Mwaka 2010, wakati mimi na mwenzangu mmoja (ambaye sitamtaja jina hapa kwa sababu ya nafasi yake sasa serikalini), tulikuwa tukishiriki kampeni za NDIO kwenye Kura ya Maoni ya Zanzibar. Ziara zetu zilitufikisha mwingi Unguja na Pemba. Ukweli mmoja tuliuona, tuliujadili na ulitutia khofu. Ukweli wenyewe ni kwamba kundi la wahafidhina kwenye Chama cha Mapinduzi (sisi tukiwaita Taliban), walikuwa hawayataki kabisa Maridhiano na walipinga wazo la Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Baya zaidi, tulikuwa tunawaona walivyokuwa wamejipanga kimkakati kutokea mashinani kabisa hadi juu. Hadi ndani ya serikali iliyokuwa ikiongozwa na muasisi wa Maridhiano, Rais Mstaafu Amani Karume, walikuwa wamejaa kibao. Tulikuwa na ushahidi wa mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi na maafisa wengine wa Chama na Serikali ambao walikuwa hadharani wanasema wanamuunga mkono raisi wao, lakini magharibi wanakwenda majimboni kupiga kampeni ya HAPANA!

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein (katikati), Makamo wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif (kushoto) na mtangulizi wake Amani Karume
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein (katikati), Makamo wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif (kushoto) na mtangulizi wake Amani Karume

Hilo halikututia khofu kwamba kura ya maoni ingelishindwa, bali ukweli kwamba hata kama ingelishinda, basi isingelikuwa kwa kura za sehemu hiyo ya Wazanzibari, ambao kwa tabia yao wasingelikubali kushindwa. Kikwazo tulichokiona kingelikuja baadaye, kwenye utawala wa raisi atakayefuatia kama angelitokea CCM. Suluhisho tuliliona lilikuwa limeonekana na wengi wakati huo: kwamba aidha lazima raisi ajaye asitoke CCM au kama kuna uwezekano, basi Rais Karume aongozewe muda. Yote mawili hayakuwezekana!

Huu ndio ukweli uliopo sasa mbele ya macho yetu. Wahafidhina wa Zanzibar, wakiongozwa na maslahi yao binafsi waliyoyabatiza jina la maslahi ya chama, wanaifanya serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ikose roho. Maana roho ya serikali hiyo ni Maridhiano. Serikali hii inaweza ikawa na muili na damu, maana ina muundo wake na uhalali wake kwenye Katiba ya Zanzibar. Ina sifa zake kwenye jumuiya ya kimataifa. Ina faida zake kwa maisha ya kila siku ya Mzanzibari. Lakini roho yake ni kukubalika kwake na pande zote husika na zenye nguvu. Upande wa wahafidhina wa Zanzibar, hauikubali.

Na kwa kuwa ukweli mwengine uliopo wazi ni kuwa chama chao cha Mapinduzi kina nguvu na mashiko yake upande wa Tanganyika, na kwa kuwa wanajua kila siku kuwatisha wenzao wa Tanganyika kuhusiana na hatima ya madaraka na utawala wao, basi wameishika Zanzibar kwenye mshipa wake wa fahamu.

Nakusudia kuwa wanachofanya ni kutumia khofu za kuvunjwa kwa Muungano na Maridhiano, ili kupata uhalali na msaada wa kuyavunja Maridhiano hayo na Umoja wa Kitaifa wa Wazanzibari. Kama ilivyokuwa kwa Mwalimu Julius Nyerere, ndivyo ilivyo kwa watawala wengine wote waliofuatia kwenye Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam. Wakitishiwa tu kuwa Muungano huu utavunjika, basi wako tayari kusalimisha chochote na kutumika kufanya lolote dhidi ya Wazanzibari, alimradi Muungano udumu.

Ndivyo ilivyokuwa. Ndivyo itakavyokuwa.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.