Na Mansour Yussuf Himid

Leo nami nimeamua kutoa mawazo yangu kupitia kwenye ukumbi huu. Kwa wale wasionifahamu mimi ni Mansoor Yussuf Himid nimezaliwa Novemba 3, 1967, kisiwani Unguja. Ni Mzanzibari kwa mama na baba. Kama walivyo Wazanzibari wengine, wazee wangu pia wana asili ya pande mbili – Bara na Arabuni. Baba yangu mzazi ana asili ya Bara ambapo upande wa baba yake ni Mnyasa na upande wa mama yake ni Mmanyema. Na mama yangu ana asili ya Arabuni (Oman), lakini ni mseto wa aina yake maana ana damu ya Kimanyema, Kisomali, na Kingazija. Hali hii si ya ajabu kwa Wazanzibari, bali ni kawaida tu na ndio hali inayotutambulisha Wazanzibari.

Mimi ni Mtanzania kama walivyo wazee na ndugu zangu na wanangu na mke wangu Asha Abeid Amani Karume, kama unajiuliza Karume yupi ni huyo huyo unayemfikiria wewe ni Marehemu Abeid Amani Karume, Baba wa Taifa la Zanzibar , mungu amlaze pema peponi na amsamehe kwa mapungufu yake na amjaalie aendelea kutajwa kwa kheri na wema kama anavyo tajwa sasa.

Marehemu mzee Karume ana haki ya kuitwa Baba wa Taifa la Tanzania pia na wala mshishangae kwani Marekani Taifa la kupigiwa mfano kwa historia na misingi yake imara ya haki za binadamu,demokrasia na utawala bora , wana baba wa Taifa (Founding fathers) zaidi ya mmoja.

Kwa wengine nikiwemo mie kutothaminiwa kwa marehemu Bwana Abeid Amani Karume kwa kuitwa muasisi tu tena wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wala sio Nchi au Taifa la Zanzibar au Tanzania ni kutothamini mchango wake katika kuasisi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani bila ya Zanzibar hakuna Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ni sehemu ya kero za Muungano wetu.

Tuelewe kuwa kwa kumthamini marehemu Sheikh Abeid Amani Karume, hatuondoshi nafasi ya Marehemu Mwalimu Julius kambarage Nyerere hata kidogo,nafasi ya Mwalimu ni kubwa mno (iconic) kwa wengine iliotukuka (saintly) sio tu kwa Tanzania na Afrika bali mwenyezi mungu amemjaalia Mwalimu kuthaminiwa na kupendwa na mataifa duniani kote,mpaka hii leo miaka kadha baada kufariki kwake, sababu za kupendwa kwa Mwalimu akiwa miongoni mwa viongozi wachache duniani wenye hadhi kama yake ni nyingi kwa leo si dhamira yangu kueleza wasifu wa Marehemu Mwalimu Nyerere.

Sasa nieleze nilioyakusudia. Historia ya Zanzibar imeandikwa sana sina haja kuirejea, dhamira yangu ni kuzungumzia hali ya kisiasa, kijamii Zanzibar ya sasa na mchakato wa marekedisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Hivi sasa Zanzibar ina Serikali yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa kwa jina fupi SUK au la kizungu ‘Government of National Unity’ (GNU) Serikali hii haikuja tu kwa sababu kulikua na watu wana mapenzi nayo au kwa kutaka kukisaliti Chama Cha Mapinduzi na Mapinduzi yetu Matukufu ,hapana palikua na haja tena haja hiyo ilikua kubwa na ya msingi.

Haja hiyo imetokana na Historia ya Zanzibar na siasa za vyama vyetu na Mapinduzi yenyewe, haja ya kujenga misingi ya siasa na utawala Zanzibar inayo heshimu haki za binadamu,utawala ulio bora,Wazanzibari kuhakikishiwa uhai wao ,Uhuru wao, fursa na haki ya kujiendeleza ndani ya Nchi yao na kupata hudumu za kijamii na kushiriki siasa bila ya kubaguliwa, ambapo la muhimu kuliko yote ni Wazanzibari wote bila ya kujali kabila,dini,rangi,eneo analotoka kuwa sawa mbele ya sheria na utoaji wa haki, misingi hii pamoja na kuitangaza Zanzibar kuwa Jamhuri ili kuondosha nafasi ya Wazanzibari kutawaliwa, misingi inayoheshimu haki za binadamu na isiyokuwa na chembe chembe za kibaguzi na utengano ndio iliokuwa ya mwanzo kutangaziwa Wazanzibari na Marehemu mzee Abeid Amani Karume baada ya Januari 12 mwaka 1964.

Zanzibar kwa miaka mingi kabla na baada ya Mapinduzi iligubikwa na inaendelea kugubikwa na siasa za chuki,hasama na ubaguzi na zisizo toa nafasi kwa binadamu kustahamiliana , dhamira ya Mapinduzi ni kuondosha mazingira hayo na kuwaunganisha Wazanzibari, kwa bahati mbaya hali hii ya utengano iilijirudia upya baada ya ujio wa vyama vingi mwaka 1992, miafaka mingi tumepitia bila ya mafanikio na nchi hii kushindwa kutafuta dawa ya kudumu.

Yote hayo (haja) ni katika kutafuta dawa ya kudumu ili Wazanzibari waishi kwa salama,kwa upendo, kuheshimiana, kustahamiliana na muhimu zaidi kuvumiliana,na siasa zao zisiwe ndio chanzo cha kugawanywa kwao bali siasa iwe chachu ya maendeleo yao na waweze kuishi kwa kushiriki siasa na kupenda vyama vyao bila ya kuchukiana,kubaguana na kuuwana ,na vyama hivyo visiwe sababu ya kuhasimiana kwao bali sera,ilani na itkadi za vyama ziwe dira ya maendeleo yao.

Kwa msingi ule ule wa demokrasia Wazanzibari waendelee kuendesha siasa kwa kukubali kutokukubaliana kiungwana na kwa kuelewa kwamba nguzo yao ni Zanzibar na wote ni Wazanzibari tofauti ni vyama vyao tu, lakini kila mmoja ana haki sawa na mwenziwe kuchagua apendako bila ya kubatizwa majina mabaya au kutengwa na sehemu ya jamii au kubughudhiwa na mtu yoyote iwe Chama cha siasa au Serikali na wakielewa kwamba vyama vyote vya siasa mwishowe vinahitaji watu na watu wanahitaji maendeleo ,kujitambua,usalama,amani na muelekeo thabiti wa Nchi yao.

Malumbano yasio na msingi isipokua huyo Mpemba na huyo Muunguja, huyu CCM na huyu CUF hayana tija wala mwisho mwema,Vijana wa Kizanzibari hawapati kazi ,elimu,huduma muhimu za kijamii wala matumaini ya maisha yao kwa U-Pemba na U-Unguja na kupelekwa pabaya na wanasiasa wanao hubiri chuki, ubaguzi na utengano,kwa bahati mbaya wengi wetu wanasiasa tumetenda na tunaendelea kutenda dhambi hizo tena wa vyama vyote CCM na CUF.

Dhana iliyopo ni kwamba wahafidhina wapo CCM tu,si kweli hata CUF wapo,zao la uhasama,ubaguzi na chuki ni watu kuvunjika moyo (frustrated) kukosa muelekeo na imani juu ya nchi yao na viongozi wao na nchi yetu kuendelea kuwemo ndani ya mzunguko (vicious circle) usio na mwisho wa hasama,chuki,ubaguzi, na kukosa muelekeo,na kuaminiana, wapi tunakotoka, wapi twendako,yepi ya maana tunataka kuyatekeleza na nini hasa dira ya Nchi yetu na nini tunataka kurithisha kizazi kijacho,kauli mbiu za wanasiasa zinazo ashiria ubaya na mivutano isiokwisha au Zanzibar yenye muelekeo na matumaini kwa walio hai leo na kizazi kipya?

Wajibu wa watu katika jamii ni kuwiana hisani,usawa,adabu,heshima na mapenzi na kwa kiungo hichi cha johari ya kuwiana Wazanzibari tuliweza kuridhiana na kuungana katika ujenzi wa nchi yetu. Kama nilivyosema awali,wajibu huu hapa Zanzibar ulimezwa na siasa za chuki, ubaguzi wa kutisha ambapo watu pengine wa kiambo kimoja au hata familia moja waliwiana chuki,kisasi na makamio huku pumzi ya kila mmoja ilijaa hofu,kushupaliana, sumu juu ya sumu.Inshaallah Mwenyezi Mungu atuepushe na ubaya na hatari hiyo leo na twendako.

Hatua iliyo fikiwa sasa ya kujenga Zanzibar mpya baada ya ujasiri na muono thabiti (vision)wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kutafuta dawa ya kudumu itakayo ondosha kabisa siasa za chuki,hasama na za kibaguzi ziliopo Zanzibar ilikuwa ni hatua sahihi yenye uzalendo ndani yake kwa ujenzi wa Zanzibar mpya na tuitakayo.

Dk. Jakaya Kikwete tulimlaani sana wenziwe huku Zanzibar na yeye kumwita msaliti wa Mapinduzi kwa kutaamka kwamba Zanzibar kuna mpasuko wa kisiasa na hali hiyo inamsononesha na kubwa zaidi kwamba hali hiyo inahitaji dawa, tena dawa chungu mno ya kushirikiana na adui mpinga Mapinduzi? lakini ukweli ukaendelea kubaki kuwa ukweli na wahenga wamesema ukweli ukidhihiri uongo hujitenga,muda ukapita busara zikatawala na tulio wengi tukakubali ukweli kwamba chuki,ubaguzi,hasama,vifo na majonzi ya mwaka nenda mwaka rudi sio njia sahihi,bali tunawajibu wa kutenda yale pengine tunayoyachukia, lakini kwa dhamana tulionayo na ubinadamu tunawajibu wa kubadilika.

Kwa upande mwengine,Ujasiri na upeo mkubwa wa Dk. Amani Abeid Karume Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (mst) ni kutambua na kukubali kwamba Nchi anayoiongoza inaumwa na siasa zake zinakwenda kinyume na dhamira ya kweli ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964 na yeye kutokukubali kumuachia mrithi wake maradhi aliorithi yeye huku akijua kwamba hatua hiyo itamchukiza sana sana kwa baadhi ya wenziwe walio wahafidhina (zealots) pamoja na mazingira hayo magumu yeye alichukua hatua ngumu lakini sahihi ya kuwataka Wazanzibari wenyewe wafanye maamuzi juu ya hatma ya Nchi yao,na kupitia kura ya maoni Wazanzibar walio wengi wakamua kwa sauti moja kwamba wamechoka na siasa za mivutano na hasama,kiongozi makini na mwema anapaswa kuongoza sio kuongozwa na huo ndo mtihani wa uongozi,tuseme tusemavyo lakini Dk Karume na Maalim Seif wamefuzu mtihani huo wa uongozi.

Huku kwetu Zanzibar ni dhambi kubwa kumtaja tu kwa vizuri kiongozi wa upinzani ,seuze kummiminia sifa, hiyo ni dhambi kubwa zaidi isio na mfano,humalizii tu kuitwa msaliti wa Chama chako na Mapinduzi bali utaitwa Hizibu(Zanzibar Nationalist Party-ZNP) namba mbili, namba moja akiwa Jamshid mwenyewe (Sultani wa mwisho Zanzibar) , Hizbu likiwa ndo tusi baya na la mwisho kupewa mwanasiasa Zanzibar hasa anaetokana na CCM ,lakini ukweli ni kwamba Maalim Seif Sharrif Hamad anastahili kila sifa ya kuacha utashi wa nafsi yake na wa Chama chake kwa kuweka maslahi ya Zanzibar mbele, na kukubali dhamira njema ya CCM na hatimaye kushirikiana na CCM kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kujenga mustakbal mwema wa Zanzibar na kizazi chake.

Siku zikapita,miezi ikayoyoma na hatimaye ni Rais Kikwete yule yule kwa kuthibitisha umakini,busara na wingi wa hekima ya uongozi wake amethubutu,ameweza kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nilimsikiliza kwa makini wakati akizindua Tume ile pale Ikulu Dar es Salaam kubwa alilotuasa ni kuweka mbele uzalendo na maslahi ya Taifa letu kwa kila mmoja kutoa maoni anayodhani yatasaidia katika kupata katiba mpya.

Kwetu sisi Wazanzibari katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatugusa katika baadhi ya mambo ambapo kati ya yote hayo kilele cha umuhimu ni suala zima la Muungano ambao umetimia miaka 48 tangu kuundwa kwake mwaka 1964. Ukelele wa mabadiliko ya muundo wa Muungano ulikuwa katika kila pembe ya viunga vya Zanzibar, kule Mtende Makunduchi, Kijini, Kibuteni,Jambiani, Ndijani, Uzini, Bambi, Umbuji, Pongwe,Uroa,Chwaka,Mkwajuni, Nungwi, Matemwe, Limbani, Jadida, Wete, Ziwani, Wambaa, Chake Chake ilimradi kila pahala.

Kwa bahati mbaya,tunataka kurudishwa kwenye siasa za chuki,hasama na kutoheshimiana na kuvumiliana hata kwa mawazo,kila anaezungumza kwa kutaka mabadiliko katika mfumo wa Muungano basi tayari ni msaliti wa Chama chake na Mapinduzi, utafikiri Chama na Mapinduzi ni hati miliki ya baadhi yetu,wengine sote sio,huna haki ukiwa Mtanzania na Mzanzibari kueleza kwa upeo fikra zako juu ya namna unavyotaka Muungano wako uwe kwani huu Muungano ni wa Watanzania wote kama hawakusema wao atasema nani,na kwanini tusiseme ni Haki yetu kusema,Watanzania hatukuwasemea Wakenya wakati wanarekebisha Katiba yao wamesema wenyewe.

Nakubaliana na raia wenzangu na Serikali yangu kwamba katika mchakato huu hatupaswi kukubali kutoa nafasi kwa wanao hubiri utengano, ubaguzi,udini, na matumizi ya lugha chafu na za kibaguzi pamoja na kutumia fujo kama njia ya kufikia malengo yao na wote wanaofanya hivyo wanapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria kwani tunako toka kubaya sana,hatupaswi Wazanzibari wenye akili timamu kushabikia vurugu tutajimaliza wenyewe maana wazee wanasema vita vya panzi neema kwa kunguru!

Lakini papo hapo sikubaliani hata kidogo na dhamira ya wachache kutaka kuwanyima wananchi wa Zanzibar haki na uhuru wao wa kutoa maoni yao kwa kisingizio chochote kile iwe vitisho,iwe kushurutishwa na kupangiwa,iwe kwa kubatizwa majina ya Uhizibu,usaliti wa Mapinduzi na Chama kwani naamini hatuwezi kupata Katiba na muundo wa Muungano ulio bora kwa kuviza maoni na matumaini ya watu, tukumbuke kuwa kwenye wengi hapaharibiki jambo nami naamini kwa uelewa wa wananchi hakuna jambo litakalokwenda kombo zaidi ya kuhuisha mahusiano ya kale baina ya watu wa Zanzibar na Tanganyika.

Tukifikiri vyenginevyo, tutakuwa tunazidanganya nafsi zetu na hatutafika kwani siku zote watu makini hawapaswi kuhofia mawazo ya wenziwao kwa visingizio vya wanataka kumrudisha Sultan na kuvunja Muungano! haya ni mawazo tu si risasi wala mzinga iwe Muungano wa Serikali mbili, tatu,mkataba au mfumo wowote ule mujarab utakao tuondosha hapa tulipo kwenda kuzuri zaidi penye heshima, na tunakhofia nini kwani Wazanzibari tulio wengi Muungano tunautaka na sisemi haya kwa kebehi au kujikosha na kujipendekeza hapana.

Kama husadiki pita kila pembe ya Zanzibar zungumza na Wazanzibari utapata jibu hilo hilo wapo wenye jazba na machungu yao hao watakwambia bila ya kukuficha kwamba Muungano hawautaki,lakini wengi wape na wachache usiwapuuze wasikilize, hatimae kila Mtu anataka kuheshimiwa utu wake tu! kwani kinachotakiwa na Wazanzibari ni Muungano wa haki,ulio sawa na wa heshima.

Pamoja na maelezo yote haya mimi bado nina amini kwamba Nchi yetu iko kwenye mikono salama ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein na viongozi wenziwe wakuu wa Nchi na wasaidizi wao la umuhimu kwetu Wazanzibari ni kuacha kulalamika sana na kuelewa kwamba tunapaswa kuwasaidia kwa dhati na kuwa wakweli kwa kusimama na ukweli.

Viongozi wa dini,wa jamii na sisi wa siasa tunapaswa kuacha viburi na jazba na kuhubiri na kutenda mema,hata kama yale tutakayoyasema yatachukiza kwa baadhi ,lakini yakiwa yenye manufaa kwa jamii na khatma njema ya Nchi yetu,basi ndio njia sahihi hiyo na ndio njia pekee ya kuondokana na hali tulionayo,siasa ya majibizano za kila jumamosi na jumapili zinaongeza hofu na suita fahamu tu miongoni mwa Wazanzibari ,lugha chafu,matusi,ubaguzi,hasama,udini,uchochezi haujatufikisha popote,wala hatufiki popote,ila tutaendelea kubaki na umaskini wetu na baya zaidi tutajirithisha umaskini wa roho pia.

Haya yatapita kama yalivyopita mengine kwani hufika muda katika maisha ya Nchi na watu wake siasa za kuridhiana, kuvumiliana,kuheshimiana na kujenga umoja na maelewano zikaonekana na wachache kuwa ni za udhaifu mkubwa na wanoa hubiri siasa hizo kuonekana nao ni watu wasio shupavu , lakini historia inatudhihirishia kwamba hali hiyo haidumu na haijapata kudumu popote duniani,inahitaji moyo na dhamira njema kuondokana nayo,Wazanzibari tuko wapi,vipi tanutaka Nchi yetu na Muungano wetu uwe ni suali ambalo letu sote kulitafutia jibu na tukumbuke Wazanzibari Marehemu Bwana Abeid Amani Karume kasema. Angalieni khatma!!!!

MWISHO.

Mwandishi wa makala haya ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki(CCM) Zanzibar

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.