Naibu Katibu  Mkuu Bara wa chama hicho, Julias  Mtatiro
Naibu Katibu Mkuu Bara wa chama hicho, Julias Mtatiro

Chama Cha Wananchi (CUF), kimemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuingilia kati tatizo la uandikishaji wa watoto wanaojiunga elimu na darasa la kwanza kutozwa michango.

Akitoa taarifa kuhusu maadhimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, Naibu Katibu Mkuu Bara wa chama hicho, Julias Mtatiro alisema, watoto wote wenye sifa za kuanza elimu ya msingi wanapaswa kuandikishwa bila masharti na vikwazo vyovyote.

Hata hivyo Mtatiro alikuwa akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba.

Alisema, kipindi cha mwisho wa mwaka, wazazi wengi nchini wanakuwa katika harakati za kuwapeleka watoto shuleni ili wakaandikishwe kujiunga na elimu ya msingi.

Alisema hata hivyo wanakutana na vikwazo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutakiwa kulipa michango inayofikia hata jumla ya Sh50,000 katika baadhi ya maeneo.
Mtatiro alisema hali hiyo inawakatisha tamaa wazazi wengi na kwamba kuna haja kwa Serikali kuondoa kero hiyo.

Alisema Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Philipo Mulugo alilitolea tamko suala hilo na kuahidi kuwachukulia hatua kali wale watakaothubutu kutoza michango hiyo.

“Inaonekana ni kama kauli ya kisiasa zaidi kuliko uhalisia, kwani zoezi hilo linaendelea katika maeneo mengi ya nchi yetu na linaweza kuleta athari kubwa hasa kwa wananchi wasiokuwa na uwezo kifedha, watoto wao watakosa elimu,” alisema Mtatiro.

Pia alisema Baraza Kuu la Uongozi la CUF, limemvua uanachama Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Somanga Ndumo, wilayani Kilwa Yusuph Muhani, kutokana na uongozi mbaya.

Mtatiroa alisema kiongozi huyo aliingiza taasisi ya uhifadhi wa fukwe ya bahari kwa njia ya udanganyifu huku akijua kuwa inaathiri ustawi wa jamii ya wakazi wa kijiji hicho.

Alisema baraza kuu pia limemteua Hamad Masoud kuwa Naibu Katibu Mkuu kwa upande wa Zanzibar nafasi iliyoachwa na Ismaili Jussa Ladhu ambaye aliyeomba kuachia nafasi hiyo ili aweze kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Mji Mkongwe.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.