Serikali  ya Mapinduzi Zanzibar, imesema haiwezi kuzuia kuku kutoka Ulaya wauzwe katika soko la Zanzibar.
Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Zanzibar, Asha Ali Abdulla, wakati akizindua mradi wa kuwajengea wajasiriamali uwezo Bwawani mjini hapa jana.

Alisema ni kweli serikali imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wafugaji kuwa kipato chao kimeanguka tangu kuku hao waanze kuingizwa katika soko la ndani la Zanzibar.

“Siyo rahisi kwa sasa kuzuia kuku kutoka Ulaya kuingizwa Zanzibar na kama tutafanya hivyo kulinda wafugaji wa ndani, tutakuwa tunakwenda kinyume cha sera ya soko huria la biashara,” alisema Asha.

Aidha, alisema katika ulimwengu wa  sasa, ni vigumu kuchukua hatua kama hizo bali jambo la msingi wafugaji wa ndani wajengewe uwezo wa kuzalisha bidhaa bora ili wamudu soko la ushindani.

Asha alisema kama wafugaji wa ndani watazingatia ubunifu na viwango vya ubora kwa bidhaa wanazozalisha, bado wana nafasi kubwa ya kushika soko la utalii pamoja na wananchi wa Zanzibar.

Alisema tangu kuku kutoka katika soko la Ulaya kuanza kuingizwa kwa wingi Zanzibar, wafugaji wamekuwa wakiwasilisha malalamiko wakitaka serikali kupiga marufuku uingizaji wa biashara hiyo.

Hata hivyo, alisema serikali imeamua kuwapatia ujuzi yakiwamo mafunzo maalum wajasiriamali ili wazingatie ufugaji bora pamoja mafunzo juu ya uhifadhi bora wa bidhaa kabla ya kuingia katika soko la ushindani.

Asha aliwataka wajasiriamali walionufaika na fedha na mafunzo yaliyotolewa na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania, (Costech) kuhusu uzalishaji bora, kutumia fedha kama zilivyokusudiwa ikiwamo kuzalisha bidhaa zenye kiwango bora.

Alisema Costech imetoa jumla ya Sh. milioni 40 kwa vikundi vitano ambapo wajasiriamali 500 wanatarajiwa kunufaika na mpango huo.

Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk. Hassan Mshinda, alisema tume hiyo tangu ifungue ofisi Zanzibar, imetumia Sh. milioni 700 kwa ajili ya kazi za utafiti, ukarabati wa maabara ya Chuo cha Kilimo Kizimbani na kufadhili wanafunzi  10 kutoka Zanzibar ambao wanasoma ngazi ya shahada na stashahada katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.

 

CHANZO: NIPASHE

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.