Nna jini aniwina, ananipanda kichwani
Hataki kutoa jina, ananipa mtihani
Visomo tushavisoma, haongei asilani
Hataki kutoa jina

Hataki kutoa jina, ya kwamba yeye yu nani
Nani aliemtuma, na kaja kwa shida gani
Maluuni aniwina, mwaka wa arobaini
Hataki kutoa jina

Tushaupiga uganga, wa kofi na kufukiza
Wakakutana waganga, jinale kumuuliza
Lakini jini apinga, yu nami aniumiza
Kagoma kutoa jina

Tushapiga makafara, na kusoma tawasuli
Jini bado yu imara, hana hata mushkeli
Aniletea madhara, anitesa kweli kweli
Hataki kutoa jina

Tukasoma na rukia, visomo vilo vikali
Yu kichwani asinzia, wallahi hata hajali
Atucheka nadhania, atuona madhalili
Katu hakutoa jina

Magwiji mlo nyumbani, nadhani mwanisikia
Wa Chambani na Bumbwini, wa Ole na Nungwi pia
Muje mutie ubani, mwenenu nateketea
Mumng’oe aondoke

Suleiman Hakum

28 Disemba 2012

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.