Na Ahmed Raajab

Mmoja kati ya Wazanzibari waliowahi kuwa mawaziri katika wizara za Tanzania Bara. Dk. Haji Mponda hadi hivi karibuni alikuwa waziri wa afya na ustawi wa jamii wa Tanzania Bara, wizara ambayo si ya Muungano. Mzanzibari kuongoza wizara isiyo ya Muungano ni sawa?

MOJA ya sifa za mfumo wa utawala wa kidemokrasia ni kuwako kwa mkusanyiko wa sheria za maadili au taratibu za maadili . Taratibu hizo ni muhimu kwa kuimarisha utawala bora kwa vile aghalabu huwa zinawafunga viongozi wawe wanawajibika kwa wananchi kwa hatua wanazochukua na kwa matendo wayatendao.

Viongozi wote wa umma, iwe waliochaguliwa na wananchi au hata wale wasiochaguliwa, lazima wawe wanawajibika. Wao, kwa kweli, ni watumishi wa umma ingawa huwa na tabia ya kujifanya kuwa ndio mabwana wa umma. Ikiwa kipengele hicho cha kuwajibika hakimo katika taratibu za uongozi basi utawala bora huwa muhali kupatikana.

Huu ni mtihani mkubwa unaowakabili viongozi wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Si wapumbavu wa kutojua kwamba lazima wawajibike lakini hujitia hamnazo wakijifanya hawajui wawajibike kwa nani.

Ni mtihani mkubwa pia kwa viongozi hao kwa sababu Jamhuri hii ni dola moja kamili yenye serikali mbili na nchi mbili kwa vile Zanzibar nayo pia ina taasisi zote za utawala. Ina serikali yake, rais wake, bunge lake (Baraza la Wawakilishi), bendera yake, wimbo wake wa taifa na pia ina mipaka yake na maji yake ya taifa katika Bahari Kuu ya Hindi. Sifa zote hizo za utaifa inazo na zimebainishwa vilivyo ndani ya Katiba ya Zanzibar.

Tanganyika, kwa upande wake, inaendeshwa na Serikali ya Muungano. Lakini kwa mujibu wa sheria za Serikali ya Muungano uwakilishi wa umma ndani ya serikali hiyo na ndani ya Bunge la Tanzania lazima uwe na sura ya Kimuungano. Hilo si jambo baya kimsingi. Hata vyama vya siasa navyo kwa mujibu wa sheria lazima viwe na wawakilishi wa Kitanganyika na wa Kizanzibari.

Tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uundwe mwaka 1964, kuna idadi ya Wazanzibari ‘waliohamishwa’ kwenda kufanya kazi katika Serikali ya Muungano na baada ya vyama vya TANU na ASP kuungana na kuunda CCM, kilichokuwa chama pekee halali cha kisiasa, kuna Wazanzibari waliohamishwa na kupelekwa Bara kwenda kukitumika chama hicho.

Hayo kama nilivyogusia yalikuwa katika enzi ya mfumo wa chama kimoja. Kwa vile chama hicho kilipevuka kwa umri na kwa vile kilikuwa na hadhi ya kuhodhi pekee madaraka ya kisiasa katika enzi hiyo ya udikteta wa chama hicho, Wazanzibari wengi walipelekwa kufanya kazi katika Makao Makuu ya CCM huko Dodoma.

Vilevile kuna Wazanzibari waliopelekwa Bara kushika nyadhifa mbalimbali na kufanya kazi katika Serikali ya Muungano, ndani ya nchi na pia nje ya nchi katika balozi za Tanzania na katika taasisi na jumuiya za kimataifa wakiiwakilisha Tanzania. Hayo yamekuwa yakifanyika ingawa hadi sasa hakuna vigezo mahsusi vilivyowekwa na vinavyotumiwa katika uteuzi wa watumishi hao wa umma.

Kwa hakika, uwakilishi wa Wazanzibari ndani ya taasisi za Muungano umekuwa ukibadilikabadilika. Kwa mfano, tukiangalia huko nyuma tunaona kwamba uwakilishi wa Wazanzibari katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano ulikuwa mkubwa mno na wenye maana mnamo mwaka 1964 kushinda ulivyo hii leo. Kinyume na hali ilivyokuwa 1964 hii leo uwakilishi wa Wazanzibari katika Serikali ya Muungano ni dhaifu wala si wa maana hivyo; hauzimi hauwashi.

Labda taasisi pekee hii leo katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania yenye idadi sawa ya wawakilishi kutoka Tanganyika na kutoka Zanzibar ni Tume ya Mabadiliko ya Katiba yenye wawakilishi 15 wa Kizanzibari na 15 wengine wa Kitanganyika. Wawakilishi wote hao kutoka sehemu mbili za Muungano wametwikwa jukumu la kukusanya na kuyaratibu maoni ya Watanzania kuhusu Katiba mpya waitakayo. Miongoni mwa maoni hayo patakuwako yale yatayopendekeza taasisi mpya za Muungano ziwe na miundo gani na nini uwe mustakbali wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Hata hivyo, kuna Wazanzibari wasio wachache wenye kufanya kazi na kushika nyadhifa kubwakubwa katika taasisi za Muungano na ndani ya vyama vikuu vya kisiasa vilivyowavutia Wazanzibari, yaani CCM na CUF.

Kadhalika, Wazanzibari wanawakilishwa katika Bunge la Tanzania kama ilivyo kawaida tangu uasisiwe Muungano. Isitoshe wapo na baadhi ya Wazanzibari walio wakurugenzi katika halmashauri mbalimbali za taasisi za kibiashara zinazomilikiwa na Serikali ya Muungano.

Lakini kutokana na mfumo wa Muungano tulionao wakubwa hao wa Kizanzibari wanaofanya kazi Bara wanashughulikia zaidi mambo yanayoihusu Tanganyika na ni nadra kuzigusa shughuli zinazoihusu Zanzibar.

Hiyo ndiyo hali halisi ilivyo na ilivyokuwa tangu Muungano uasisiwe miaka 48 iliyopita. Tukiangalia dhima ya mawaziri wa Kizanzibari waliomo ndani ya Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano utaona kwamba wengi wao wanashughulikia masuala ya kiutawala yahusuyo Tanganyika. Wazanzibari walio katika Bunge la Muungano nao pia wanajadili na kuyatungia sheria masuala ya Tanganyika, ingawa mara chachechache hutushangaza wanapowasilisha mbele ya Bunge la Muungano mada zinazohusika na Zanzibar.

Kwa vile Muungano huu ni baina ya Tanganyika na Zanzibar, kuna maswali mawili ya kimsingi ambayo lazima waulizwe walioiwakilisha Zanzibar katika taasisi za Muungano tangu mwaka 1964. Swali la kwanza ni hili: Ni hatua gani za maana walizozichukua kuleta maendeleo Zanzibar na kuistiri nchi yao? La pili na la kimsingi zaidi ni: Wawakilishi hao wa Kizanzibari (wa zamani na wa sasa) wanawajibika kwa nani? Kwa serikali iliyowateua au kwa Wazanzibari wenzao?

Ndipo tunapolirejelea lile suala letu la awali, suala la uwajibikaji. Viongozi na wakubwa wengine ndani ya serikali na ndani ya taasisi na mashirika ya umma lazima wawe wanawajibika kwa sababu ya dhamana na majukumu mazito waliyo nayo. Wanahitajika wayatekeleze kwa dhati majukumu yao kwa maslahi ya wananchi bila ya kuzifikiria nafsi zao au za walio wao.

Tunatambua kwamba mtu hapati uongozi hivihivi tu, hakabidhiwi uongozi akaachwa mikono mitupu. Uongozi huandamana na manufaa, marupurupu, heshima na fadhila za kila aina. Hivyo, tunajua kwamba kuna Wazanzibari wengi walionufaika binafsi kutokana na ‘mahusiano’ yao na taasisi za Muungano.

Kwa sababu ya manufaa hayo waliyoyapata na wanayoendelea kuyapata kuna miongoni mwao wanaokhiyari kuyaangalia tu maslahi yao badala ya kuyazingatia na kuyateteta maslahi ya nchi yao na ya wananchi ‘wanaowawakilisha’.

Tutawafanyia jamala kubwa wawakikishi wa Kizanzibari walio katika taasisi za Muungano ikiwa mara kwa mara tutawakumbusha kwamba wanapaswa wawajibike kwa Serikali ya kwao na kwa Wazanzibari wenzao, ingawa kweli mara nyingi wawakilishi hao huwa hawachaguliwi na Wazanzibari wenzao bali huwa wanateuliwa ama na Serikali ya Muungano huko Bara au na vyama vya kisiasa wanavyoviwakilisha.

Inasikitisha kuona kwamba kwa vile Wazanzibari hao wamepewa vyeo na Serikali ya Muungano baadhi yao wamepoteza dira ya hali halisi ilivyo huko kwao. Wasingekuwa hivyo basi pasingekuwa na sintofahamu miongoni mwa baadhi yao kuhusu madai wanayoyatoa Wazanzibari wenzao katika mchakato wa kulipatia taifa Katiba mpya.

Ushahidi uliopo kutokana na maoni yaliyowasilishwa hadi sasa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni kwamba asilimia 47 ya Wazanzibari wanaoishi sehemu za Unguja Kusini wamependekeza muundo wa Muungano ubadilishwe na pawepo na Muungano wa Mkataba. Pendekezo hilohilo limetolewa na asilimia 87 ya Wazanzibari waishio sehemu za Pemba Kusini.

Hiyo ni idadi kubwa ya watu na wote hao watapiga kura katika kura ya maoni itayoamua kuhusu Katiba ya aina gani iwe nayo Tanzania.

Mwelekeo uliopo ni kwamba pale Tume ya Mabadiliko ya Katiba itapoanza tena shughuli zake za kupokea maoni ya wananchi Unguja Kaskazini na Unguja Mjini dai la kutaka Muungano wa Mkataba litazidi kushika kasi.

Ikiwa ni hivyo serikali ya Muungano haitodiriki kulipuuza dai hilo ijapokuwa inasemekana kwamba Tume itatoa mapendekezo yake kwa kuzingatia nguvu za hoja zinazotolewa kuunga mkono rai fulani. Haitotoa mapendekezo kwa kuzingatia rai fulani inaungwa mkono na wingi gani wa wananchi. Kipimo kitakuwa nguvu za hoja za kulitetea pendekezo fulani na wala si wingi wa idadi ya watu wenye kuliunga mkono pendekezo hilo.

Wakati huohuo sidhani kama hapa tulipofika Wazanzibari wataridhika kuwa na muundo wa Muungano wa Serikali tatu ikiwa muundo huo utapendekezwa kuwa ndio uwe muundo mbadala wa kulifunika kombe na kuunusuru Muungano.

Wawakilishi wa Kizanzibari walio wajumbe katika taasisi za Muungano wa Tanzania, ikiwa pamoja na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hawana budi ila kukuna vichwa vyao na kuyazingatia maoni ya walio wengi miongoni mwa wananchi wenzao. Ni muhimu vilevile wawe kila baada ya mara wanajikumbusha kwamba wanawajibika kwa wanaowawakilisha.

_______________________________________________________

Makala hii ilichapishwa kwenye gazeti la Raia Mwema la tarehe 29 Agosti 2012

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.