Karani wa Sensa akitekeleza wajibu wake
Karani wa Sensa akitekeleza wajibu wake

                                                                     Press Release:-

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete Jumatatu ya Tarehe 31 Disemba  2012 anatarajiwa  kuzindua matokeo ya Sensa ya Watu  na Makazi ya mwaka 2012.

Uzinduzi huo utakaoshirikisha wananachi wa Mkoa wa Dar es salaam na Vitongoji vyake wakiwemo pia waalikwa kutoka sehemu mbali mbali za mikoa ya Tanzania utafanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.

Wajumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya watu na Makazi ya Mwaka 2012 walikutana pamoja na mambo mengine katika kikao chao cha 10 walipitia ratiba ya shughuli hiyo kwa matayarisho ya mwisho chini ya Mwenyekiti mwenza wa Kamati hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Mjini Dar es salaam.

Akiwasilisha Taarifa za kazi mara baada ya kumalizika kwa zoezi la Sensa kwa wajumbe wa Kamati hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania Dr. Albina Chua alisema kazi ya miongozo ya Takwimu hivi sasa inaendelea vyema.

Dr. Albina Chua alifahamisha kwamba miongozo hiyo inakwenda sambamba na kuhakiki taarifa na kuanza kwa zoezi la uingizaji Taarifa katika compyuta kazi inayofanywa na wataalamu wa Takwimu baada ya kupata mafunzo maalum ya wiki sita.

“ Jumla ya watu mia nne walilazimika  kuwajiriwa kufanya kazi hiyo muhimu inayohitaji utaalamu na umakini wa hali ya juu katika kuikamilisha  hasa kwenye uchambuzi wa takwimu za Sensa “. Alifafanua Dr. Albina Chua.

Naye Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. William Mgimwa alisema Wizara ya Fedha itaendelea na uchambuzi wa Takwimu zitakazotokana na sensa hiyo kwa lengo zaidi la kiuchumi.

Dr. Mgimwa alisema katika kukamilisha zoezi zima la sensa ya watu na makazi Serikali imeshatoa shilingi Bilioni sita kati ya Bilioni 12 zilizotengwa ambapo kazi ya usafirishaji vifaa vya sensa imeshafanywa na hivi sasa  uingizwaji wa taarifa katika Kompyuta unaofanywa na Wahariri maalum inaendelea.

“  Tumefanikiwa vyema katika kazi hii muhimu licha ya changamoto ndogo ndogo zilizojichomoza katika zoezi hili ikiwemo madai ya Wenyeviti wa Vijiji waliosaidia kusimamia zoezi hili katika maeneo yao”. Alifafanua Waziri Mgimwa.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Dr. Mwinyihaji Makame Mwadini kwa niaba ya Waziri anayesimamia Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar alisema zoezi la sensa kwa kiasi kikubwa limefanikiwa vyema licha ya changamoto za baadhi ya vikundi vya kidini kupinga Zoezi hilo.

Dr. Mwinyihaji alieleza kwamba sensa ya watu ambayo inakusanya takwimu tofauti itasaidia chachu ya maendeleo hasa katika mpango wa maendeleo katika kipindi cha miaka kumi ijayo.

Akitoa nasaha zake Mwenyekiti mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya watu na makazi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza watendaji wa sekta tofauti Nchini waliojitolea kufanikisha zoezi zima la sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.

Balozi Seif alisema zoezi hilo lilikumbwa na changamoto zilizopelekea kuongezwa kwa siku za uandikishaji kutokana na sababu za baadhi ya makundi ya dini kushawishi wananchi kutojiandikisha kwenye zoezi hilo.

Kikao cha kumi na moja cha Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi kinatarajiwa kufanyika Zanzibar mnamo Wiki ya Pili ya Mwezi wa Machi mwaka 2013.

 

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

29/12/2012

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.