Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Bi Fatma Ferej
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Bi Fatma Ferej

Mwaka umetimia tangu tarehe kama ya leo mwaka uliopita (2011) nilipotoa taarifa ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani kupitia vyombo vya habari vya hapa nchini. Nategemea kwamba sote tunaelewa kuwa tarehe 1 Disemba ya kila mwaka Dunia nzima huadhimisha siku hii kwa madhumuni ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana na changamoto zinazotukabili katika mapambano dhidi ya janga hili la UKIMWI.

Ndugu Wananchi,

Yapo mafanikio mengi yaliyopatikana duniani kutokana na juhudi zilizofanyika ndani ya kipindi cha miaka kumi iliyopita. Dunia imeshuhudia kuwa juhudi kubwa za kitaalamu ambazo zinatokana na kufanyika kwa tafiti mbali mbali katika maeneo ya kinga na tiba. Juhudi za kubuni mikakati madhubuti inayotekelezeka na kuongezeka kwa uelewa wa jamii katika kulifahamu tatizo linalowakabili, pamoja na ushiriki wao mzuri ni mambo yaliyosaidia sana katika mafanikio yaliyopatikana.

Kwa mfano katika miaka hiyo kumi, maambukizo mapya yamepungua, vifo vinavyotokana na UKIMWI halikadhalika vimepungua na pia idadi ya watu wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU wameongezeka maradufu na sasa wanaishi kwa muda mrefu zaidi na kwa matumaini.

Ndugu Wananchi,

Mafanikio yaliyopatikana ni mengi na si rahisi kuyataja yote hapa. Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo bado changamoto zipo, nazo ni nyingi pia. Kwa mfano, pamoja na kuona kwamba viwango vya maambukizo katika nchi nyingi kwa jumla vimepungua, bado zipo nchi hasa kusini mwa jangwa la Sahara zenye viwango vya zaidi ya asilimia kumi (>10%). Aidha, ndani ya baadhi ya nchi moja moja yako maeneo yana viwango vikubwa vya maambukizi. Kwa mfano, wakati kiwango cha maambukizi ya VVU nchini Tanzania ni asilimia tano nukta saba (5.7) baadhi ya mikoa michache kiwango chake ni zaidi ya asilimia kumi (>10%).

Hapa Zanzibar wakati tunazungumzia kiwango cha maambukizi cha chini ya asilimia moja yaani zero nukta sita (0.6) (kwa kila watu 100,000 watu sita wameathirika na UKIMWI) bado katika baadhi ya makundi ndani ya jamii yetu yana kiwango cha zaidi ya asilimia kumi.

(>10%). Wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao MSM) asilimia kumi na mbili nukta tatu, (12.3), Wanaojidunga sindano za dawa za kulevya (IDU) ni asilimia kumi na sita (16) Wakinadada wanaojiuza miili yao ni asilimia kumi nukta tatu (10.3) na kwa Wanafunzi walioko katika vyuo vya mafunzo ni asilimia mbili nukta tano (2.5). Hali kama hiyo ni ya hatari kwani wakati wowote, kama hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa maambukizi yanaweza kutokea kutoka jamii yenye kiwango kikubwa kwenda kwenye ile yenye kiwango kidogo na hatimae kusababisha mripuko. Hivyo, inamaanisha kwamba bado tunayo kazi kubwa ya kufanya na wala tusidharau.

Kawaida kila mwaka tunapoadhimisha siku hii adhimu. Umoja wa Mataifa hutoa kauli mbiu. Kauli mbiu inayotumika mwaka huu wa 2012 ni ile ile ya mwaka jana, yaani kuzifikia zero tatu, kwa maana ya kuwa na zero katika maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI, kuwa na zero katika unyanyapaa dhidi ya Watu wanaoishi na VVU na pia kuwa na zero katika vifo vinavyotokana na UKIMWI. Tafsiri yake ni kwamba, tunatakiwa tuongeze nguvu zaidi ili tufikie hali ya kutokuwepo maambukizi mapya, kutokuwepo kwa unyanyapaa wa Watu wanaoishi na VVU na kutokuwepo kwa vifo vinavyotokana na UKIMWI ifikapo mwaka 2015.

Kauli mbiu hiyo inaonekana kuwa itaendelea hadi kufikia mwaka 2015 ambapo kila nchi itatakiwa ijitathmini imefikia wapi katika utekelezaji wake.

Ndugu Wananchi,

Wakati tunaelekea katika kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani hapo kesho, ni vyema sote kwa pamoja, jamii na taasisi zote tukakumbuka kwamba tuna wajibu wa kuchangia katika kufanikisha kuifikia kauli mbiu iliyowekwa yenye shabaha ya kuzifikia zero tatu.

Kwa mara nyengine tena, ninatoa wito maalum kwa taasisi mbali mbali na jamii kwa jumla kuwa lazima zitekeleze kwa vitendo, kwa kasi na ufanisi zaidi programu za UKIMWI ili kuhakikisha kwamba wanafikiwa lakini pia huduma za kinga na tiba wanazipata bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile, yakiwemo makundi maalum yaliyo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi.

Makundi haya ni yale ya wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao, wanawake wanaojiuza miili yao na watumiaji wa dawa haramu za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano. Makundi yote haya ni lazima kuyafikia kwa vile tafiti zinaonesha kuwa ndiyo yenye maambukizi makubwa zaidi kuliko maambukizi katika jamii kwa jumla.

Ndugu Wananchi,

Unayanyapaa ni kikwazo kikubwa bado kwenye jamii yetu kinachokwamisha juhudi zetu katika mapambano dhidi ya UKIMWI. Hivyo basi, hatuna budi kuendeleza juhudi zetu za kupiga vita unyanyapaa kwa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI. Aidha, nachukua nafasi hii kutoa wito maalum na kuwanasihi sana watoaji wa huduma za UKIMWI katika taasisi zote za Serikali na za binafsi kuendelea kufuata maadili ya kazi zao kutowabagua wala kuwanyanyapaa wateja wao wanaofika kwa kutaka huduma mbalimbali kwani haki ya kila mtu kupata huduma. Natoa wito huo pia kwa jamii kwa jumla kuacha tabia ya kuwanyanyapaa ndugu zetu wanaoishi na virusi vya ukimwi tukifanya hivyo, na kama tutafanya kazi kwa kushirikiana vizuri, tunaweza kupiga hatua kubwa katika kufanikisha malengo yetu ya zero tatu.

Ndugu Wananchi,

Huu ni mwaka wa 26 tokea UKIMWI ugundulike hapa Zanzibar. Kumekuwa na hatua nyingi sana zilizokwisha kuchukuliwa na Serikali yetu kuhakikisha kwamba ugonjwa huu hauenei na huduma za kinga na tiba zinapatikiana na pia misaada inayopatikana inawafikia wote wanaohitaji. Juhudi nyengine zilizochukuliwa ni pamoja na kupanua huduma za kinga, ikiwemo ya upimaji wa virusi, kuhakikisha usalama wa damu inayochangiwa wagonjwa na huduma za kukinga maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto , tiba ya magonjwa nyemelezi, dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI. Ushauri nasaha na mafunzo kwa wanaoishi na VVU. Hivyo, nataka nikiri kuwa yale yote ambayo tumeyatekeleza yamewezekana tu kutokana na mashirikiano mazuri kati ya Serikali, Washirika wa Maendeleo na taasisi zisizo za Serikali na wanajamii walio katika ngazi za shehia mbali mbali (Unguja na Pemba).

Tunayashukuru mashirika na nchi wahisani kwa misaada yao ya kifedha na utaalamu ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia sana katika kupanua na kuimarisha muitiko dhidi ya UKMWI nchini mwetu. Nachukua fursa hii pia kuzipongeza na kuzishukuru taasisi zote za ndani, za Serikali na zisizokuwa za Serikali zikiwemo taasisi za kidini zinazoshiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya UKIMWI. Tunawaomba wasichoke na badala yake waendelee kushirikiana nasi katika vita hivi kwa maslahi ya taifa letu na wananchi wetu kwa jumla.

Ndugu wananchi,

Ningependa kutanabahisha kuwa kwa muda wote wa mapambano tumekuwa tukitegemea sana misaada ya wafadhili ambayo kwa kiasi kikubwa sasa imepungua. Wakati umefika sasa kuliona tatizo la UKIMWI ni letu na kwamba sisi tunawajibika kupambana nalo kikamilifu kwa kutumia rasilimali zilizo ndani ya uwezo wetu, wafadhili watusaidie kwa yale mambo yaliyo nje ya uwezo wetu. Ninashukuru sana kuona kwamba Kamati za UKIMWI za baadhi ya Shehia zimeliona hilo na kutayarisha mipango madhubuti ya kukabiliana na changamoto wanazoziibua wenyewe katika Shehia zao na kukabiliana nazo, bila ya kutegemea wafadhili. Ninatoa wito kwa Kamati za Shehia nyengine ambazo bado hazina mipango hiyo zijifunze kwa wenzao ili ziandae mipango endelevu. Kwa kufanya hivyo hivyo vita vyetu na ushindi wetu utakuwa wa uhakika zaidi.

Ndugu Wananchi

Kwa kuwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia uratibu wa shughuli za UKIMWI hapa Zanzibar, napenda kutoa wito kwa wananchi na wadau wote kushiriki ipasavyo katika kilele cha maadhimisho haya ya siku ya UKIMWI ambayo kwa mwaka huu wa 2012 yatafanyika katika Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini huko Mangapwani ambapo mgeni rasmi atakuwa ni Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Juma Duni Haji. Katika maadhimisho hayo kutakuwa na shughuli mbali mbali zikiwemo huduma za kupima virusi vya UKIMWI bila ya malipo na burudani zinazolenga maudhui ya maadhimisho yetu. Nyote mnakaribishwa.

Ndugu wananchi,

Mwisho lakini sio kwa umuhimu , nachukua fursa hii kutanguliza shukrani za dhati kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na kutoka kwangu binafsi, kwa uongozi wote wa Mkoa wa Kaskazini na Wilaya zake zote mbili kwa mashirikiano mazuri katika kufanikisha maadhimisho haya.

Tukumbuke kwamba:

ZANZIBAR BILA YA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU

ZANZIBAR BILA YA UNYANYAPAA WA WATU WANAOISHI NA
VVU NA

ZANZIBAR BILA YA VIFO VINAVYOTOKANA NA UKIMWI INAWEZEKANA
AHSANTENI

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.