Ningetamani rais wangu awe rais….

Mimi ni Mzanzibari. Nina imani na taasisi halali za utawala katika nchi yangu. Ningelipenda taasisi hizo ziwe huru na siasa za vyama, ili zinapovurunda tuweze kuzikosoa, bila kujivika wala kuvishwa magwanda ya vyama vya siasa.

Ningetamani uraisi kama taasisi, kwa mfano, uwe chombo cha utawala ulio mbali mno na vyama na, kwa hivyo, rais auvae uraisi wa nchi na sio uongozi wa chama. Kwa kufanya hivyo, angeliweza kujipa nafasi ya kukosoleka kama rais na sio kama chama.

Lakini hebu angalia hotuba za Rais Ali Mohammed Shein ambazo amekuwa akizitoa ndani ya kipindi hiki cha mwezi miezi miwili. Amekuwa akisema na kurudia kiapo cha kuviandama vile anavyoviita “vikundi vinavyojificha nyuma ya dini kufanya fujo“. Mintarafu hapa ni jumuiya ya Uamsho.

Amekuwa akizitoa kauli hizi hata baada ya viongozi wa Uamsho kukamatwa na kufunguliwa kesi mahakamani. Kwa mtu kama yeye aliyetokea kwenye uwaziri wa utawala bora, haitoshi kumkumbusha kwamba anaingilia uhuru wa mahakama na anashawishi uamuzi wa mahakama hizo.

Haitoshi kumkosoa kwamba anazungumzia “wasababishaji fujo“ wa Uamsho, lakini anapuuzia mateso ya mamia ya raia wanaovamiwa na vyombo vya dola na makundi ya kihuni yanayoungwa mkono na dola.

Ningetamani mno kwamba Rais Shein asimame kama rais wa nchi na si mwakilishi wa maskani ya chama chake. Ningelitamani sana kiongozi wangu awe kiongozi.

Lakini ni bahati mbaya sana taasisi ya uraisi katika nchi yangu, nayo pia haiko huru kutokana na siasa chafu za ubabe na vitisho vilivyojengwa juu ya misingi ya chuki na ubaguzi. Ubaguzi ambao, kwa hakika, unamgusa hata yeye mwenyewe.

Laiti dhamira ya Rais Shein ni kutekeleza wajibu wake wa kusimamia amani na utulivu, basi angelisimama kama rais wa nchi na hivyo akaelekeza hatua za kuisimamisha amani kwa dhati yake. Amani ni matokeo ya imani, na imani hujegwa. Viashiria vya kuibomoa vinapokuwa wazi, bila ya shaka ni wajibu wa serikali kuvizima.

Lakini unapata jibu gani pale Rais wa nchi anapowakamata watu wa upande mmoja kwa “kusababisha uvunjifu wa amani“, lakini akawaacha na kuwaruhusu wa upande mwengine kuivunja kabisa amani hiyo, kwa kauli za matusi, ubaguzi na chuki?

Unafahamu nini upande mmoja ukikandamizwa na vyombo vya dola “kwa sababu ya kutoa kauli za kuvuruga amani“, lakini upande mwengine ukipanda viririni, ukiandika mabango na ukichawanya makaratasi ya kuhubiri chuki, utengano na machafuko!?

Je, inapotokea kwamba upande unaopigwa mabomu na kukumbwa na kisago kikali ndio upande huo huo unaokamatwa na kufikishwa mahakamani, na ndio wao wenye historia ya kuupinga msimamo wa Rais wa nchi na chama chake kuelekea muundo wa Muungano, kweli itakujia kuwa dola inapambana na wasababishaji fujo au inapambana na wapigania mabadiliko kwenye mfumo wa Muungano!?

Ningelitamani rais wangu awe rais!

One thought on “Ningelitamani Rais wangu awe rais….”

  1. Tunapenda rais wetu awe Maalim Seif. (ila wasojua wajue lazima Tufanye kitu juu ya hili la sio hivyo Tunajidanganya mkono wa kanisa utabaki pale pale…..

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.