Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah,
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah.

Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Bhoke Ryoba, amefariki dunia baada ya kupigwa risasi na ofisa mwenzake wakati wakisherekea ufukweni mwa Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Afisa Uhusiano

“Tumekuwa tukipokea simu nyingi kutoka kwa watu wakihitaji kufahamu ukweli wa tukio la kupigwa risasi kwa mtumishi Bhoke Ryoba. Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, anapenda kutoa ufafanuzi kuhusu tukio hili kwamba ni kweli alifariki dunia Jumamosi (juzi) usiku baada ya kupigwa risasi,” ilieleza kwa kifupi taarifa hiyo.

Hata hivyo, taarifa ya Takukuru haikueleza chanzo cha mtumishi huyo kupigwa risasi wala eneo lilipotokea tukio hilo, lakini iliongeza kuwa uchunguzi kuhusu chanzo cha tukio hilo bado unaendelea kufanywa na Jeshi la Polisi.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke. Engelbet Kiondo, akizungumza na NIPASHE jana, alisema Ryoba alipigwa risasi na ofisa mwenzake, Mussa John (34), mkazi wa Mabibo, jijini Dar es Salaam.

Kamanda Kiondo alisema kuwa tukio hilo lilitokea katika eneo la ufukwe wa Hoteli ya Southern Beach saa 1:30 usiku wakati watumishi wa Takukuru walipokwenda kuburudika.

Kwa mujibu wa Kamanda Kiondo, wakati watumishi hao wakiburudika, ndipo mmoja wao, Mussa John, alipochukua bastola yake na kuanza kupiga risasi hewani.

Alifafanua moja kati ya risasi hizo, ilimpiga Ryoba na kumsababishia majeraha kifuani.

Baada ya kujeruhiwa, Ryoba alikimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya matibabu, lakini alifariki dunia usiku wa kuamkia jana wakati akiendelea kupatiwa matibabu.

Aliongeza kuwa baada ya tukio hilo, John alikwenda kujisalimisha katika Kituo cha Polisi Chang’ombe na anaendelea kushikiliwa.

Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Ahmed Msangi, na maafisa wengine wa polisi walikwenda eneo la tukio.

Kamanda Kiondo alisema katika mahojiano na polisi, John alisema kuwa alimpiga risasi marehemu kwa bahati mbaya.

Kamanda huyo alisema kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

CHANZO: NIPASHE

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.