Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.

Vyombo vya habari vya Tanzania Bara vimekuwa vikiripoti kuwepo kwa hali ya kutoelewana ndani ya chama kikuu cha upinzani huko, CHADEMA, kwa kipindi kirefu sasa. Zanzibar Daima inachapisha hapa moja ya taarifa refu zilizoandikwa kuhusu mgogoro huo wa ndani, kwa maslahi ya kutanua mjadala. Je, ni kweli CHADEMA inasambaratika au kusambaratishwa mithali ya ilivyotokea kwa NCCR-Maguezi? Soma makala ifuatayo na changia maoni yako:

Hali ya kisiasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ni mbaya na tayari kumeanza kuwapo hofu ya chama hicho kikuu cha upinzani hapa nchini, kufa.

Hofu hiyo inayokana, pamoja na mambo mengine, kuibuka kwa makundi yanayohasimiana, yanayoundwa na baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hicho.

Katika fukuto hilo, JAMHURI imefanikiwa kupata habari za uhakika kutoka kwa baadhi ya wanachama na viongozi, zinazohusu kuwapo mkakati madhubuti wa kuwafukuza baadhi ya viongozi wa chama hicho.

Duru za uchunguzi zinaonesha kuwa walengwa wakuu kwenye mpango huo ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zitto, na Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda. Pamoja nao, walengwa wengine ni wafuasi wa wanasiasa hao.

Moja ya sababu zinazotajwa kuchochea au kuibua makundi makuu matatu ndani ya Chadema, ni mbio za kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015. Makundi yanayotajwa, na ambayo yameanza kujitokeza hadharani yamejiegemeza kwa viongozi watatu maarufu – Zitto, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, na Katibu Mkuu Dk. Wilbrod Slaa.

Zitto anatajwa kama mmoja wa vinara wa migogoro ndani ya Chadema, akidaiwa kutumia umaarufu wake kama

kinga ya kufanya lolote analotaka akiamini kuwa “CHADEMA bila Zitto, haipo”.

Pia urafiki wake wa karibu na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, na viongozi wengine waandamizi wa CCM umekuwa ukiwatia shaka baadhi ya wanachama, wafuasi na viongozi wa CHADEMA.

Tayari Zitto ameshatangaza hadharani nia yake ya kuiwakilisha CHADEMA kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015, na kwa sasa anaendesha kampeni ya umri wa wagombea urais kupunguzwa na ikiwezekana iwe miaka 35. Mwaka 2015, Zitto atakuwa anatimiza umri wa miaka 39.

Hii si mara ya kwanza kuibuka kwa makundi ndani ya CHADEMA, kwani miaka kadhaa iliyopita Zitto na Mbowe walisuguana kutokana na uamuzi wa Zitto wa kutangaza kuwania nafasi ya uenyekiti wa CHADEMA Taifa. Mzozo huo ulimalizwa kwa busara ya wazee na wanachama waandamizi ndani ya chama hicho, kwa Zitto kukubali kuondoa jina lake mbele ya waandishi wa habari.

Hata kurudi kwake kwenye nafasi ya Naibu Katibu Mkuu CHADEMA kulitokana na busara za wazee, kwani Mbowe hakumtaka kabisa Zitto aendelee kuwa na madaraka ya juu katika chama.

Katika hotuba yake kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CHADEMA, Mbowe hakuficha kutamka wazi kuwa alinyanyaswa vya kutosha, na kwamba baada ya kuchaguliwa kwa mara nyingine kuwa mwenyekiti, alikuwa na uamuzi wa kuamua nani awe nani ndani ya chama hicho.

Aidha, aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, ambaye alionekana kutofautiana na Mbowe, alikufa katika ajali ya gari ambayo mazingira yake bado yanahojiwa na wafuasi wake. Wangwe anakumbukwa kwa kuwa mstari wa mbele kudai wigo mpana wa demokrasia ndani ya chama hicho.

Mtafaruku ndani ya CHADEMA umeenea hadi kwa Mratibu wa Sera na Utafiti wa CHADEMA, Mwita Waitara, ambaye kwa sasa haelewani kabisa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVITA), John Heche.

Ugomvi wa wanasiasa hao vijana, ulianza wakati wa kura za maoni za kumpata mwanachama wa CHADEMA kwa ajili ya kuiwakilisha katika uchaguzi wa ubunge Jimbo la Tarime mkoani Mara. Waitara alimshinda Heche, ingawa naye baadaye aliangushwa na mgombea wa CCM, Nyambari Nyangwine.

Tangu wakati huo, Waitara na Hache hawapikiki chungu kimoja. Uhasama huo umeshika kasi baada ya Heche kwenda Tarime hivi karibuni na kutangaza nia yake ya kuwania ubunge katika jimbo hilo.

Ugomvi ndani ya BAVICHA umezidi kuwa mkali, kwani Heche pia haelewani kabisa na Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo, Julian Shonza. Ugomvi wao ulipamba moto baada ya Shibuda kutangaza kuwania urais kupitia CHADEMA akiwa katika mkutano wa CCM.

Baada Shibuda kutangaza nia hiyo, Heche alimkosoa kwa kusema alifanya makosa kutangaza nia akiwa katika jukwaa lisilostahili. Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida, Shonza alijitokeza hadharani na kumpinga Heche, akisema Shibuda alikuwa na haki ya kufanya hivyo. Hadi sasa wanasiasa hao vijana hawaelewani.

Wakati hali ya mambo ikizidi kuwa mbaya ndani ya CHADEMA, viongozi wake waandamizi wanajitahidi kuficha ukweli wa mambo.

Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwanasheria wa CHADEMA, Mabere Marando, katika mahojiano yake na JAMHURI, amejitahidi kuwa na kauli kali za kushutumu waandishi wa habari na kusema kwamba chama hicho hakina mgogoro wowote wa kiuongozi.

Amekwenda mbali zaidi kwa kusema baadhi ya magazeti na vyombo vya habari vinatumiwa na CCM kwa ajili ya kuivuruga CHADEMA.

“Kama unapenda kuandika, andika, lakini mimi najua hakuna migogoro wala makundi matatu wala matano ndani ya CHADEMA, kama unataka kuandika andika hayo uliyoambiwa. Unapoendelea kuhoji hayo unafanya kazi ya CCM na Usalama wa Taifa,” amesema ambaye amewahi kufanya kazi ya ushushushu katika Usalama wa Taifa.

Pia Marando ana historia ya kuwa kwenye migogoro, kwani akiwa NCCR-Mageuzi (chama alichokiasisi) aligombana na hatimaye kushindwa na aliyekuwa Mwenyekiti wake, Augustine Mrema. Alikihama chama hicho na kujiunga CHADEMA.

Wakati Marando akisema hivyo, uhasama miongoni mwa viongozi wa chama hicho unaonekana wazi hata kwenye Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) ambako baadhi ya viongozi, akiwamo Zitto, wamejitenga kabisa.

Mwanasiasa huyo hahudhurii mikutano wala hafla za uchangishaji fedha zenye lengo la kufanikisha mpango huo. Wakati wa Operesheni Sangara, wakati ambao CHADEMA haikuwa na mpasuko mkubwa, Zitto alishiriki mikutano mingi na sehemu mbalimbali nchini.

Pia kuna habari za uhakika kwamba Zitto amekuwa akisafiri nje ya nchi bila ruhusa au kutoa taarifa kwa uongozi wa juu wa chama chake. Si hivyo tu, bali kuna baadhi ya vikao vya chama vinavyohitaji msimamo wa pamoja ambavyo amekuwa hahudhurii.

Waitara, Heche wazungumza

Kwa upande wake, Heche anajitahidi kumung’unya maneno kwa kusema hakuna makundi yanayohasimiana ndani ya CHADEMA, na kwamba chama hicho hakiamini katika kufukuzana, bali katika kujenga chama kwa kufuata misingi ya Katiba, miongozo na kanuni.

“CHADEMA ina kanuni, misingi na miongozo, iwapo mtu atakosea basi anatakiwa kufukuzwa kwa kufuata kanuni hizo na si vinginevyo,” amesema Heche.

Kwa upande wake, Waitara anasema hajisikii vizuri kuona Heche amekwenda Tarime kutangaza nia ya kuwania ubunge, ilhali akitambua yeye (Waitara) bado ana mtaji wa wapigakura waliomuunga mkono katika kinyang’anyiro cha ubunge jimboni humo mwaka 2010.

“Katika hali ya kisiasa, kibinadamu, lazima ujisikie vibaya, tena ni mtu (Heche) ambaye nilipogombea hakuniunga mkono, mimi ninaona ni kama inatangazwa vita ambayo inabidi itumike busara kuimaliza, lakini mtu huwezi kuwa mnafiki lazima ujisikie vibaya. Katika hali ya kawaida kitendo cha kwenda kutangaza kwamba anagombea na mimi nilikuwa mgombea pale… Mwaka 2010 baada ya Heche kushindwa kwenye kura aliondoka kuja Dar es Salaam kujiunga kwenye timu ya Dk. Slaa akamsaidia kufanya kampeni, lakini hata ndugu yake kama Mwenyekiti wa BAVICHA Tarime aliondoka kabisa Tarime.

“Kwa ujumla watu wa Heche waliokuwa wanamuunga mkono hawakunisaidia kampeni, kwa hivyo kilichofanyika watu waliingia kwa maana ya kusema CHADEMA, siyo mtu… tukapambana mpaka tukafikia tulipofikia, matokeo yake hilo lilileta mgawanyiko yakatokea matokeo ambayo yalitokea, tukapoteza jimbo.

“Kwa hiyo, huo ndiyo ukweli, kwamba wao tulipokwenda kwenye mchakato wa kura za maoni baada ya kushindwa, hawakuniunga mkono… hata familia ya akina Heche haikuniunga mkono kabisa na sina hakika kama walinipigia kura.  Ukweli ni kwamba watu wangu wametangaza kwamba lazima watanisapoti kwa nguvu zote…lakini nilishasema mimi sina tatizo tukienda kwenye mchakato wa chama, kama kitamteua mtu ambaye wataona kwamba anafaa mimi nitafanya kazi ya chama. Lakini ninachokifahamu ni kwamba kwa sababu niligombea 2010 tukapambana na watu wa Tarime bado wananiunga mkono, nina mtaji pale, mimi nadhani bado nitapambana,” anasema.

Waitara ameomba mara kadhaa kukutana na Heche kujadili kuhusu kugombea ubunge wa Tarime, lakini bado juhudi hizo hazijazaa matunda na kwamba hata uongozi wa juu CHADEMA haujaonyesha nia ya kuingilia kati suala hilo.

“Mimi na yeye (Heche) tunazungumza mambo ya kawaida sana, hatujawahi kukaa tuzungumzie mustakabali wa Tarime, na hilo jambo amejaribu kulikwepa muda mrefu sana, na mimi nimeomba mara nyingi kwamba hata chama kiingilie kati tujadiliane, nimeomba viongozi wengi, nimemuomba Dk. Slaa. Lakini kama waliniteua kugombea, lakini kuna mtu anatangaza katika utaratibu usio wa kawaida, ametangaza mapema. Kwa hiyo, binafsi nisingetaka hayo mapambano yaendelee kuwapo,” amesema Waitara.

Kwa upande wake, Heche amesema hana ugomvi na Waitara kwa kuwa kila wakati wamekuwa wakikutana na kusalimiana vizuri.

Kuhusu kutomsaidia katika kampeni za mwaka 2010, Heche anasema hakufanya hivyo kwa vile alichaguliwa na uongozi wa Taifa wa CHADEMA kuwa kiongozi wa msafara wa kampeni za kitaifa za chama hicho.

“Kwa sasa CHADEMA hatuzungumzi mambo ya mwaka 2010, kwa sasa tunazungumzia kuchukua dola mwaka 2015, wakati Waitara anagombea mimi nilichaguliwa na uongozi wa juu kuwa kiongozi wa msafara wa mgombea urais wa CHADEMA. Hata hivyo, CHADEMA inao wanachama wengi na si mimi tu ambaye wanatakiwa kufanya kazi ya chama, si mimi tu niliyetakiwa kubaki mkoani Mara na kumpigia kampeni mgombea huyo. Hata hivyo, nilimtambulisha Nyamongo na Sirari (miji iliyopo Tarime). Hata mwaka 2015 uongozi wa juu wa chama ukinichagua kuongoza msafara wa kampeni, na kama sigombei ngazi yoyote ya uongozi wa chama nitafanya hivyo,” amesema.

Kinana azungumza

Uongozi mpya wa CCM umetajwa kama moja ya sababu zinazoifanya CHADEMA ianze kuyumba. Chini ya Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, CCM imeanza kujijenga upya kwa wanachama wake na wananchi kwa lengo la kurejesha imani iliyokuwa imeporomoka mno.

Kinana, ameiambia JAMHURI kwamba ugomvi ndani ya CHADEMA ni wao wenyewe, na kwamba CCM haihusiki kwa namna yoyote kuibua au kukuza mgogoro.

Amesema tangu ateuliwe kushika wadhifa huo, amefanya mikutano sehemu mbalimbali nchini, na kwamba hajawahi hata siku moja kuzungumza masuala ya CHADEMA na vyama vingine kwenye mikutano wanayofanya.

“Sina muda wala nafasi ya kuzungumza mambo ya wapinzani, tangu niteuliwe kuwa Katibu Mkuu nimefanya mikutano 23, hakuna mahali nilipotaja chama cha siasa. Kazi yangu ni kunadi Ilani ya CCM, kukabiliana na matatizo ya wananchi. Matatizo tunayoyakabili kupitia Ilani yetu yanatosha kabisa, sina wala hatuna sababu ya kujadili wapinzani. Kama wao wana matatizo yao, hayo ni yao. Wasituhusishe. Narudia tena, sisi kazi yetu ni utekelezaji Ilani yetu, kupambana na matatizo ya wananchi na kuimarisha chama chetu, basi. Wasitafute mchawi, hatuna muda wa kujadili mambo yao,” amesema Kinana.

Wimbi la viongozi kuihama CHADEMA

CHADEMA inakabiliwa na changamoto nyingine ya kuwatimua baadhi ya viongozi na wanachama. Madiwani kadhaa wa Arusha na Mwanza wamefukuzwa kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo za usaliti.

Hatua hiyo imekuwa ikungwa mkono na wafuasi wengi wa CHADEMA, lakini imekuwa kete kwa CCM kuwapata wanachama hao.

Wiki iliyopita, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CHADEMA ambaye pia ni Katibu wa chama hicho Mkoa wa Mbeya ambaye amesimamishwa, Edo Mwamalala, alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kusema kwamba Dk. Slaa ni mamluki namba moja wa CCM, kutokana na kumiliki kadi ya chama hicho.

Viongiozi wengine wa CHADEMA wakiwamo Mbowe, Dk. Slaa, Zitto na John Mnyika (Mkurugenzi wa Habari na Uenezi) hawakupatikana kuzungumzia sakata la mgogoro ndani ya chama hicho.
Source: http://www.wavuti.com/4/post/2012/12/chadema-inakufa-ripoti-maalumu-gazeti-la-jamhuri.html#ixzz2FxHcLY4L

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.