Waumini wa Kiislamu wakibeba mabango ya kukataa sensa.

Na Salim Said Salim (Tanzania Daima la 26 Agosti 2012)

LEO ni siku ya kufanyika zoezi la kuhesabu watu na makazi nchini lijulikanalo kama sensa. Upo wasiwasi mkubwa kwa zoezi hili kupata mafanikio yanayotarajiwa Zanzibar na inawezekana zaidi ya theluthi moja ya watu wakalisusia.

Katika siku za karibuni kumekuwepo na kampeni kabambe za chini kwa chini na hadharani katika baraza za kahawa, maskani za vijana na katika mikutano ya hadhara kuwataka watu wa Zazibar walisusie zoezi hili Unguja na Pemba. Wapo watu ambao wamekuwa wakipita majumbani pia kuwataka wananchi wasikubali kuhesabiwa.

Kumesikika maelezo kwamba kwa vile haki haitendeki na serikali ya Zanzibar inawabagua baadhi ya watu wake na kuwanyima haki za raia hapana sababu ya wananchi kushirikiana na serikali iliyo madarakani, iwe ya chama kimoja au umoja wa kitaifa. Njia mojawapo wanayoiona hao wanaopiga chapuo ya kususia sensa ni kutaka watu wakatae kuhesabiwa.

Kundi lililopo mstari wa mbele katika kampeni hii ya kususia sensa ni baaadhi ya viongozi wa dini ya Kiislamu, hasa wa Umoja wa taasisi na Jumuiya za Kiislamu Zanzibar. Amir (kiongozi), Sheikh Msellem Ali, alitoa masharti kadhaa katika mkutano wa waandishi wa habari ambayo alisema kama hayatatekelezwa alisema viongozi wa Kiislamu waliojiunga na taasisi hizo wataendelea kuwashawishi wafuasi wao kususia zeozi la sensa ya watu na makazi visiwani.

Miongoni mwao masharti hayo ni kutekelezwa mara moja haki ya kisheria kwa wananchi kupewa vitambulisho vya Uzanzibari kwa kuwapatia vitambulisho wale wote wanaostahili na pia itoe amri kwa watu wote waliopewa vitambulisho hivyo kwa utashi wa kisiasa kuvirejesha.

Sharti jingine ambalo jumuiya hii inataka ni kuingizwa kwa kipengele cha dini katika dodoso za sensa hiyo. Pia wanataka kiwepo kipengele kinachoeleza huyo aliyehasabiwa ni muumini wa dini gani.

Kiongozi wa jumuiya hiyo aliitaka serikali isitishe mara moja vitambulisho kutoka Tanzania Bara kuletwa visiwani kwa sababu tayari Zanzibar ina vitambulisho vyake.

Vikundi vinavyounda mwamvuli wa Umoja wa taasisi na jumuiya za Kiislamu Zanzibar ni pamoja na Taasisi ya Vijana wa Kiislamu Zanzibar, Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu na taasisi za Kiislamu za kuendeleza Uchumi Zanzibar.

Vile vile vimesambazwa vipeperushi vinavyopiga chapuo ya kutaka kugomea sensa na vitambulisho vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mpaka mfumo wa Muungano ueleweke baada ya mchakato wa Katiba. Kwa hakika kilichopo ni mkorogo mtupu.

Lakini tukitaka tusitake ukweli ni kwamba upo mgogoro visiwani juu ya sensa inayotarajiwa kufanyika leo na sababu kubwa hasa ni juu ya utoaji wa vitambulisho vya Mzanzibari .

Inakisiwa kuwa zaidi ya watu 50,000 hawana vitambulisho. Mimi katika familia yangu ni watu sita na inasemekana kuvipata hivyo vitambuliso ni shida kubwa na zaidi ni kutokana na ukorofi wa masheha.

Mtu anaweza kupewa barua ya kwenda kuchukua kitambulisho ikiwa haina tarehe na akifika ofisi inayotoa vitambulisho anaelezwa haifai kwa vile haina tarehe. Wengine wanapewa barua ikiwa haina muhuri na wapo wanaokataliwa kabisa kupewa barua hiyo kwa madai kuwa sheha hawatambui kama wanaishi katika eneo lake, ijapokuwa huyo sheha anamjua kwa zaidi ya miaka 10 na ni jirani yake.

Baadhi ya hawa masheha walidai hata kutowajua watoto wao waliowazaa wakati wa zoezi la kuandikisha wapiga kura. Visa na mikasa yao unaweza kuviandikia kitabu au kufanyia mchezo wa sinema.

Kwa mfano, mtu ilibidi amchukue mwanawe kwenda kuandikisha kupiga kura kwa kuamini sheha atasema hamjui na hapo ndipo alipomuuliza yule mtoto kama anamjua sheha na mtoto akajibu huyu ni babu. Ukweli ni kwamba yule bwana alioa binti wa huyo sheha na yule mtoto ni mjukuu wake.

Mtu mwengine baada ya kukataliwa kuandikishwa kupiga kura aling’oa mlango wa nyumba yake na kwenda nao kwenye kituo cha uandikishaji wapiga kura na hapo alimuuliza hati zilizopo mlangoni za namba ya nyumba ni za nani.

Sheha alikiri kuwa ni zake na aliyebeba mlango akamwambia kuwa yeye ndiye mwenye ile nyumba na hapo ndipo karani alipomuandikisha kuwa mpiga kura. Hivyo ndivyo visa vya masheha wa Zanzibar ambao wamechangia sana kuwepo mgogoro huu wa sensa Visiwani.

Serikali inasema kila anayestahiki kupata kitambulisho apewe, lakini hilo ni porojo tu na mpaka leo mamia ya watu wamekuwa wakihangaika kwa miezi kupata vitambulisho na juhudi zao kugonga ukuta.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, aliwaahidi waandishi wa habari mwaka jana kwamba atalifuatilia suala la watu kunyimwa vitambulisho, lakini hadi sasa hakuna maelezo yoyote juu ya huo ufuatiliaji wake.

Watu wengi wanaamini kwamba wananyimwa vitambulisho kwa sababu za kisiasa kutokana na kufikiriwa ni wapinzani na hivyo wakinyimwa vitambulisho watakosa haki ya kupiga kura.

Kichekesho ni kuwa inamchukua mtu siku tatu au nne kupata hati ya kusafiria (pasipoti), lakini anaweza kuhangaika hata kwa miezi minne na akashindwa kukitia mkononi kitambulisho cha Mzanzibari.

Wengi wa watu waliokosa vitambulisho ni wenye asili ya Kisiwa cha Pemba na hii imewafanya Wapemba wengi kufanya majumuisho kwamba wanabaguliwa kutokana na msimamo wao wa kisiasa wa kuwa wapinzani.

Tatizo la vitambulisho vya Mzanzibari ni kubwa ingawa linafumbiwa macho. Ni kweli mamia ya watu wasiostahiki kupata hivi vitambulisho wamepatiwa (wengine majirani zangu) na inadaiwa hilo lilifanyika ili wapige kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Chama gani walikipigia wanajua wenyewe.

Hata serikali inalielewa hili vizuri na ndio maana miezi miwili iliyopita ilitoa tamko rasmi la kuwataka watu wote waliopatiwa vitambulisho wakati hawastahiki kuwa navyo wavirejeshe haraka.

Hapa yanazuka masuala mengi. Mojawapo ni kwanini watu hao walipewa hivyo vitambulisho wakati hawastahiki na nani alitoa amri ya watu hao kupewa vitambulisho? Hapa sheria ilivunjwa na kwahivyo waliohusika wanapaswa kuwajibishwa kisheria.

Kichekesho kingine katika hili suala la vitambulisho ni kwamba ni kosa la jinai kwa Mzanzibari kutokuwa na kitambulisho, lakini kama mtu ananyimwa hicho kitambulisho afanyeje?

Kama kweli sheria ya vitambulisho ilitakiwa ionekane kuwa ya haki basi watu wanaowanyima vitambulisho wale wanaostahiki kupewa nao wahesabiwe wametenda kosa la jinai, lakini sheria imekaa kimya na kuwafumbia macho kama vile kuwaruhusu wahusika wabague nani apewe kitambulisho na nani asipewe ni sawa.

Katika huu ususiaji wa kujiandikisha sensa watu waliokosa vitambulisho na kunyimwa haki ya kupiga kura wanaeleza kuwa wao hawatambuliki kuwa Wazanzibari wala si Watanzania na ndiyo maana walinyimwa haki ya kupiga kura katika uchaguzi wa Zanzibar na hata ule wa Jamhuri ya Muungano.

Wanachosema watu hawa na hoja yao ni ya msingi ni kwamba kama hawatambuliki kuwepo kwao Zanzibar kwa nini wahesabiwe? Hii ni hoja ya msingi na haifai kutafutiwa suluhisho la kisiasa. Njia pekee ni kuhakikisha kila Mzanzibari mwenye haki ya kupata kitambulisho anapewa bila ya masharti.

Nilieleza mapema kupitia gazeti hili mwezi uliopita kuwa huenda zoezi la sensa likawa na matatizo Zanzibar kwa sababu ya mwenendo wa kisiasa wa siku zilizopita na ambao unaonekana bado kuendelezwa kimya kimya hadi hii leo.

Kwa mtazamo wangu, kinachoonekana hivi sasa juu ya suala la sensa ni matokeo ya kunyima watu vitambulisho na sasa watu walionyimwa haki ya msingi ya kiraia wanaamua kususia jambo ambalo lina umuhimu mkubwa kwa nchi kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hii ndiyo hatari ya siasa kuongoza sheria badala ya sheria kuongoza siasa.

Katika makala yangu yenye kichwa cha maneno “Sensa ina matatizo Zanzibar” nilieleza kuwa baadhi ya viongozi wa dini bado hawana imani na kufanyika kwa zoezi hili. Sina hakika kama suala hili lilishughulikiwa na wahusika na sasa tunaona matokeo yake.

Vile vile niliweka wazi kwamba lipo kundi kubwa la watu ambao hawatataka kuhesabiwa kwa sababu wanadai kuwepo kwao hakutambuliwi na serikali na ndiyo maana hawapewi vitambulisho. Hili nalo limepuuzwa na tunaona matokeo yake.

Sasa sensa imeshapiga hodi. Sijui hao wanaohesabu kura watapokewa vipi watakapopiga hodi katika baadhi ya nyumba kutaka kuhesabu watu. Kama kweli dalili za mvua ni mawingu basi ninachokiona kama hawatakaribishwa kwa shari pia hawatapokewa kwa heri.

Lakini ukweli ni kwamba pamoja na kutotolewa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya sensa pia haikufanyika kazi ya kutosha kutatua matatizo ambayo yalionekana kutaka kujitokeza. Tuombe salama wakati wa zoezi la sensa na siku zinazofuata.

One thought on “Vitambulisho vya Mzanzibari vyaiponza sensa”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.