Na Ahmed Omar

Kwa ukweli na kwa mkato kabisa, inatamkika hadharani kwamba Amani Karume ni mtu aliyeko ndani ya nyoyo za wazanzibari. Jambo hili lilikaa bayana Novemba 14, 2012 pale Rais huyu mstaafu alipoagana na CCM, kama Makamo Mwenyekiti wa Zanzibar kupitia mkutano mkuu uliofanyika Dodoma. Katika mkutano huo, Abdulrahman Kinana alitoa maazimio ya CCM, Pius Msekwa akitoa hotuba yake ya kuaga, na hatimaye Amani Karume naye akatoa hotuba yake ya kuaga.

Hotuba ya Karume ya Kuaga imekuwa na inaendelea kuwa gumzo na yenye kujadiliwa sana kati ya zote kutokea katika Mikutano Mikuu wa CCM. Kilichoifanya hotuba hiyo kuwa gumzo ni mzizi wa fitna za kuirudi na kuipinga hotuba hiyo na baadhi ya Wana-CCM Zanzibar.

Kwa yeyote aliyemsikiliza, alimuelewa, kama ilivyo kawaida, hakuweza kuficha furaha yake anayochukulia kuwa ni mwisho mwema wa mafanikio makubwa ya tangu alipoitumikia CCM, zaidi ya miaka 10, huku pia ukiwa muda wake muafaka wa kuwasilisha mawazo ya umma na pia kwa kuzingatia mtazamo wa chama chake.

Hapakuwa na hitilafu yoyote kutokana na kile alichokielezea, alijadili Historia ya CCM, Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, na Mchakato wa Marekebisho ya Katiba; Jukumu la Uongozi na Uongozi Bora; na pia furaha yake kuona damu changa au sura mpya zikiibuka ndani ya Uongozi wa CCM.

Kwa ufupi, juu ya Historia ya CCM, Karume alilikumbusha Taifa kwamba CCM ni Muungano wa Vyama Viwili, Afro Shirazi Party kutoka Zanzibar, na TANU kwa upande wa Tanganyika, ambavyo viliamua kuungana na kwa azma ya kuufikia ufanisi. Akataja namba ya kadi yake na akammhoji Rais Shein kama nay eye anayo kadi yake ya ASP.

Pia akakumbusha kuwa ASP bado ipo hai kwani wanachama wake wapo hai. Akatanabahisha warithi wasije kusahau azma ya Waasisi, hususan Waasisi wa ASP walioweka misingi imara, inayokwenda sambamba na utekelezaji wa dhati wa Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binaadamu; ili kuondosha hali zote za ubaguzi, ukandamizaji, na kadhalika.

Kuhusiana na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Karume alionelea kwamba hili lilikuwa ni chaguo la Wazanzibari wenyewe kwa asilimia 66, ya wingi wa Kura ya Maoni, lililopelekea Mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar, na hivyo CCM lazima iheshimu chaguo hilo.

Kwa upande wa Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unaoendelea sasa, Karume aliwataka wahusika wa Chama chake, pamoja na Viongozi, kuwacha watu watoe mawazo yao kwa uhuru, na hasa juu ya namna ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar; uhuru huo unaweza kutekelezeka pale ambapo mamlaka hazitowateza nguvu.

Hatimaye, Karume aliinasihi CCM kwamba inahitaji kushinda nyoyo na akili za watu, iwapo inataka kubakia yenye kukubalika, na hiyo inategemea utawala wa sheria na kwa heshima ya kujali, wala siyo kwa mabavu na vitisho.

Hata hivyo, wengi walishitushwa kupita kiasi, kutokana na ile fitna ya sumu mbaya, pale baadhi ya wafuasi wa Chama chake walivyoipokea na walivyoichukulia hotuba yake. Kwa wafuatiliaji wa habari wanajua kwamba baadhi ya Wana-CCM walikasirishwa mno na hotuba hiyo na waliamua kuirarua (kuichanachana) Picha kubwa ya Karume iliyokuwapo Michenzani, Zanzibar.

Kwanini makundi ndani ya CCM Zanzibar yakaguswa mno na maneno ambayo hayakuwa na lolote zaidi ya kueleza kwamba mamlaka ya Chama kuongoza inatokana na ridhaa ya watu, na ni watu hao ambao hapana budi kuwaheshimu, na kuachiwa wawasilishe mawazo yao kwa uwazi? Hii bila shaka ni athari mbaya ya kutofahamu historia ya ASP na ya Nchi yetu.

Baadhi ya Wana-CCM Zanzibar, kwa bahati mbaya wanashindwa kupambanua baina ya ukweli halisi na mitizamo yao. Utengamano huo sambamba unahamasishwa zaidi na harakati ya hivi karibuni ya kikundi cha takriban watu 50 hivi, akinamama na wasichana, wakiwa wamevalia sare za CCM, ambao kawaida hujiweka safu za usoni za mikutano; hawa ni kama kwamba huchochewa ghafla na mtu, nao wakaibuka kwa kuimba kwa kibwagizo cha Komando! Komando! Komando!

Kibwagizo hiki ni cha kuwahadaa watu na kuihadaa hadhira, ili iweze kuamini kuwa watu hao ni waumini wa dhati wa Raisi Mstaafu wa Zanzibar wa CCM mwaka 1990- 2000, Salmin Amour, aliyejipa mwenyewe jina la “Komando”, kutokana na hulka yake ya kukosa uvumilivu dhidi ya wapinzani hasa, CUF, na kuthibitisha imani hiyo pale alipowapeleka jela bila ya hatia, Viongozi 20 wa Chama cha Wananchi, CUF.

Vibaraka wahafidhina wanachohitaji ni CCM Zanzibar kutawaliwa na “Komando” katika himaya zake, hatimaye asisalimike “adui” yeyote kutokana na makucha ya chuma ya kundi hilo. Wapo wanaojidanganya vipembeni, chini ya vivuli vya Wahafidhina wa Chama, bado wakiamini kuwa na haki pekee ya kuendelea kutawala, ati waliikomboa Zanzibar kutokana na Usultani, na ati mabadiliko ya katiba yamewawacha solemba kama siyo kupotea kabisa, tena katika ulimwengu huu wa siasa makini za ushindani ambapo hata Watanzania wanahitaji kuchagua chama kipi kitawale na kinachowafaa kuwaongoza, wala si vinginevyo.

Vyema sawa! wote ambao wamediriki kutoa hisia zao na ambao waliitumikia Zanzibar kutoka katika makucha ya Usultani, sasa wameshafariki au vinginevyo ni watu wazima sana; hao hawakuongoza Mapinduzi ili hatimaye waje kufia ndani ya magofu ya Sultani yasiokuwa na kitu.

Kwa bahati mbaya, maadui wa kisiasa wa Amani Karume hivi sasa ni Wana-CCM wa Zanzibar, wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kusahau kabisa juu ya Maridhiano na Mabadiliko ya Katiba, yaliyopelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa; ambao bila shaka hawaridhiki na mfumo huu, wamekuwa wakiweka vizuizi na kunong’ona chini kwa chini, kutokana na kukosa ustahamilivu na pia ukosefu wa kubaini athari za mifarakano, ndiyo maana wanamvurumishia lawama Amani Abeid Karume, ati yeye ndiye aliyeasisi mizizi ya hili. Wapo waliokubali na kuridhia matakwa ya Wazanzibari; ingawa kwa Wahafidhina, hao ni wasaliti, kwa kuwa ni kinyume na matakwa yao.

Katika Mkutano wa hivi karibuni wa CCM uliofanyika Zanzibar, Wahafidhina wa CCM walitumia lugha chafu, matusi, uchochezi, na maneno yasiyofaa kuchochea na kukumbusha mambo yaliyopita ambayo yakitumiwa na Wanamapinduzi dhidi ya Wana-CCM waliodaiwa kuwa na msimamo wa wastani. Bila shaka malengo ya Mapinduzi ni kuondosha ubaguzi, ingawa yanatumiwa sasa na baadhi ya Wahafidhina kufungua na kurejesha majeraha ya zamani yaliyokwishapoa, ili kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Alichokifanya Amani Karume na Maalim Seif Novemba 5, 2009 kupitia Maridhiano na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ni pamoja na kulidhibiti kundi la wahafidhina lenye fikra potofu na misingi miovu ya KISONGE. Azma kubwa ya hili ni kuwafanya wazanzibari waongozwe na uzanzibari wao katika kuishi kwa amani na utulivu katika nchi yao na kuyatafuta maslahi yao kwa pamoja bila ya kujali tofauti zao.

Kuondoka kwa utawala wa Karume katika uongozi wa Nchi ya Zanzibar na CCM imechukuliwa na wahafidhina kua ni sawa na kuirejesha Zanzibar katika mikono yao na mtandao wao ndani ya sura mpya kabisa ya kuwateka nyara washirika wa Maridhiano hayo na serikali ya umoja huo wa kitaifa.

Tayari wahafidhina wameshajaribu kumchimba Dr. Ali Moh’d Shein aiwachie kamba ya maridhiano ambayo Amani Karume na Maalim Seif waliishika na baadae kumkabidhi Dr Shein aienzi. Dr Shein amekuwa kwa muda mrefu akishawishiwa kuwateka nyara viongozi wa CUF serikalini na kuwawacha kama wageni waalikwa wa GNU. Lengo ni kuwa viongozi hao wa CUF serikali wabakie hawana sauti yoyote yenye nguvu, si kimaamuzi wala kiushauri.

Timu iliyoasisi maridhiano na serikali ya umoja wa kitaifa ikiwemo kamati ya watu sita (six comandos) tayari limeshatangaza wazi msimamo wake wa kutaka mabadiliko ya muungano kutoka mfumo na muundo kandamizi uliopo sasa wa serikali mbili kwenda katika muungano wa MKATABA kupitia kongamano kubwa lililoitishwa hivi karibuni katika ukumbi wa Bwawani ili kuweka msimamo wao huo.

Baada ya hilo kufanyika kundi la wahafidhina limejaribu kumteka Dr Shein na kumfanya aamini kuwa wana CCM hawana haki ya kuweka msimamo wa mabadiliko ya mfumo na muundo wa muungano kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sera ya chama chao.

Akina Mansoor Yussuf Himid na Mzee Moyo ambao ni machampioni wa maridhiano ndani ya CCM wanaendelea kutishwa kwa kauli kali kali, kutukanwa, kufanyiwa vitendo vya kuwakatisha tamaa, na kudharauliwa kutokana na misimamo yao ya kudai mabadiliko ya mfumo wa muungano. Lengo ni kuwatisha na kuwafanya waamini kwamba fikra, misingi, ushawishi na nguvu za wahafidhina zimerejea katika safu yake ya awali na zimeshika hatamu upya.

Wanavyoamini wahafidhina akina Mansoor na wenzao watamini kwamba misingi, fikra na nguvu za maridhianao na serikali ya umoja wa kitaifa iliyotandikwa na Amani Karue na Maalim Seif bila shaka ishapigwa teke na wao watakuwa woga wa kusimamia misimamo yao ya mabadiliko.

Vitimbi kadhaa wa kadhaa vinavyoendelea dhidi ya harakati zote zinazodai mabadiliko, CUF, harakati za UAMSHO, akina Mansoor, Mzee Moyo nk ni suala moja tu, yaani ni vita dhidi ya umoja ambao wazanzibari wanaringia hivi sasa.

Hivyo vyote ni visu vinabadilishwa hiki na kile kuhakikisha kuwa kamba hii ya umoja iliyowaweka pamoja na kuwapa sauti moja wazanzibari bila kujali vyama vyao, asili zao, rangi zao wala historia za babu na bibi zao inakatwa ili wasambaratike wasifikie lengo walilolikusudia na badala yake nguvu ya wahafidhina zichukue nafasi yake. Amani Karume aliyapuuza mengi ya Dodoma na maagenti wao waliopo Zanzibar ndio umoja wa wazanzibari ukapatikana na serikali ya umoja wa kitaifa ukaundwa.

Aliamua kubakia zaidi kwao Zanzibar kuliko Dodoma. Aliamua kubaki na uzanzibari zaidi kuliko chama chake. Aliangalia maslahi ya Zanzibar na wazanzibari zaidi kuliko maslahi binafsi. Alimpigia debe Dr Shein ili awe rais na amrithishe kiti cha serikali ya umoja wa kitaifa kwa misingi hiyo hiyo ya kuangalia zaidi uzanzibari kuliko Dodoma kwenye chama chao.

Kitu cha kusikitisha sana ni kuona Dr Shein amekubali pole pole kutolewa katika mstari wa uzanzibari na kusogezwa zaidi Dodoma ambako wahafidhina ndiko wanakokuangalia zaidi, ndiko wanakokutegemea na ndiko kuliko na ushawishi na nguvu zao zote.

Anajaribu kupokea kila analoambiwa na wahafidhina na kila hila ya kuwaondoa wazanzibari katika agenda yao bila ya kufikiria kwa kina athari yake kwa kuogopa eti wahafidhina ndio waliomueka madarakani. Anajaribu tena kubariki vitendo vya chaguzi za KISONGE, za upigaji kura wa kimamluki, enzi za anjaribu kuunga mkono tena vita ya kuzuia mabadiliko ambayo wazanzibari wanayadai, anajaribu kubariki tena uundwaji wa vikundi vya uharamia na kufanywa vitendo vya uharamia na kuwasingizia wanaharakati wanaodai mabadiliko.

Dr Shein Amehamia KISONGE kwa kubariki bila ya hata kukemea matusi dhidi ya Amani Rais mstaafu Amani Karume, dhidi ya Makamo wa kwanza wa Rais, Maalim Seif, dhidi ya Muasisi na Mzee wa Nchi, Mzee Moyo, dhidi ya CUF, na dhidi ya watu wenye asili ya kisiwa cha Pemba.

Matusi hayo na kejeli yanachapishwa kila leo na wazi wazi katika mabango ya KISONGE huku yakilindwa na askari wenye silaha, katika vipeperushi, na magazeti ya wahafidhina wanamtandao likiwemo nipe habari. Amehamia KISONGE na kuamua kumfuta uwaziri Manssor Yussuf Himid kwa kosa la kudai muungano wa MKATABA kinyume na fikra ya wahafidhina.

Ahsante Amani Karume kwa kuwaona wahafidhina wa Zanzibar ni sawa na samaki. Tunaamini unazo sababu nyingi za kuwaita samaki. Kwanza, samaki hulana wao kwa wao. Pili, samaki ni rahisi kuwakamata kwa mitego wanayoiona kila siku. Tatu, wakongwe ndio wenye sauti. Nne, hata wakikusayika wengi hawawezi kuizuia meli isiwavue. Tano, siku zote hasira zao zinawanufaisha wavuvi. Sita, wakiona mwanga wa taa wanaukimbilia hata kama ni mtego kwao.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.