Kanisa lililochomwa moto Zanzibar wakati kile kilichotakiwa kionekane kama vurugu za kidini.

Na Sammy Makilla (imechukuliwa kutoka ukurasa wa Facebook)

VIJANA wa Zanzibar hawawezi kubahatika wachaguliwe mabalozi au wabunge au mawaziri au wajumbe au viongozi wa tume au kamati hii au ile kimuungano. Mfumo wetu wa kisiasa na kiuchumi haukuundwa kwa namna ya kuwapa uhakika wa maisha na matarajio yao ya kesho. Ni wahaka au wasiwasi au hofu hii inayowafanya wawe ni pono rahisi katika ajenda binafsi za watu na taasisi visiwani humo.

Vitendo vya kuchoma makanisa, magari na mali nyingine za mapadri na waumini wa Kikristo sio kielelezo au ushahidi, sembuse uthibitisho wa udini au Uzanzibari na Uzanzibara, bali maelekezo ya hasira na ghadhabu arijojo zisizokuwa na mahala pa kutupwa.

Na ikawa kama vile takataka zinazonuka, ukaacha kutupwa uwani mwako ukazimwaga uwa wa jirani. Na kwa bahati mbaya haraka na papara ya viongozi kadhaa wa dini na kisiasa ni kurukia kusikika na kuonekana kwenye tivii kwa kulifanza hili ni tatizo la udini, wakashindwa kutanabahi tatizo halisi lililoko na linalohitaji kutafutiwa dawa visiwani humo.

Kwenye nchi ndogo yenye kila sababu na iliyokaa kimkakati kufanya mambo mengi makubwa tu kuliko nchi nyingi kubwa huu ndio mtihani unaoikabili Zanzibar hivi leo. Wazanzibari wengi na hasa vijana wana njaa na kiu ya kutumika kuiendeleza nchi yao, lakini hawapewi nafasi hiyo.

Tofauti za hali ya maisha na kipato ndio mchawi wa kuangaliwa na wala sio kitu kingine. Wageni na viongozi ndio wanaotajirika lakini sio watu wa kawaida. Matokeo ya hili ni wivu, husuda, inda, chuki na magomvi ambayo hayawezi kumalizwa kwa mabavu au mtutu wa bunduki.

Nimeamua kuandika makala haya baada ya watu kadhaa kuanza kudai wanachokifikiria kama vile udini ghafla umegeuka kuwa tatizo Tanzania. Ikawa watu waanza kushughulikia kitu kisichokuwa na chanzo halisi kikasahauliwa.

Kihistoria Zanzibar imekuwa ikiitegemea bara kwa mahitaji yake mengi. Bei ya karafuu ilipoanguka chini, uchumi wao uliyumba vibaya. Jitihada zao za kujenga na kuendesha viwanda ambavyo vingeliweza kutoa ajira zimekwama. Ushindani wa kielimu uliokuwepo hapo zamani umeporomoka kiasi cha kutisha, na hivi leo Zanzibar inaongoza kwa kufelisha sio kupasisha.

Aidha jitihada za Zanzibar ambayo ni nchi yenye Waislamu takriban asilimia 97 kujiunga na OIC na kushirikiana karibu zaidi na nchi za Kiislamu na Kiarabu zinaonekana kukutana na mkwara huu au ule.

Wazanzibari wengi ni wapenda michezo, sanaa na utamaduni. Hata hivyo serikali huko imeshindwa kujenga mazingira muafaka yanayoweza kuchangia vijana kujiajiri kwa michezo, sanaa na asili yao au Uzanzibari wake.

Kilichobakia ni jitihada za watu binafsi kama vile Bi Hamdani aliyeweza kuwafunza wanawake kupiga ala za muziki wa taarabu na hao aliowafundisha hivi leo sio tu wanaweza piga ala hizo, bali wamejiajiri na wanahitajika kama sio kuuzika kote duniani.

Kwa kukosa ajira na kukosa nafasi za mazoezi na mchezo vijana wanaghilibiwa n kuwa mateja wakiwanufaisha wazungu wa unga visiwani humo na pia wale wa Mrima.

Vile vile uwekezaji unaoendelea visiwani humo umemtenga mzawa na anatumika katika kazi za kutoa jasho na sio kutumia akili na maarifa. Zanzibar kama nchi, kwa maneno mengine imeshindwa kuwa na mkakati wa kuwafanya vijana wa Kizanzibari kujiona kuwa sio tu nchi ni yao,bali kubwa zaidi uchumi ni wao na historia na utamaduni wao unaenziwa badala ya kubakwa na wageni.

Pamoja na udogo wake, Zanzibar imeshindwa kutumia eneo na nafasi iliyopo kuendeleza teknohama na teknolojia nyingine za wakati wetu zinazoweza kukuzwa na kustawi kwa haraka na kwa manufaa makubwa visiwani humo.

Zanzibar ikijipanga ipasavyo ni kituo kikuu cha kati katika kuunganisha Afrika na Mashariki ya Kati na mbali katika matumizi mbalimbali ya teknohama na hivyo kutoa ajira kwa maelfu kama sio malaki .

Harakati za Wapemba baada ya Mapinduzi ya 1964 hadi kuuawa kwa Karume mwaka 1972, kwa namna moja au nyingine kulifanya kazi kama vile kiondoa msongo kwa maelfu ya Wapemba na Waunguja kuhamia Mrima, yaani Tanzania Bara na Pwani ya Kenya. Siasa za CUF dhidi ya CCM nazo pia kwa kiasi fulani zilitoa sio tu bali nafuu ya namna fulani ya visiwa hivyo kuja kupata nuru na neema siku za mbele.

Baada ya CCM kuikubali CUF kuunda Serikali ya mseto/umoja, matumaini ya vijana wengi kwamba maisha yangeliweza kugeuka kuwa bora yametoweka. Vijana leo wanaamini kwamba CCM na CUF ni kitu kile kile, na hali yao itabaki vile vile.

Ieleweke kama vile vyombo vya dola vilivyoshidwa kuwadhibiti watu walokuwa wakidai haki wakati wa mgogoro kati ya CCM-CUF Zanzibar, ndivyo vivyo hivyo ninavyohofu kwamba rasilimali za taifa huenda zikatumika kushughulikia ishara za maradhi na sio maradhi yenyewe.

Kwa maneno mengine, hivi leo Zanzibar kuna ombwe la kisiasa hususan katika kazi ya kuujenga uchumi wa nchi ili kuwapa ajira na matumaini vijana wa Kizanzibari kuwa kesho na kesho kutwa yao ina kila sababu ya kuwa nzuri na yenye faida kwao.

Kwa hali ilivyo sasa, inaonekana wazi kuwa nchi ina utawala lakini haina viongozi au wakubwa wameingia katika utandu wa siasa za kibara na hivyo kushindwa kujimiliki na kujinasua na kuchanua kama watu huru wanaoweza kuipelekea Zanzibar kule
inakostahili kwenda na sio vinginevyo.

Katika hali kama iliyopo sasa hivi vijana wako tayari kujiunga na kufanya kazi na mtu yeyote yule anayewapa matumaini mapya kwamba anaweza kuchangia kubadili maisha yao na kwa sababu watu kama hao, hawana mtazamo wa mbali na mbele ila wakaribu huishia kuibua matumaini ya vijana, lakini wakashindwa kuyatafsiri wayatakayo vijana kwa vitendo.

Katika sehemu ya pili ya makala yangu haya ambayo hayatachapishwa gazetini humu, nimetoa mapendekezo kadhaa ambayo yanaweza kuisaidia Zanzibar kuondokana na masahaibu yake ya leo na kesho.

Nimewahi kutembelea sehemu mbalimbali Zanzibar kwa hisani ya watu kama kaka zangu Salim Saidi Salim wa Deutsche Welle na Ally Saleh wa BBC na Bwana mdogo Jabir Idrissa, na kuona mambo mengi ambayo yanataka tu Zanzibar izaliwe upya kifikra na kimawazo kuyageuza mambo hayo kuwa ni mtambo isiyochoka kuingizia Zanzibar cha kuipa uhuru wa kweli na nusura ya kutotegemea tena watu wengine kwa maendeleo yake baada ya muda si mrefu.

Katika mapendekezo yangu, nimependekeza pamoja na mambo mengine umuhimu wa Zanzibar kama nchi kuwa na Mpango-Mkakati wake wa angalau miaka 10 tokea sasa. Wakati wa kuandaa mpango mkakati huo, kazi muhimu zitakuwa ni pamoja na kutambua ni wapi Zanzibar ilipo leo kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kiteknolojia.

Na kisha kuwa na picha ya wapi Wazanzibari wanataka nchi yao iwe baada ya miaka hiyo kumi. Kisha baada ya hapo malengo, mikakati, sera, mbinu, rasilimali mali na watu, fikira, dira na msimamo, mtazamo na mwelekeo wa visiwa vyote utakuwa ni kujenga daraja kati ya pale visiwa vilipo hivi sasa ili kwenda kule wanakotaka muongo ujao.

Vijana wasiokuwa na ajira, kazi, maisha na matumaini sio tatizo la Unguja na Pemba tu, ni tatizo la dunia nzima. Kama yalivyo Zanzibar ndivyo yalivyo bara. Hivyo, yafaa kufanya kazi hii pamoja.

Kutokana na ukweli huu, itakuwa ni ujinga basi kutarajia kuwa ufumbuzi wa tatizo hili huko visiwani unaweza ukatoka Ulaya au Marekani hivi sasa.

Maana ukweli jamaa hao, ndugu zao, baba na mama mmoja wako kwenye hali mbaya zaidi. Nina imani kuwa tatizo hili linaweza kushughulikiwa kwa haraka na kasi zaidi kwa kushirikiana na nchi za Kiislamu za Urussi ya zamani, Malaysia Uchina, Indonesia na nchi za Kiarabu ambazo zina kila sababu za kihistoria kusaidia Zanzibar kuliko nchi nyingine yoyote duniani.

Na nyenzo kubwa katika kuwasaidia vijana ni kuhakikisha wana elimu bora na wana uwezo wa kuzungumza lugha mbalimbali na hasa Kiarabu na Kichina na kufanya vitu tofauti kwa uwezo uleule.

Ni matarajio yangu kuwa mchango huu mdogo utasaidia kulipa tukio la mwisho wa mwezi Mei, mwaka 2012 huko Zanzibar picha na sura sahihi zaidi, na pande zote zinazohusika zitaanza kuchangamkia tatizo la vijana na ajira visiwani humo ikiwemo misikiti na makanisa badala ya kushughulika na vidonda vya maradhi yaliyopo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.