Dk. Ali Mohamed Shein akirudi Dodoma

Na ZDaima, Mzalendo.Net

Kile kilichojidhihirisha Dodoma hapa majuzi hakitapita bure. Kwa waungwana na watu wenye upeo lazima wajiulize kunani kiasi cha aliyekuwa kipenzi cha wana-CCM kwa miaka 10, mtu aliye akishangiliwa na kusifiwa kwa kila hali na kupachikwa majina ya kumpongeza na kumsifu, sasa anazomewa hadharani katika kikao kizito cha chama chake!?

Hii ndio dunia na kadhia hii inatukumbusha jambo moja muhimu: hatma njema. Mimi niseme Dk. Amani Karume kuzomewa na wana-CCM kwa kujihidhirisha katika kikao chao, ndio hatma njema kwake. Hongera sana Karume. Lakini kazi anayo sasa Rais Ali Mohamed Shein
.

Kiini cha Mambo

Kila mmoja wetu anajuwa kwamba kilichomshushia hadhi Rais Mstaafu Karume mbele ya wana-CCM wenziwe, ni ile kuvunja mwiko wa kuwaunganisha Wazanzibari. Kwani hali hiyo huwakosesha usingizi wabinafsi wahafidhina na wanaojali maslahi yao zaidi kuliko ya nchi. Ili kupata kwao uluwa, siku zote wamekuwa wakitumia utengano wa Wazanzibari.

Bahati mbaya sana hawa jamaa wana ushawishi na, kwa tathmini ya haraka, ndio ambao wameingiya kwa wingi katika NEC na CC ya CCM. Ikiwa leo Dk. Karume asulubiwe na wanachama wenzake kwa kuwafanyia wema Wazanzibari ataachwa Dk. Shein ambaye hakuwa chaguo la wahafidhina hao!? Lazima azomewe tu.

Hali ya Mambo kwa Dk. Shein

Kiukweli Dk. Shein amezungukwa na wahafidhina ambao ndio washauri wake wa chama na serikali. Siri za hivi karibuni zilizoenea katika sakata la kushikwa viongozi wa Uamsho ni dhahiri Dk. Shein kaelemewa au hashauriki. Suali ni je, atakuwa tayari kuvunja umoja na mshikamano wa Wazanzibari, ili aendekeze maslahi ya wahafidhina na wabinafsi na kuwarejesha kule walikotoka au atalinda Maridhiano yaliyosababisha Karume azomewe na kujiletea heshima kwa umma wa Wazanzibari na ulimwenguni kwa jumla?

Hapa ana hiari yake lakini kwa hali ilivyo ajiandae kuzomewa muda si mrefu. 
Ikiwa atakubali kuburuzwa na wahafidhina na kusahau tunu ya watu wa visiwa hivi kwa nusu karne sasa ajiandae kuzomewa na Wazanzibari na atambuwe dunia imebadilika na au atazomewa na dunia!? Mazingira yanaonesha hivyo, ila ni suala la muda tu.

Kwa upande wa pili, atazomewa kwa karibu zaidi na maswahiba zake maana yale mazoweya ndio imekuwa sharia na usipokuwa mbaguzi, mbabe, ghilba na vitisho kamwe hutakiwi CCM Zanzibar. Maana ndio mtaji wa CCM, ili ishinde Zanzibar na je, atakuwa tayari kuvunja mwiko huo!? Akithubutu tu asubiri kuzomewa kabla ya wakati. Itakuwa ni afadhali Dk. Karume kazomewa mwisho, sasa lipi la muhimu? Ngoja tuone.

2 thoughts on “Baada ya kuzomewa kwa Karume, zamu ya Shein inafuatia?”

    1. Paul Mabere, mbona mwenyewe Mansour anasema yeye ni kizazi cha mchanganyiko wa Kiafrika na Kiarabu kama ilivyo sehemu kubwa ya Wazanzibari!? Au hujasoma makala yake ya wiki iliyopita? Hebu angalia hapo mbele ya Zanzibar Daima kuna makala inasema “Zanzibar ni yetu sote” iliyoandikwa na Mansour!!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.