Waraka huu ni kuhusu nyenzo na vigezo vya kuipata Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyo na mamlaka kamili ndani na nje na baadae kufuatiwa na Mashirikiano/Muungano wa Mkataba. Shabaha ni kubainisha njia na vipimo vya kufikia hapo. Kwa kujua na kutumia nyenzo sahihi inatarajiwa kupatikana sio tu Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Mashirikiano/Muungano wa Mkataba; bali pia faida zake.

Aidha, kwa kutumia vigezo, inategemewa kwamba itajulikana nani mzalendo na nani msaliti na kwa kaisi gani. Uzalendo ni imani na amali (vitendo).

Hadi sasa juhudi zimekuwa zikielekezwa zaidi katika kutafuta na kuorodhesha mambo ambayo Wazanzibari tunapaswa kuamini na kutenda.

Imekubaliwa na wengi kwamba Wazanzibari wanapaswa kuamini juu ya haja ya kuirudisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyo na mamlaka, uwezo na nguvu kamili kitaifa na kimataifa na baadae kuwe na Mkataba na kila nchi jirani utakaotokana na ridhaa ya wananchi wa nchi husika kwa maslahi sawa ya pamoja.

Kwa baadhi, hizi ni nyenzo tu za cause hii; kwa wengine haya ndio malengo makuu. Kama ambavyo Maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa baadhi ndio lengo; kwa wengine ni nyenzo za kutusaidia kufikia lengo. Maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ulikuwa mwanzo tu.

Lakini bado juhudi hazijaelekezwa vya kutosha katika kufafanua nyenzo za kutusaidia kuirudisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na hayo Mashirikiano/Muungano wa Mkataba.

Kama mambo hayo mawili yameeleweka, njia za kuyafikia bado hazijaeleweka. Kama imekubaliwa kuwa na Zanzibar yenye uwezo wa kujiamulia mambo yake wenyewe ni jambo la kuaminiwa; bado namna ya kuamini hivyo haijaeleweka.

Kadhaalika juhudi hazijaelekezwa vya kutosha katika kubainisha vigezo vya imani hiyo na matendo yanayoakisi mambo hayo. Kutokana na hali hii imekuwa si rahisi kumtambua mwenye uzalendo na aliemsaliti.

Hata akitambuliwa, ni vigumu kuweza kujuwa kiwango chake cha uzalendo na usaliti. Aidha, ukosefu wa vigezo umepelekea tofauti za msingi baina ya wazalendo na wasaliti kutoweka.

Bila ya nyenzo na vigezo malengo hayapatikani. Vivyo hivyo uzalendo wa kweli haupatikani bila ya kujua na kutumia nyenzo na vigezo vyake.

Kuna dalili za kuonesha kuwa Umma wa Kizanzibari una ukosefu au upungufu wa kujua nyenzo za kufikia malengo. Ukosefu wa malengo baada ya kujaribu unaweza tu kutokana na ukosefu wa nyenzo na vigezo sahihi.

Pamoja na uzuri na uhalali wa shabaha yetu hiyo ya kuirudisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyo na mamlaka kamili kitaifa na kimataifa na kufuatiwa na Mashirikiano/Muungano wa Kimkataba – bado tunakosa nyenzo muhimu mno ya kutusaidia ktika kuyafikia mambo hayo – nayo ni umoja, mashirikiano na kuaminiana baina yetu.

Kwa kweli kuendelea kwa mtindo huu uliojitokeza wa kila kundi – kuanzia yale ya kisiasa na yale ya kidini kunyoosheana vidole – maana yake ni kwamba ‘tunawakabidhi watu wengine ambao ni maadui zetu mamlaka ya kufanya uamuzi muhimu juu ya mambo ya nchi yetu’.

Vyama vya Siasa pamoja na Taasisi za Kidini kwa pamoja vina wajibu kuwasaidia Wazanzibari kuyagomea maisha ya kuamuliwa mambo yao na watu wa nje. Lazima Vyama na Taasisi ziungane kusaidia kufanya hivyo kwa haraka iwezekanavyo. Vyama vya Siasa na Tasisi za Kidini zina wajibu kushirikiana kwa vitendo katika kupanga, kuanzisha, na kuendeleza mabadiliko yaliyo ya lazima kwa Wazanzibari, na ambayo lazima yatakuja, tutake tusitake, insha’Allah. Vyama na Taasisi hizo zinalazimika kuheshimiana na kila upande kutambua mchango wa mwengine katika harakati hizi ndipo tu zitakapoweza kutarajia kupunguza chuki na kudumisha imani yake kwa Wazanzibari wote.

Mapenzi ya Wazanzibari kwa Vyama vya Siasa na Taasisi za Kidini surely yataonekana katika vitendo vya makundi haya katika kupinga maovu na kuleta mema. Makundi mawili haya ni lazima yashirikiane na Wazanzibari. Makundi mawili haya yanapaswa kuwasaidia Wazanzibari kuishi pamoja na kufanya kazi ya harakati hizi kwa pamoja kwa faida ya wote.

Kazi ya makundi mawili haya ni ya thamani kubwa mno; lakini inatubidi tukubali kuwa wao ni wachache sana mbele ya Wazanzibari. Wazanzibari ni zaidi ya CCM, ni zaidi ya CUF na ni zaidi ya UAMSHO. Naomba ieleweke hivyo.

Kadhaalika, lazima makundi haya yatambue kwamba watu wengine, wasiokuwa UAMSHO, wasio CUF na wasio CCM, pia watakuwa wanajitahidi katika kuhakikisha mipango ya siasa na uchumi wa Zanzibar inafanywa na nchi ya Zanzibar na si vyenginevyo na kwamba uamuzi huo ufanywe na Wazanzibari wenyewe.

Kwa hiyo ni Wazanzibari watakaoamua shabaha na mustakbal wa nchi yao. Vile vile, makundi haya yanawajibu kutambua kuwa wako watu nje ya makundi hayo wanaotaka kuona Zanzibar inajitawala na inajifungua kabisa kutokana na pingu za nchi za nje.

Kusema hivyo maana yake nn? Maana yake ni kuwa kuyatenda hayo si haki ya makundi hayo peke yao. Hayana haja haya kulihofia hilo.

Muhimu zaidi na lililo busara ni kutambua kuwa jambo jema haliwi ovu kwa sababu kundi moja limesema ni jema; wala jambo ovu haliwi jema kwa sababu tu kundi jengine linaliunga mkono.

Wazanzibari tutoke kwenye mivutano iliyotugharimu kila kilicho chetu. Tuungane baina ya makundi yote kwa kigezo cha – Uzanzibari utuunganishe katika kuirudisha Jamhuri ya watu wa Zanzibar yenye uwezo wa kujiamulia mambo yake (self determination), itakayoweza kuingia mikataba na ushirikiano na nchi nyengine, itakayokuwa na balozi zake, itakayokuwa na utaratibu wake wa VISA, itakayokuwa na sarafu yake, itakayokuwa na kiti chake UN, AU, EA na kadhaalika.

Tusameheane na kusafiana nia Wazanzibari. Huu si wakati wa kulumbana na kutoaminiana baina yetu. Huu ni wakati wa kusameheana, kuungana, kushauriana na kuaminiana katika kutimiza shabaha ya kuirudishia Zanzibar yetu heshima na thamani yake katika uso wa dunia.

Mwenyezi Mungu (SW) anaeleza katika Qur’an: “Na lau Muhammad ungelikuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangelikukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo”.

Kadhaalika, anasema tena kwenye sura nyengine kuwa: “ Mema na maovu hayalingani. Ondoa ovu kwa kufanya lililo jema zaidi – hapo yule ambaye baina yako na yeye pana uadui – atakuja kuwa mwenzio wa kukunusuru mwenye moyo safi. Lakini hawaruzukiwi tabia hii ila wanao subiri; na hawaruzukiwi tabia hii ila wenye bahati kubwa”.

Tuichukue falsafa hii ili ituongoze katika kufanikisha shabaha yetu kwa umoja na kushirikiana kwetu. Licha ya udogo wetu, tunaweza kwa umoja wetu Wazanzibari kuyafikia mengi ambayo hatukuweza kuyafikia kwa kugawanyika kwetu. Ushirikiano ni msingi wa ukombozi.

Zanzibar yenye mamlaka kamili hayawezekani bila ya umoja wa Wazanzibari. Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Kwanza!

Khalid Gwiji,
Zanzibar

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.