Jengo la Mahakama ya Wilaya, Chake Chake, Pemba.

Mahakama ya wilaya ya Chake Chake, Pemba, imewapandisha kizimbani askari watatu kutoka Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) kwa tuhuma za ubakaji. Mwendesha Mashtaka, mkaguzi msaidizi wa polisi Gongo Shaaban Gongo, amewataja askari hao kuwa ni Abdu Khamis, Hafidh Yussuf Masoud na mmoja aliyejuilikana kwa jina moja la Adibu na ambaye hakuwepo mahakamani hapo.

Mahakama, chini ya Hakimu Mcha Hamza, imeelezwa na upande wa mashitaka kwamba askari hao kwa pamoja walimbaka mtoto wa miaka 18 siku ya Jumatatu ya 29 Oktoba 2012 saa 2:00 usiku walipo kuwa kazini katika eneo la ZSSF huko Chake Chake, Pemba. Upande wa mashitaka umesema kwamba watuhumiwa hao walitenda kosa hilo lililo kinyume na sheria kwa mujibu wa Kifungu Namba 127{1} Sheria Namba 6 ya Mwaka 2004 ya Zanzibar.

Watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kisheria wa kusikiliza kesi hiyo na kesi hiyo imeakhirishwa hadi itakapotajwa tena tarehe 2 Disemba 2012.

Mahakama iliweka masharti ya dhamana kwa kila mmoja kuwa kiasi cha shilingi 500,000 za maandishi na wadhamini wawili ambao kila mmoja awe na kiasi kama hicho ikiwa mmoja ni mfanyakazi wa serikali.

Stori na Hamed Mazroui, Zanzibar Daima

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.