balozi

SERIKALi ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema kitendo cha kupigwa risasi kiongozi wa kiroho, Padre Ambrose Mkenda kumeleta sura mbaya kwa serikali na taifa na kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa na wapenda amani na umoja wa kitaifa visiwani Zanzibar.

Tamko hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi katika ziara yake maalumu ya kuwapa mkono wa pole uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, pamoja na wanafamilia wa kiongozi huyo huko Tomondo mjini Zanzibar jana.

Hata hivyo Balozi Seif alisema kwamba vyombo vya ulinzi vitahakikisha vinawatafuta na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu waliohusika na kitendo cha kumpiga risasi Padre huyo nyumbani kwake wakati akisubiri kufunguliwa mlango (geti) kabla ya kuingia nyumbani kwake Desemba 25 mwaka huu.

“Ni tukio baya kwa taifa na serikali… tena linapaswa kulaaniwa na wapenda amani na umoja wa kitaifa,” alisema.

Alisema kwamba kitendo hicho ni kibaya na kinasikitisha hasa kwa kuzingatia kwamba Tanzania ni nchi ya amani na kuwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kuwapata watu hao.

Kiongozi huyo wa kiroho alipigwa risasi mbili wakati anasubiri kufunguliwa geti na mlinzi wa Shule ya Francis Maria ambapo ndani kuna nyumba za kuishi viongozi wa kiroho wakiwemo watawa.

“ Serikali tutaendelea kufanya uchunguzi kupitia vyombo vya ulinzi na kuhakikisha watu hao wanapatikana na kufikishwa katika vyombo vya sheria,” alisema.

Alisema kwamba serikali itaendelea kulinda amani na umoja wa kitaifa kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.

Kwa upande wake Padre Cosmas Shayo alisema kwamba wakati umefika kwa serikali kuimarisha ulinzi dhidi ya raia wake hatua ambayo itasadia kuondolea hofu wananchi katika maisha yao ya kila siku Zanzibar.

Hata hivyo, alisema kwamba jamii lazima ijiepushe na vitendo vya kuwafundisha chuki za kidini watoto wadogo kwa kuwa kitendo hicho ni mwanzo wa kuvuruga amani na mshikamano.

“Kuna watoto wadogo hufundishwa tabia ya kukashifu watu wengine, tuelewe kuwa taifa halitakuwa na muelekeo mwema wa jamii yake ya baadaye,” alisema Padre Shayo.

Matukio ya kuhujumiwa viongozi wa dini Zanzibar ikiwemo kumwagiwa tindikali Katibu wa Mufti, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga Novemba 6 mwaka huu, yametanguliwa na kuchoma moto makanisa 25, na baa 12 katika kipindi cha miaka 11.

Hata hivyo hakuna watu ambao waliwahi kukamatwa na kufikishwa mahakamani kuhusiana na matukio hayo, lakini viongozi wa madhehebu ya dini wamekuwa wakisisitiza serikali kuunda tume huru ya kuyachunguza.

MTANZANIA DAIMA

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.