wa watu na wananchi ndiyo walionichagua,” alinukuliwa Murji akisema na kuongeza:

“Nawajibika kwa ajili ya wananchi na siyo kitu kingine. Nasisitiza kuwa tuijenge Mtwara kwanza vyama baadaye…naungana na kauli mbiu ya wananchi wangu inayosema kuwa gesi kwanza, vyama baadaye.”

Maandamano hayo, ambayo yalifanyika Decsemba 27, mwaka jana yaliratibiwa na baadhi ya vyama vya siasa, ikiwamo Chadema, NCCR-Mageuzi, Sau, TLP, APPT Maendeleo, ADC, UDP na DP, yakiwa na kaulimbiu ya ‘gesi kwanza vyama baadaye, hapa hakitoki kitu’.

Yaliwashirikisha wananchi wa wilaya za mkoa huo wa Mtwara, zikiwamo Tandahimba na Newala, yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara mjini kupitia barabara ya kwenda Msimbati eneo, ambako gesi asilia inapatikana.  Katika madai yao, wananchi hao walisema serikali haijaweka wazi namna gani wakazi wa Mtwara watanufaika na gesi hiyo, huku tayari Rais Jakaya Kikwete akiwa ameshazindua ujenzi wa bomba kwenda Dar es Salaam na kutaka ujenzi huo usitishwe.

Pia walisema uamuzi wa kupeleka gesi Dar es Salaam unapingana na tamko la Rais  alilolitoa kwenye ziara yake mkoani humo mwaka 2009 kwamba, mkoa huo unaandaliwa kuwa ukanda wa viwanda.  Nyingine walitaka vinu vya kuzalishia gesi vijengwe Mtwara kwa kuwa wanayo maeneo ya kutosha ya ujenzi huo tofauti na Dar es Salaam.

Wakati wa hotuba yake ya kuukaribisha mwaka 2013, Rais Jakaya Kikwete aliwahakikishia wakazi wa Lindi na Mtwara na maeneo mengine ambayo gesi itagundulika, wakanufaika, lakini alisema kuwa rasilimali hiyo ni mali ya Watanzania wote.

Kauli kama hiyo ilitolewa wiki iliyopita na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.
Baadhi ya wanasiasa waliojitosa katika mjadala huo na kuwaunga mkono wakazi wa Mtwara kuandamana ni Mwenyekitiwa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba; Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia; Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.

CHANZO: NIPASHE

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.