HIVI karibuni imeelezwa kuwepo mpango wa kutaka kuwashirikisha kikamilifu wananchi wa Zanzibar katika mchakato wa kutoa maoni kwa sheria zitakazoandaliwa na serikali.

Hatua hii, kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad, ni kuzifanya sheria za Zanzibar kwenda sambamba na matakwa na matarajio ya wananchi.
Ukiyatafakari maelezo haya juu juu utaona huu ni mpango mzuri na unaokubalika katika mfumo mzuri wa utawala bora, lakini uzoefu unaonyesha kuwa mara nyingi kinachosemwa na serikali ni tofauti na kile kinachotekelezwa.

Kwa ufupi, kwa muda mrefu na mpaka hivi sasa, serikali imekuwa ikiona ni haki yake kuudanganya umma kwa maneno matamu yaliyopakwa asali, lakini kinacholiwa ni shubiri.
Nasema hivi kwa sababu nyingi zilizotokana na uzoefu. Mojawapo ni kwamba mara nyingi tumeambiwa kwa vishindo kwamba Zanzibar imepania kuwa na mfumo wa utawala wa haki na sheria na uliokuwa wa kweli na uwazi.
Lakini hili halionekani kutendeka na kila siku tunaona sheria zinatoka juu na kutelemshwa chini na hata sheria ikiwa nzuri usimamizi wake huwa mbovu na baadhi ya wakati unanuka na kukirihisha.
Kwa mfano, mpaka hivi sasa dhamana kwa mshtakiwa sio haki bali inatokana na mapenzi ya hakimu. Wapo mahakimu waliokuwa na ubavu wa kusema walipewa amri na wakubwa juu ya namna walivyotakiwa kuziendesha kesi, lakini hao mahakimu na majaji hawakuwa na ujabari wa kusema viongozi waliotoa amri hizo ni kina nani.
Katika utoaji wa dhamana mahakama za Zanzibar zimekuwa zikiweka masharti magumu kama ya kulazimisha wadhamini wawe watumishi wa serikali na kwa maana hiyo raia wengine hawana haki ya kuwawekea dhamana washtakiwa.
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Makungu, alikiri hivi katika kipindi kimoja cha Televisheni ya Zanzibar nyakati za asubuhi kuwa mwenendo huu wa kutaka watumishi wa serikali wawe ndiyo wanaoruhusiwa kuwadhamini washtakiwa ni mbovu.
Lakini kwa masikitiko makubwa, badala ya kueleza kwamba anachukua hatua za kuirekebisha hali hii ya kusikitisha na kutisha alisema atakaa na wenzake kujadili suala hili. Lini atafanya hivyo hakueleza.
Lakini hapa inafaa ieleweke kwamba wakati Jaji Mkuu anapanga kuwa na kikao wapo watu waliokosa kupata dhamana na wanateseka mahabusu kutokana na haya masharti magumu ya dhamana.
Ni kawaida kusikia katika mahakama za Zanzibar upande wa mashtaka kuomba anayeshtakiwa aendelee kukaa mahabusu hata ikiwa imepita miezi mitatu kwa vile upelelezi wa tuhuma zinazomkabili mshtakiwa, haujakamilika.
Hapa unajiuliza kama upelelezi haukukamilika ilikuwaje basi mtu akamatwe na kufunguliwa mashtaka? Au ndio kusema dhana au ndoto huwa inatosha kuwa sababu ya msingi kumfungulia mtu mashtaka? Hii ni hatari kubwa. Jambo hili linafaa lichunguzwe kwa makini na kufanyiwa marekebisho ya haraka.
 Njia moja itayosaidia kuzuia matumizi mabaya ya sheria au uonevu wa aina moja au nyingine ni kuwa na kipengele kinachowapa watu wanaofutiwa kesi kutokana na kukosekana ushahidi kulipwa fidia kwa bughudha, hasara na mateso waliyoyapata wakiwa mahabusu wakati hapakuwa na ushahidi wa kutenda kosa.
Njia hii itapunguza matumizi mabaya ya sheria na kupunguza uonevu kwa kutumia vyombo vya dola na mahakama. Jingine linalofaa kutupiwa macho ni huu mtindo wa wawakilishi kujadili na kupitisha sheria mbalimbali bila ya kuwa na vikao vya kushauriana na wananchi katika majimbo yao.
Hawa wawakilishi hudiriki hata kueleza bila ya aibu kwamba walikuwa wanazungumza kwa niaba ya watu katika majimbo yao na wanaunga mkono au kuukataa muswada wa sheria mia kwa mia wakati hawajafanya hata mkutano mmoja katika majimbo yao kuujadili huo muswada wa sheria. Vilevile huenda huyo mwakilishi hajataka hata ushauri juu ya huo muswaada wa sheria kutoka kwa mume au mke wake, jirani au rafiki.
Ni vizuri kutoka sasa wakati wawakilishi wanapojadili muswada watoe uthibitisho wa vikao vingapi walifanya katika majimbo yao na idadi ya watu walioshiriki katika mijadala na sio kusimama ndani ya Baraza la Wawakilishi na kutoa kauli zisiokuwa na ukweli.
Vile vile vyombo vya habari vya serikali, bado sio vya umma kama tunavyotakiwa tuamini, viendeshe mijadala ya wazi juu ya hizo sheria zinazotaka kutungwa ili wananchi waelewe kinachoendelea katika nchi yao.
Mimi binafsi sikumbuki hata siku moja kuambiwa kipo kikao katika jimbo langu ambapo mwakilishi alikuwa anataka maoni ya wananchi juu ya muswada wa sheria unaotaka kuwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi. Njia gani hao Wawakilishi wetu wanatumia kujua fikra za wananchi, wanazijua wenyewe na ni siri yao ya mioyoni. Sasa tunaambiwa unakuja mfumo mpya. Tunasema ahlan wa sahlan, lakini kinachozungumzwa kiwe cha kweli na sio danganya toto.
Watu wazima wanapodanganywa huona sawa na kutukanwa kwani anayedanganywa ni mtu zuzu na asiyejua lolote. Kwa hivyo ni vizuri tukabadilika, tena kwa haraka sana na kuhakikisha wananchi wanashiriki katika kutunga sheria za nchi yao.
Lakini jingine muhimu ni kuhakikisha sheria zinasimamiwa kwa uadilifu na pasiwepo mazingira ya watu kutia mashaka kwamba zinatumika vibaya, hasa kukidhi malengo na utashi wa kisiasa.
Wote wanaovunja sheria au kunyanyasa watu, bila ya kujali nyadhifa zao katika serikali wachukuliwe hatua ili kila mwananchi awe na uhakika kuwa Zanzibar ni ya watu wote na sio wengine mabwana na wengine watwana.
Tunausubiri huo mchakato kabla ya kuutolea hukumu, lakini kama lengo ni kudanganya basi wahusika waelewe kwamba kwa sasa watu wa Zanzibar hawadanganyiki. Kama maneno matamu yanamtoa nyoka pangoni hiyo haitoshi kama hayaendani na vitendo kupata imani ya Wazanzibari kwa serikali yao.
Wanaofikiri bado wanaweza kuendeleza ubabaishaji wajue wamechelewa na historia itakapowahukumu wasije kusema wanaonewa.
Chanzo: Makala ya Salim Said Salim kwenye gazeti la  Tanzania Daima

5 thoughts on “Zanzibar hatudanganyiki tena”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.