Majeruhi wa Kinuni mwaka 2005. Miaka saba baadaye, bado Zanzibar inaamwaga damu ya yatu wake.

Ukweli ni kwamba kuna viongozi wa juu kwenye serikali ya Zanzibar ambao kwa kushirikiana na Idara ya Usalama wa Taifa ya Tanzania wanahusika moja kwa mja kwenye machafuko ya Zanzibar kuanzia yale ya kwenye uchaguzi mdogo wa Bububu hadi haya sasa. 

Lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba ajenda ya Wazanzibari kudai mamlaka kamili kupitia mchakato wa Katiba Mpya inashindwa kwa kuiua kabisa serikali ya Umoja wa Kitaifa na Maridhiano.

Makubaliano ya pamoja kati ya Dodoma, kundi la vibaraka wao kwenye GNU na CCM Zanzibar na Idara ya Usalama wa Taifa, ni kwamba Maridhiano yaliyozaa GNU ndio adui nambari moja wa mfumo wa Muungano uliopo. Sasa ili kuulinda mfumo huu wa Muungano, ni lazima kumuangamiza adui huyo. Na ndicho kinachofanyika sasa.

Tukio la kutekwa kwa Ustaadh Farid lilikuwa la kweli na lilikuwa ni sehemu ya programu hiyo kubwa ambayo inagharimu mamilioni ya fedha za walipa kodi wa Tanzania nzima na si wa Zanzibar peke yake.

Kiasi cha mwezi mzima kabla ya Ustaadh Farid kutekwa, kijana mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa anayefanya kazi Zanzibar, alijenga mahusiano makubwa na viongozi wa juu wa Uamsho, hasa Sheikh Farid.

Kijana huyu, ambaye hakujificha kwamba ni mtu wa Usalama wa Taifa, alijitokeza kama sehemu ya kundi la watu waliomo kwenye taasisi za dola na ambao wanaunga mkono Ajenda ya Zanzibar. Kwa maslahi ya ajenda hiyo, na kwa maslahi ya Zanzibar, bahati mbaya viongozi wa Uamsho walimuamini. Ni yeye ndiye aliyekuwa mtu wa mwanzo kabisa kumpigia simu Sheikh Msellem saa 2:00 usiku wa siku ya kutekwa kwa Imamu Farid, kumjuulisha kwamba Usalama wa Taifa wamemkamata Sheikh Farid.

Ndani ya siku tatu za suintofahamu hiyo, ni yeye aliyekuwa akiwashinikiza viongozi wa Uamsho na vijana kwamba ni lazima shinikizo kubwa lifanyike kama kweli wanataka kiongozi wao aachiwe akiwa salama.

Kwa hakika, siku ya pili yake aliwasiliana na kukutana na Sheikh Msellem, na kumuambia kwamba alikuwa tayari kumpeleka aliko Sheikh Farid. Baada ya kuingia kwenye gari, hakumpeleka kwa Sheikh Farid, bali alimwambia kwamba wazungumze naye kwa simu kwanza, akiwa tayari ameshaipiga simu hiyo, kwa alivyosema.

Kwenye simu, ni kweli Sheikh Msellem alisikia sauti ya Sheikh Farid ikimuambia kwamba ametekwa na wanamtesa, na kwamba kama hawakujikaza basi wanaweza hata kumuua. Alipotaka kuuliza mengi zaidi, Sheikh Msellem hakuweza maana ile simu ilikatwa.

Kumbe kilichokuwa kimefanyika, ni kuwa Sheikh Msellem alisikilizishwa sauti ya kurikodi ya Sheikh Farid na hakuwa anazungumza naye moja kwa moja. Ilikuwa ni baadaye sana, viongozi wa Uamsho walipokuja kung’amua hayo.

Ndani ya kipindi hicho cha kupotea kwa Ustaadh Farid, viongozi wa serikali ya Zanzibar wanaohusika na programu yao, waliyatoa makundi ya vijana wao kuchoma maskani za Kisonge, kuharibu mali, kuiba, kupiga, kujeruhi, na hata kuua.

Katika purukushani hizo, vijana hao walikuwa wakipigana na kuumizana wenyewe kwa wenyewe. Miongoni mwao ni askari aliyepigwa risasi na kuuawa na wenzake, lakini huyo hatajwi kabisa na vyombo vya habari, badala yake anatajwa askari aliyeuawa Bububu kwa kukatwa mapanga, na ambaye huenda kabisa asiwe na uhusiano na matukio haya.

Miongoni mwa vijana walioumizwa wako waliojeruhiwa vibaya na ambao hadi sasa wamelazwa kwenye hospitali ya jeshi ya Bububu, lakini taarifa zao zimewekwa siri sana.

Kilichotokea, ikiwa ni sehemu ya programu hiyo kubwa, ni kwa Idara ya Habari Maelezo ya SMZ kutoa agizo kwa vyombo vyote vya ndani vya habari kutokutangaza kabisa matukio ya sasa, tangu kukamatwa kwa Sheikh Farid.

Kwa hakika, hata katika kamatakamata ya polisi, nao pia wamewakamata vijana kadhaa wa makundi hayo lakini huwa wanawaachia kwa amri ya Kamishna Mussa Ali Mussa, Mkuu wa Jeshi la Polisi la Zanzibar, ambaye ni sehemu ya programu hiyo ya kuivunja GNU.

Sheikh Farid aliachiliwa baada ya uingiliaji kati viongozi wawili wa juu GNU, kwa kuanzia na Makamo wa Kwanza wa Rais Seif Sharif ambaye baada ya kufahamishwa undani wa mkasa mzima alimwendea Rais Ali Shein, na kumuambia maneno yafuatayo: “Mhe. Rais ninasikitika sana kwamba sisi wenyewe ndio tunaohusika na haya yanayotokezea hivi sasa. Watu wetu wanajua wapi alipo Sheikh Farid. Wanafanya hivi kukuharibia wewe uonekane kwamba huna uwezo wa kuongoza na kwamba unaiwachia nchi iingie kwenye machafuko.

Lakini zaidi wanafanya hivi ili kuivunja GNU, maana watatufanya sisi tujihisi kwamba ni sehemu ya uozo huo nasi hatutakubali. Sasa waambie watu wako ambao wako chini ya ofisi yako (akamtaja kwa jina yule kijana wa Idara ya Usalama wa Taifa) wakuoneshe walipomueka Farid.” Usiku wake, saa 2:00 Sheikh Farid akaachiliwa.

Lakini hadi kuachiliwa kwa Sheikh Farid, tayari sehemu ya lengo moja kwenye mkakati wao ilishafanikiwa: nayo ni kutengeneza mazingira ya fujo na kuhalalisha matumizi ya nguvu, ghasia na uvunjwaji wa haki za binaadamu kama yanayoendelea sasa.

Pia kwa sababu ya kuficha uovu na asili ya mkasa mzima, wamemkamata Sheikh Farid na viongozi wa Uamsho ambao wanaujua ukweli wote wa mkasa huu, na sasa wamewaweka ndani na kuwafungulia mashitaka kadhaa, ili wasiwe nje wakaweza kuueleza umma kile hasa kilichotokea.

Kwa upande mwengine, wanavilisha vyombo vya habari vya Tanzania Bara na vile vya Zanzibar vinavyopinga Maridhiano na Umoja wa Kitaifa, taarifa za uongo kuhusu viongozi hao wa Uamsho na wafuasi wao. Picha inayojengwa ni kwamba Uamsho ni magaidi na hivyo wapate kuhalalisha kuongeza wanajeshi na matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola dhidi ya raia wanaodai mfumo wa Muungano wa Mkataba.

Hivi sasa operesheni ya kijeshi imeimarishwa kisiwani Unguja, hasa kwenye mkoa wa Mjini Magharibi, ambako Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba Mpya inakuja hivi karibuni. Wananchi wanatishwa na wanatiwa hofu na mazingira yanajengwa ya kuzuia maoni ya wananchi hao mbele ya Tume, maana hadi sasa wengi waliokwishatoa maoni yao, wameshasema wazi wanataka mabadiliko ya msingi kwenye Muungano.

Matokeo wanayoyatarajia ni aidha kwa wananchi wanaopigwa na makundi waliyoyatayarisha na vikosi vya SMZ kujibu mapigo na hivyo kuiingiza nchi moja kwa moja kwenye fujo za kudumu, au kwa wajumbe wa CUF kwenye GNU kuja juu na kujitoa kwa kupinga dhuluma hii. Lolote kati ya mawili hayo, mwisho wake ni kuyavunja maridhiano na umoja wa kitaifa na hivyo kuiua na kuizika kabisa Ajenda ya Zanzibar.

Kwa upande wa wananchi, programu hiyo inalenga kuwavunja moyo wao kwa serikali ya GNU, hasa kwa wafuasi wa CUF mbele ya Makamo wa Kwanza Seif Sharif, ambaye wanajengewa picha ya kwamba amewasaliti na haguswi na mateso wanayoyapata.

Mwenyewe Maalim Seif analijua na analifuatilia kwa karibu kila linalotokea na anamshauri Rais Shein kama ulivyo wajibu wake kama makamo wa kwanza wa Rais. Amechukua na anaendelea kuchukua kila jitihada za kumsaidia Rais Shein na kuilinda GNU isianguke, maana ikianguka ndio hatima ya Zanzibar imekwenda pamoja nayo.

Katika ghasia zinazoendelea sasa kwenye jimbo la Bububu, amemfahamisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayehusika na vikosi vya SMZ, Dkt. Mwinyihaji Makame, na amemueleza wazi kwamba kinachofanyika ni uvunjaji wa haki za binaadamu, mateso na udhalilishaji, ambao mwisho wake ni kwa wananchi kuamua kujilinda na machafuko yakisambaa, hakuna hata mmoja atakayenusurika, si Dkt. Mwinyihaji wala si yeye Maalim Seif.

Laiti Rais Ali Mohammed Shein ana dhamira, nia na uwezo wa kuinusuru ndiye mwenye nafasi ya juu kufanya hivyo. Wapinzani wa Maridhiano na Umoja wa Kitaifa walikuwapo pia wakati wa muasisi wake, Rais Amani Karume, lakini alikuwa na uthubutu wa kuwadhibiti.

Rais Shein kwa upande ake anaonekana kuelemewa vibaya na kundi la wapinzani wa Maridhiano na Umoja wa Kitaifa waliomo kwenye serikali yake, chama chake na vyombo vyake vya usalama. Kundi hilo ambalo linatumikia ajenda ya Tanganyika dhidi ya Zanzibar, kama ilivyoonekana wazi, liko tayari hata kukanyaga maiti za Wazanzibari alimradi tu lifikie kwenye lengo lake.

Kwa hivyo, inabakia kuwa juu ya Wazanzibari ambao sasa wanateseka chini ya mikono ya kundi hilo aidha kulipa nafasi ya kumaliza kazi liliyoianza ya kuisimamisha ajenda ya Tanganyika, au kuyapa nafasi Maridhiano na Umoja wa Kitaifa nayo kumaliza kazi yaliyoianza ya Ajenda ya Zanzibar.

Zanzibar imeanza tena kuzama. Inahitaji kuokolewa hivi sasa.

Makala hii imechukuliwa kutoka ukurasa wa Facebook kwa akaunti inayojitambulisha kama Ukweli Zanzibar

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.