Siku Zanzibar ilipopetewa kumvini.

Na Gwandumi Gwappo Atufwene Mwakatobe
Septemba 15, 2012, Mwakaleli (Kandete)

Awali ya yote, kama alivyowahi kusema Mwalimu Nyerere kuwa ukimwambia mtu mzima ukweli unamheshimu, lakini ukimwambia uongo unamdharau. Ni kuwadharau wananchi kuendelea kuwaambia kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina serikali mbili.

Kusema ukweli tuna serikali za aina nne hapa nchini – na si mbili kama ambavyo wengi wameaminishwa. Serikali hizo ni:

1. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambayo imekuwa wazi sana kiutendaji na kimuundo
2. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT/URT) ambayo ilianza na masuala 11 wakati wa kuanza muungano mnamo Aprili 26, 1964
3. Serikali ya Tanganyika ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikijificha kwenye masuala ya muungano au kama ambavyo wengine kimakosa wamebuni jina la Tanzania Bara
4. Serikali za mitaa ambazo zinatenda kazi katika ngazi ya vitongozi, mitaa, vijiji, wilaya, miji, manispaa na majiji.

Na ieleweke kuwa Tanganyika na Zanzibar hazikufuta hadhi ya kuwa nchi isipokuwa tu katika masuala ambayo ni ya muungano, na kwa miezi kadhaa baada ya kuungana, nchi ya muungano iliendelea kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hadi pale ambapo mshindi wa kutunga jina moja la muungano alipounganisha TAN kutoka kwenye herufi tatu za kwanza za Tanganyika na ZAN kutoka kwenye herufi tatu za kwanza za Zanzibar, na kumalizia vifupisho vya majina yake mawili vya I na A na kupata TANZANIA. Unapotaja TANZANIA unataja mambo ambayo ni ya muungano, yanayobaki yanakuwa ya nchi ya Zanzibar upande mmoja wa muungano na nchi ya Tanganyika kwa upande mwingine.

Hadi leo hakuna mahali popote ambapo jina Tanganyika lilifutwa na kuwekwa jina lingine. Na hadi leo Hati ya Muungano ndio mkataba pekee ulio hai kuhusiana na muungano wa nchi mbili. Wanaoita Tanganyika kuwa ni Tanzania Bara wanakosea sana kwa kuwa hatujawahi kubadili jina la Tanganyika kuwa Tanzania Bara. Hata tungekubaliana kisheria bado tungekosea kuiita Tanganyika Tanzania Bara kwa kuwa pwani yote (Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam na Tanga) haiko bara! Aidha visiwa vya Mafia, Songosongo, Koma, Kwale, Ukerewe na kwignineko haviko bara!

Nisisitize kuwa, hali halisi na muundo halisi wa kiutendaji uliopo sasa tangu Aprili 26, 1964 ni wa serikali tatu: Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Tanganyika ambayo kimakosa inajificha kwa kutumia jina la Tanzania au Tanzania Bara. Pia kuna watu walijitungia kienyeji kwa kubdadili jina la Zanzibar na kuita Tanzania Visiwani bila kujua kuwa hata visiwa vya Ukerewe na Mafia ni Tanzania Visiwani lakini haviko Zanzibar! Na waliendelea kutapatapa tena kwa kuiita Zanzibar Tanzania Zanzibar wakati ni Zanzibar na ndiyo jina lililomo kwenye hati ya muungano. Nashukuru kwamba wazanzibar wameendelea kuiita nchi yao kwa jina la Zanzibar.

Nisisitize kuwa mambo yote yasiyo ya muungano yanashughulikiwa au yanasimamiwa na Zanzibar au Tanganyika. Kusema masuala yasiyo ya muungano yanashughulikiwa na Tanzania kwa upande wa Tangayika ni makosa kwa kuwa si ya muungano, maana Tanzania ni kwa ajili ya masuala ya muungano tu! Wenzetu Zanzibar wanakwenda sawia na unavyosema mkataba almaarufu Hati ya Muungano na wako wazi sana katika kufuata mkataba huo na kuulinda.

Hadi leo hii tuna sikukuu za aina tatu: uhuru wa Tangnyika wa Desemba 9, mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12 na muungano wa Aprili 26. Kimahesabu huwezi kuunganisha vitu viwili ukabakiwa na vitu viwili. Utakuwa na kimoja au zaidi ya viwili! Huwezi kuwaoza mwanamke na mwanaume ukawa na ndoa mbili. Itakuwa ndoa moja tu. Ukiunganisha maumbo mawili yaliyounganika kwa sehemu tu unapata maumbo matatu: kiunganiko (intersection set) na sehemu mbili ambazo hazijaunganika. Kuendelea kusema uongo kwa kudai kuwa Tanzania kuna serikali mbili wakati hali halisi kiutendaji ni serikali tatu ni kuwadharau wananchi.

Tanganyika ilikuwa na umri wa miaka miwili na miezi mitano tu ilipoungana na Zanzibar kwa mambo 11 tu (sasa yako 22), tangu ilipopata uhuru Desemba 9, 1961; na Zanzibar ilikuwa na umri wa miezi minne tu na siku kadhaa tangu ilipopata uhuru Desemba 10, 1963, na ilikuwa na umri wa miezi mitatu tu tangu ilipofanya mapinduzi Januari 12, 1964, ambayo ndiyo yanayoenziwa. Leo hii hatuwezi kujigamba kwamba Zanzibar imefaidika na muungano kwa kuwa haikuishi muda mrefu nje ya muungano (miezi mitatu tu) na kuzitumia vizuri fursa za kitaifa na kimataifa. Na Tanganyika pia haikuishi muda mrefu nje ya muungano (miaka miwili tu na miezi mitano). Tanganyika imekuwa ikigharamia mambo mengi ikiwa pamoja na kuwaruhusu Wazanzibar washiriki bungeni kwa mambo yasiyo ya muungano wakati Watanganyika hawashiriki kabisa kwa upande wa Zanzibar.

Nihitimishe kwa kusema kuwa suluhisho muafaka na thabiti la kudumisha uhusiano mwema na Wazanzibar ni kuwaachia kabisa wawe taifa huru na dola kamili kitaifa na kimataifa. Tanganyika nayo ibakie kamili ili tuondokane kwa amani na kero nyingi za muungano. Tubakie majirani wema kama ilivyo kwa Zambia, Msumbiji, Rwanda, Kenya na kwingineko. Kuwa na mahusiano mema na jirani ni jambo la msingi na si lazima muunganishe nchi. Kuna nchi nyingi tunahusiana nazo vizuri sana na kwa ukaribu japo haziko jirani. Undugu ni mahusiano mema si kuunganisha nchi.

Zanzibar imekosa fursa nyingi za kimataifa kwasababu ya kubanwa na kufinywa na muungano. Kwao muungano ni jinamizi! Si vema kuendelea kuwabana watu ambao ni ndugu zetu kama ilivyo kwa nchi zote jirani. Kuna faida nyingi kwa Tanganyika na Zanzibar kuwa nje ya muungano. Hatuwezi kuendelea na serikali tatu na mifumo tata inayotugharimu fedha nyingi na kero zisizoisha. Mungu ibariki Zanzibar, Mungu ibariki Tanganyika, na bariki uhusiano wetu mzuri na wa kijadi kati ya Zanzibar na Tanganyika na nchi zingine jirani na zilizo mbali.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.