Angalia vidio hii, halafu soma tamko lifuatalo ambalo lilisambazwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook na Vijana wa Umoja wa Kitaifa wa Zanzibar kuwaonya viongozi na watu wanaozuia uhuru wa maoni kuelekea Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Halafu unganisha na matukio ya uvunjifu wa amani, vitendo vya vyombo vya dola visiwani Zanzibar na itafakari hatima ya Zanzibar. Maswali ya kujiuliza ni ikiwa je, haya yanayoendelea sasa Zanzibar ni kweli hayana mkono wa waliotoa hotuba hizi kali kwenye kampeni za uchaguzi mkono wa Bububu? Je, ni kweli kwamba Zanzibar inasukumwa kurudi ilikotoka? Na nani?

“Vijana wa Umoja wa Kitaifa Zanzibar tumeshtushwa sana kufuatia matamshi/kauli na misimamo ya baadhi ya viongozi na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yenye shabaha ya kutumia vitisho na mabavu katika kuzizima hoja za baadhi ya viongozi, wanachama na wafuasi wake wenye mawazo mbadala/tofauti.

“Hapa tunawakusudia viongozi wa CCM wa Wilaya ya Mjini na Afisi Kuu, Kisiwandui pamoja na baadhi ya viongozi wastaafu wa CCM ambao wanawatisha na kuwashinikiza viongozi katika chama chao hususan Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Wananchi wa Zanzibar waliochaguliwa na wananchi wa Zanzibar wakiwa na wajibu wa kuwatetea wananchi wa Zanzibar kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wakilindwa na kinga kwa mujibu na kanuni za Baraza na Sheria za nchi.

“Hao wenye kutoa vitisho na kuweka shinikizo wajue kuwa vitendo vyao hivyo ni kupora uhuru wa wananchi na kuondosha uhalali wa zoezi zima la marekebisho ya katiba.

“Vitendo vyao hivyo ni sawa na kuwapangia wananchi nini cha kusema na vitendo kama hivyo ni uvunjifu wa katiba na sharia za nchi na ni uporaji wa haki za msingi kabisa za wananchi wote na ni fedheha na aibu kubwa kwa CCM.

“Ifahamike wazi kuwa kupatikana kwa aina ya mfumo wa muungano tunaoutaka utapatikana pale tu ambapo wananchi wote bila ya kujali vyama vyao watakuwa na uhuru usio na masharti ili waweze kutoa maoni yao vinginevyo zoezi hili lote litapoteza maana na uhalali wake na hivyo kuwa batili.

“Katika hali kama hii tunamuomba Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein waingilie kati ili kulinda uhuru wa wanachama na sisi wananchi kwa ujumla wetu. Halikadhalika tunamuomba Mwenyekiti wa Tume ya Pamoja ya Marekebisho ya Katiba, Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba pamoja na Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kutoa tamko juu ya kauli hizi za kushtusha za baadhi ya viongozi hawa wa CCM ili wananchi turidhike juu ya uhuru wetu na uhalali wetu wa kutoa maoni bila ya shinikizo la aina yoyote kutoka chama chochote.

“Kauli na misimamo hiyo inaonekana sio tu kwenda kinyume na Azimio la Haki za Binaadamu zinazodhamini uhuru na uwezo wa kila raia kuwa na mawazo na maamuzi tofauti. Misimamo na matamshi hayo yanapingana hata na kauli ya Rais Jakaya Kikwete, Rais Ali Mohammed Shein na Jaji Warioba ambao kwa pamoja walisema wazi kuwa wananchi wako huru kuwa na maoni tofauti juu ya mchakato wa katiba na wawe huru katika kuyatoa mawazo yao.

“Aidha, Rais Kikwete alisema na tunamnukuu: “Kwa upande wa mchakato wa kupata katiba mpya, nawasihi Watanzania tujiandae kwa maoni ya kutoa. Tutofautiane bila kupigana”.

“Hata anayeitwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kusema katika hotuba aliyoitoa kwenye mkutano wa Uganda People’s Congress (UPC), tarehe 7 Juni, 1968: “Chama kina uwezo kuiambia Serikali nini matilaba ya watu, na kwamba ni muhimu kuweko wanachama ndani ya chama wanaoweza kuhakikisha kwamba Serikali na watu wanashirikiana kutekeleza matilaba ya watu”.

“Tunatanabahisha kuwa tutofautiane katika fikra bila ya kubezana, kutishana wala kupigana. Aidha, tunatanabahisha kuwa kauli kama hizi zilizoanza kutolewa zinazobeba agenda ya vitisho na kuiviza demokrasia hazitavumiliwa. Ni busara kusoma alama za nyakati.

“Nchi hizi mbili za Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimetokana na asili ya utawala wa chama kimoja cha siasa baada ya mapinduzi ya Zanzibar na uhuru wa Tanganyika, na hatimaye kuwepo kwa chama kimoja tu kwa nchi zote mbili.

“Siasa ya vyama vingi imeanza katika uchaguzi mkuu wa 1995, kiasi cha miaka kumi na saba iliyopita, tofauti na utawala wa chama kimoja wa miaka zaidi ya thelathini.

“Kwa miaka hiyo thelathini na kitu, hakukuwa na tafauti kubwa baina ya Chama na Serikali. Kwa mfano, Mkuu wa Mkoa alikuwa Katibu wa Mkoa wa Chama, viongozi wa Chama walikuwa na hadhi ya viongozi wa Serikali kama vile kusafiria pasi za kibalozi. Katika kila Wizara, Idara na Mashirika, kulikuwa na ofisi za Chama cha Mapinduzi, na Mwenyekiti wake, na bendera ya chama ndio ilokuwa ikipepea.

“Hii inaonesha wazi tutokapo na jinsi mfumo wa fikra za watu (mindsets) ulivyojengeka.

Kutokana na hali hii sera za Chama na Serikali hazikuweza kuwa na tafauti yoyote. Sera zote za chama ndio zilikuwa sera za serikali. Kwa maana hiyo sera ya kuwa na Muungano wa Serikali mbili iliyopo ndani ya Katiba ya Muungano ndiyo ya Chama tawala cha wakati huo na ndio maana bado kuna baadhi ya viongozi (wahafidhina) wanaolalamika leo juu ya haya mabadiliko tunayoyatarajia, na ndio maana vilevile tunashuhudia wakikaripia na hata kupinga juu ya mabadiliko ya sera hizo.

“Wakati umebadilika na nchi zetu zina vyama vingi vya siasa, vyenye sera zao na wanachama wao ambao wote ni wananchi wenye haki sawa juu ya maamuzi mazito ya nchi kama katiba zinavyoeleza. Zaidi ya Chama tawala, hakuna hata chama kimoja chenye sera yake ya muundo wa nchi, kwa sababu vinafahamu kwamba sera hii haiwezi kuwa ukiritimba wa chama kimoja, bali ni ridhaa ya wananchi wote, hata wale ambao siyo wanachama au wafuasi wa chama chochote cha siasa.

“Kwa hivyo huu utaratibu wa kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi ni wa kupongezwa. Hata hivyo, indhari ichukuliwe ya kuhakikisha kwamba ukweli na uadilifu unatawala katika zoezi hili, na kwamba kila mwananchi apewe fursa ya kutoa maoni huru bila ya shinikizo la kuimba nyimbo ya sera za Chama chake. Hii itakuwa kinyume kabisa na wanavyofanya baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutaka kuwatisha na kuwanyanyapaa baadhi ya wanachama wake wenye fikra tofauti zinazokwenda kwa mujibu wa hali ya siasa zilivyo hivi leo.

“Huu ni wakati wa wananchi kupingana bila ya kupigana na hii ndio demokrasia itakayotuletea amani na usalama. Hapa elimu ya uraia ndipo inapohitajika.

Tunasisitiza kuwa matokeo ya zoezi hili yaheshimiwe na wote. Tunajua kwamba Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni kiongozi mwandamizi wa Chama chake. Tunamuomba kwamba asiyumbishwe na sera za Chama chake katika zoezi hili. Tume ni suala linalojitegemea na maslahi ya nchi na watu wake ni makubwa kuliko sera za vyama. Huu ni wakati wa kusonga mbele si wakati tena wa kutazama nyuma. Wakati na mawimbi hayamsubiri mtu.

Tufanye kazi katika maadili ya shabaha yanayoheshimu mawazo, maoni na maamuzi ya wananchi. Tuna wajibu wa kusimama juu ya ukweli kama tunavyouona bila ya kujali misingi na mirengo ya vyama. Sote kwa ujumla wetu kuanzia vyama, Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Serikali zote mbili ni watumishi wa watu. Na watumishi hawana haki wala mamlaka wala nguvu zinazowazidi mabwana zao ambao ni wananchi kama Katiba zote mbili zinavyolidhamini hilo. Tunawajibika katika hili kutoa huduma ya kizalendo na kwa sababu hiyo itakuwa huduma ya kweli na isiyosimamia misingi ya vyama.

Sisi Vijana wa Umoja wa Kitaifa ni waumini wenye kuheshimu uhuru wa mawazo ya kila mwananchi; lakini pia tunabeba kauli mbiu (motto) isemayo: “Maslahi ya wananchi ni makubwa zaidi kuliko yale ya vyama vya siasa.” Historia itakuja kutuhukumu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.