Mwalimu Julius Nyerere
Mwalimu Julius Nyerere

Na Ahmed Omar

Kwa kauli yake, Julius Nyerere alikuwa akiumia kichwa sana na kukosa usingizi kutokana na kuwepo kwa nchi iitwayo Zanzibar pembeni ya nchi yake, Tanganyika. Alitamka wazi kwamba alitamani Zanzibar aididimize katika Bahari ya Hindi kama angeweza.

Hakuna mwanadamu mwenye uwezo wa kulitekeleza hilo, bila shaka, lakini ambacho Nyerere alikusudia ni kuiondoa Zanzibar katika ramani ya dunia na aidhibiti kwa kuiweka ndani ya viganja vya mikono yake, ndani ya mamlaka yake, amri yake, uendeshaji wake – aipe atakacho na ainyime atakacho.

Basi Nyerere akaanzisha vyema mradi wake huu kwa kulitumia vuguvugu la ukabila katika zama za kupigania uhuru lililoanzishwa na wakoloni kwa kulifanya mtaji wa kuwasambaratisha Wazanzibari na kuwagawa mafungu ili azma yake itimie, jambo hilo hilo ambalo alilipinga kwake, Tanganyika.

Alichokifanya Nyerere ni kulichukua kundi moja la Wazanzibari na kulipa maarifa ya umajumui wa Kiafrika (Pan Africanism) uliojengeka juu ya msingi kwamba kila mwenye ngozi nyeusi na mwenye asili yake kutokea Bara, ndiye Muafrika wa kweli, mzawa na mwenye haki za Kiafrika zitokanazo na ardhi ya Afrika. Kinyume chake ni kuwa mwengine yeyote ni mgeni Afrika na ni mgeni hivyo hivyo kwa Zanzibar ambayo ni sehemu ya Afrika.

Alilihamasisha kundi hilo kuwadharau na kuwaona wenzao kuwa hawana sifa ya kuwa Wazanzibari. Kupitia fitna hizo Wazanzibari wakachinjana na kuuana mara kadhaa wenyewe kwa wenyewe, wazawa wa visiwa hivi (badala ya wakoloni wao) katika zama za kupigania Uhuru na Mapinduzi ya 1964 na akatimiza mradi wake wa kuiweka Zanzibar katika mikono yake kupitia muungano wa kijanja wa 1964.

Kupitia muungano huo Nyerere aliyajengea rasmi misingi ya kisheria isiyo na mipaka na wala isiyohojiwa mamlaka yake ya kuidhibiti Zanzibar. Hapo ndipo ilipoanza enzi ya Wazanzibari kunyanyasika kupitia kitanzi cha Muungano.

Utawala wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea mwaka 1964 ulijaribu kwa nguvu zote kumzuia kila mtu mwenye mwenye asili ya kisiwa cha Pemba kushika nyadhifa za juu za serikali hiyo kwa shutuma kwamba eti Wapemba wananasibika na wapinga Mapinduzi ya 1964.

Nyerere alihakikisha anailinda na kuisimamia kwa nguvu zake zote misimamo hii ya wanamapinduzi ili aweze kujenga ridhaa ya mamlaka yake kwa Zanzibar kwa wanamapinduzi wa Zanzibar.

Hali hiyo ilikwenda hivyo hivyo kwa takribani miaka yote ya Muungano huu, hadi mwaka 2009, kwa mara ya mwanzo Wazanzibari walipong’amua mtego waliotegwa kwa umoja wao na kuanza kuelekea kwenye Maridhiano chini ya uongozi wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar wa wakati huo, Amani Karume, na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.

Sehemu inayofuatia ya makala hii, tutazungumzia namna Maalim Seif alivyokuja kuibuka kwenye siasa za Zanzibar, licha ya siasa za uwagawe uwatawale za Nyerere.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.