NDEGE YA TANAPA
Mabaki ya ndege ya TANAPA iliyopata ajali.

NDEGE ndogo ya abiria mali ya Hifadhi ya Taifa ya Tanapa yenye uwezo wa kubeba watu wanne aina ya C 182, imeanguka katika eneo la Kasimba umbali wa kilometa moja kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda uliopo katika Mkoa wa Katavi na kumjeruhi rubani wa ndege hiyo.

Akizungumza na vyombo vya habari, Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda, Maulid Mohamed alisema ajali hiyo ilitokea jana majira saa 10 .55 jioni katika eneo la Kasimba lililopo ndani ya Kijiji cha Nsemlwa wilayani hapo.

Mohamed aliitaja ndege hiyo iliyoanguka na kusababisha majeraha kwa rubani aliyetajwa kwa jina la Adam Athuman Kajwaa kuwa ni aina ya C182.

Mohamed alieleza kuwa ndege hiyo ilikuwa imetoka katika uwanja wa ndege wa Mpanda ikielekea katika Hifadhi ya Wanyamapori ya Katavi.

Hata hiyo alisema kuwa ajali hiyo ilitokea umbali wa kilometa moja na nusu kutoka Uwanja wa Ndege wa Mpanda mara baada ya kuondoka katika uwanja huo ambapo imeharibika sana sehemu ya bawa lake na upande wa injini.

Meneja wa uwanja huo wa ndege alisema taarifa za awali zinaonyesha chanzo cha ajali hiyo kilitokana na kufeli kwa injini ya ndege na kuwa rubani wa ndege hiyo alipata msaada wa kuokolewa na wananchi waliokuwa wakifanya shughuli za kilimo kwenye mashamba.

Mmoja wa wa mashuhuda wa tukio hilo Credo Mwanisenga alieleza kuwa wakati akiwa anafanya shughuli zake za kilimo ghafla aliona ndege hiyo ikiwa angani ikizimika na baada ya muda mfupi ikaanguka jirani na mti wa mwembe.

Hata hivyo alisema kuwa zoezi la kumuokoa rubani huyo lilichukua muda kuanza kutokana na mti wa mwembe kuwa na nyuki wengi.

Hata hivyo alisema mara baada ya kufanikiwa kumtoa rubani huyo, huku akiwa amepata majerahi makubwa sehemu ya uso na maumivu sehemu ya kifua na kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kwa matibabu zaidi,

Pia akiwa anakohoa damu, rubani huyo aliwahishwa haraka katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda baada ya kupata msaada wa gari la meneja wa uwanja wa ndege aliyefika eneo la tukio.

MWANANCHI

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.