Nianze kwa kusema kwamba uumini wangu kwa Maridhiano na Umoja wa Kitaifa wa Wazanzibari ni asilimia 100+. Lakini imani yangu kwa kiongozi wa serikali ya kwanza yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa iliyotokana na Maridhiano, Dk. Ali Mohammed Shein, sasa ni -0.

Kwa haya yanayotokea sasa Zanzibar, sijioni kuwa na sababu za kutosha za kunifanya nisihoji uwezo halisi wa Rais Shein kama kiongozi. Sisi waandishi wa habari tunakubaliana kitu kimoja kuhusu uwezo wa Rais Shein kama mtaalamu: kwamba ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi – sifa muhimu kwa mwanafunzi katika mfumo wa elimu wa kwetu unaompima mwanafunzi kwa uwezo wake wa kukumbuka masomo aliyofundishwa na mwalimu wake.

Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein
Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein

Kuna hata kauli kwamba, Dk. Shein ana uwezo wa kuhutubia Unguja, Pemba na Dar es Salaam kwa nyakati tafauti, lakini katika mwahala mote humo akasema maneno yale yale bila kubadili hata alama ndogo wala kuangalia karatasi.

Lakini hii si sifa ya uongozi na kama ndiyo haitoshi kuiongoza serikali ya mwanzo ya umoja wa kitaifa, maana uhai wa serikali hiyo unategemea sana moyo wa kujitolea kujenga umoja, uthubutu wa kuulinda umoja huo na utayarifu wa kusimama imara nje ya siasa za makundi au hata za vyama.

Hana. Nahoji kwamba Dk. Shein hana uwezo huo wa kiuongozi. Alichonacho, inavyoonekana ni kinyume chake. Na matokeo yake ndio haya yanayotokea sasa, hata miaka miwili bado tangu ashike madaraka kwa ridhaa na maridhiano. Na hili nalisisitiza, kwamba huyu ni rais wa ridhaa na maridhiano, si wa kura kama vile wanavyojidanganya wengine.

Msingi wa Dk. Shein kuingia madarakani, baada ya yote na juu ya yote, ni Maridhiano yaliyofikiwa na mtangulizi wake, Rais Amani Karume, na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad. Bali ni kwa sababu ya moyo wa Maridhiano hayo, ndipo ile siku ninayoiita “Siku ya Maamuzi ya Bwawani”, Dk. Shein alitangazwa mshindi licha ya yote yanayofahamika kwa uwazi na kwa usiri. Kwa hivyo, jukumu kubwa na la pekee la Rais Shein ni kuulinda msingi huo uliomuweka yeye madarakani, yaani Maridhiano, maana nje ya hayo, u wapi uhalali wa urais wake!?

Nimesema ninataka kusema, na sitachelea kufanya hivyo, maana sisi waandishi wa habari tuna wajibu wetu kwa nchi yetu. Licha ya kuwa kwangu mbali na nyumbani, kimwili, bado jukumu hilo haliniachi na linaniandama niendapo. Na kwa jukumu hilo, naukosoa utendaji kazi wa Dk. Shein kama rais, maana sioni na kuusifia katika wakati ambapo nchi inatoka kubaya ikielekea kubaya zaidi.

Ninachokiona, kwa kukosa kwake uthubutu wa kiuongozi, Dk. Shein amejiwachia awe kama kikombe kitupu ambacho kile kijacho mwanzo ndicho kinachoingia na kujaa na hakitoki mpaka kimwagwe. Ikiwa aliyewahi kuamkia mwanzo Ikulu na kumpa ushauri ni muhafidhina wa Kisonge, basi mawazo ya Kisonge ndiyo yatakayobakia kichwani mwa Rais wetu mpaka hapo yatakapomwagwa na kuwekwa mengine – kama yatawekwa. Na kama hayakuwekwa, basi yatabakia hayo milele, kama inavyoonekana sasa.

Na kwa hili , wala sitaki kujipa kisingizio cha kawaida cha kuwalaumu wasaidizi wake. Kwamba ati ni Makamo wake wa Pili, Balozi Seif Iddi, Katibu wa Baraza la Mapinduzii Abdulhamid Yahya Mzee, au mawaziri Mohammed Aboud na Mwinyihaji Makame! Hapana, si Balozi Iddi wala si Mohammed Aboud, kwa hili ni mwenyewe, Rais Shein.

Huu ni udhaifu wake yeye kama yeye. Na wala sisemi kwa kumsingizia, bali kwa kumnukuu mwenyewe alipowahi kusema kwamba hao wote ni wasaidizi na washauri wake. Mwisho wa siku ni yeye mwenyewe – peke yake – ndiye mwenye jukumu la mwisho, kama kiongozi wa nchi, kuingoza Zanzibar. Ikiwa kuna watu wameamua kuyaua na kuyazika Maridhiano, mbele ya macho yake, basi ni yeye ndiye aliyewapa uwezo na nguvu hizo.

Na kwani unapata hisia gani nyengine, baada ya kuangalia vidio kama hii http://www.youtube.com/watch?v=Pa8dx3jbZn4 ? Utasemaje pia baada ya kusikia kauli yake kwenye Baraza la Iddi akiwakabidhi hundi tupu vikosi vya serikali yake kuyafanya haya yanayoshuhudiwa sasa Zanzibar? Kwamba rais anaonesha urais wake?

Kinachoshuhudiwa Zanzibar hivi sasa ni kile kilichokuwapo kabla ya Maridhiano ya Novemba 2009. Na sipendi sana kutumia kauli ya kwamba ati Rais Shein amezidiwa na kundi kundi la wanaopinga ya Maridhiano, maana kundi hilo lilikuwapo pia wakati Maridhiano hayo yanafikiwa, kwa wingi na nguvu hizi hizi. Lakini kilichotokea ni kwamba mtangulizi wake, aliweka maslahi ya Zanzibar mbele na akalenga kwenye Maridhiano na Umoja wa Kitaifa tu, na si huku wala kule. Kwa sababu alikuwa anajua anakokwenda, aliijua pia njia ya kumfikisha huko.

Ninachokiona ni kuwa Rais Shein hakujuwi anakokwenda na kwa hivyo hajuwi njia ya kumfikisha huko. Badala yake anashika kila njia: ya Kisonge, ya Kachochora, ya Kisiwandui, ya Dodoma, na mwisho wa siku, analiwacha kabisa lengo la waasisi wa Maridhiano na Umoja wa Kitaifa, ambao yeye alipaswa kuwa mlinzi na muongozaji wake mkuu.

Na hili, pasitafutwe visingizio. Ikiwa maisha ya mwanamke na watoto wake hayako salama ndani ya nyumba yake katika ardhi inayoongozwa na unaoitwa utawala wa sheria, ikiwa mchunga ng’ombe hayuko salama kuwapeleka ng’ombe wake malishoni bila ya baba yake kupigiwa simu akachukuwe maiti yake kituo cha polisi, hatuwezi kusema kwamba tunahofia kumuoteza vidole Rais – ambaye ndiye mwenye dhamana ya kuwahakikishia hao ulinzi na usalama wao – ati kwa kuwa tu tutamuudhi na kumvunja moyo asiyatekeleze Maridhiano!

Asitekeleze kipi tena wakati tayari ameshatelekeza kitambo na sasa ameshika nyundo na shoka la kuyavunjavunja!? Hapana, Mheshimiwa Rais, hili ni lako. Hili ni alama ya kutokuwa kwako na uwezo wa kiuongozi ndani ya serikali ya Umoja wa Kitaifa yenye kutokana na Maridhiano!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.