Wawili hawa. Rahimahumallah!

PROFESA Issa Shivji na mimi tumetoka mbali. Kwangu, yeye ni kama ndugu. Sote ni waumini wa falsafa ya umajumui wa Kiafrika na tunaitetea kwa nguvu hoja ya umuhimu wa kuungana kwa bara la Afrika. Isitoshe sote tunaamini kwamba tunapoichambua jamii tunapaswa tuichambue kitabaka kwani kwa kufanya hivyo tu ndipo tunapoweza kuwatetea kwa haki wanyonge wa dunia hii.

Shivji, ambaye ni Mwenyekiti wa Wataalamu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) na pia Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni mtu mwenye kuheshimika ndani na nje ya nchi kwa michango yake ya kitaalamu. Ameandika mengi na kusema mengi kuhusu masuala ya kikatiba ikiwa ni pamoja na suala la Muungano wa Tanzania na uhalali wake.

Miaka kama minne iliyopita aliandika kitabu alichokiita ‘Pan-Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika-Zanzibar Union.’ Maudhui ya kitabu hicho yalikuwa ni kuangalia nini kilichochochea kuundwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na mafunzo gani tunayoweza kujifunza kutokana na Muungano huo.

Wiki iliyopita Shivji alishiriki katika mjadala uliofanywa Dar es Salaam wa nafasi ya vyombo vya habari katika Muungano. Kwenye mjadala huo aliueleza kinaganaga msimamo wake juu ya Muungano. Kwa bahati mbaya gazeti moja nchini liliyapotosha aliyoyasema na kudai kwamba aliupinga Muungano. Taksiri hiyo ya uandishi ikampa Shivji fursa ya kuyakanya hayo na kuueleza tena msimamo wake katika makala aliyoandika katika hilo gazeti lililomnukuu sivyo.

Ama mimi nilishangazwa mno na aliyoyasema kwenye mjadala na aliyoandika kwenye makala. Nilishangazwa kwa sababu baadhi ya matamshi yake si matamshi ya kusemwa na mtu wa kipaje chake. Nilishangazwa pia kwa sababu msimamo wake wa juzi unanikanganya na sasa sijui ni upi msimamo wake halisi kuhusu Muungano — huu wa juzi au ule aliouainisha katika kitabu chake cha miaka minne iliyopita?

Hayo ya juzi yanakinzana na aliyoyaandika kitabuni alipokuwa anauchambua uhalali wa Muungano. Humo kitabuni aliandika kwamba lau Tanzania ingekuwa na mahakama huru basi Katiba ya Jamhuri ya Muungano ingefutwa kama hoja ya kufanya hivyo ingepelekwa mbele ya Mahakama hiyo.

Shivji alikuwa na sababu ya kuhoji hivyo na sababu yenyewe ni kuwa katiba hiyo ilianza kama katiba ya muda na ilifanywa na mtu mmoja yaani Rais wa Tanzania bila ya hata kumshirikisha Rais wa Zanzibar. Hiyo ndiyo hatimaye ikawa katiba ya kudumu kutoka mwaka 1977 ilipoidhinishwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kinyume na utaratibu uliokubaliwa na Hati ya Muungano ya 1964.

Utaratibu uliokubaliwa ni kuwa katiba ya Tanganyika itatumika kuwa katiba ya muda kwa kipindi cha mwaka mmoja na kwamba katiba ya kudumu itatungwa na Baraza Maalumu la Kutunga Katiba ambalo litapendekezwa na pande zote mbili za Muungano na ambalo litakuwa na idadi sawa ya wawakilishi wa Zanzibar na wa Tanganyika.

Kwa vile hilo halikutendwa na badala yake chama ndicho kilichotunga katiba ya Jamhuri ya Muungano labda ndiyo maana Shivji akasema kwenye kitabu chake ya kwamba Mahakama huru ingeifutilia mbali katiba ya sasa ya Tanzania. Hayo yanaingia akilini.

Kinachokanganya akili ni kumuona Shivji akiuvuka mstari wa kuwa mwanasheria, tena mwanasheria mahiri, na kujifanya msemaji wa wale wenye kuwatisha Wazanzibari. Ninasema anawatisha kwani amenukuliwa kuwa aliyasema yafuatayo mwenye mjadala wa wiki iliyopita: “Wazanzibari wengi wanafanya kazi na kufanya biashara Tanzania Bara, kwa hiyo wanaposema Muungano uvunjwe italeta athari kubwa sana kwa sababu itabidi wafukuzwe.”

Kwa nini itabidi wafukuzwe? Na hivi Shivji anakuwa anasema kwa niaba ya nani anapowatisha hivyo Wazanzibari kuwa ukivunjika Muungano watafilisiwa mali zao na kufukuzwa kutoka Bara?

Hapo kuna mambo mawili matatu ambayo Shivji anayasahau. Kwanza, anasahau kwamba siku hizi kuna utawala wa sheria katika sehemu zote mbili za Muungano: Tanzania Bara na Zanzibar.

Vilevile anasahau kwamba Watanganyika nao wana rasilimali zao nyingi Zanzibar. Kwa mfano, wao ndio wenye kuyamiliki takriban mabenki yote yaliyopo Zanzibar isipokuwa People’s Bank of Zanzibar.

Kadhalika, wanamiliki mengi ya mashirika ya bima na mabaa yalioko Zanzibar, mjini na mashambani. Kuna Wabara wanaohodhi biashara za utalii hasa katika Mji Mkongwe. Kuna waliopewa ekari tatu tatu za ardhi na serikali ya Zanzibar na kuna waliojaa katika mashamba na mjini na kuna Wabara wanaofanya kazi Zanzibar hasa katika sekta ya utalii na kuna mamia ya wafanya biashara wadogo wadogo kutoka Bara.

Shivji aliendelea kuwatisha Watanzania wote kwa kuandika kwenye makala yake ya wiki iliyopita kwamba: “Tukianza kubaguana kati ya Watanganyika na Wazanzibari, tutaendelea kubaguana kwa msingi wa Uislamu na Ukristo, na Usukuma na Uchaga, Uarabu na Uafrika, weusi na weupe bila kikomo.”

Sijui kwa upande wa Watanganyika lakini kwa upande wa Wazanzibari dai la kutaka mfumo mbadala wa Muungano si dai la kuwabagua Watanganyika. Ni dai la kutaka kuuimarisha kidhati Muungano wa nchi zetu. Shivji hajitendei haki hata yeye mwenyewe pamoja na utaalamu wake anapoligeuza dai hilo na kulisingizia kuwa ni kubaguana kati ya Watanganyika na Wazanzibari.

Hali kadhalika, kauli yake kwamba Muungano umeleta tija ya kiuchumi kwa pande zote mbili na kwamba ukivunjika wananchi watateseka ni kauli ya kichekesho ukizitathmini hali zetu za kiuchumi na mfumo tulionao wa uchumi tegemezi.

Swali linalostahili kuulizwa ni: Je, wananchi wapi walionufaika na Muungano? Ni walala hoi walio wengi na wenye kazi pevu ya kujitafutia riziki au ni wafanyabiashara wachache na wale wanaopata natija kutokana na mfumo uliopo wa utawala?

Na wala si sahihi kusema kama asemavyo Shivji kwamba kuwapo kwa Muungano kumesaidia kuunganishwa kwa chumi za pande mbili za Muungano. Kwanza, hakutoa ushahidi wenye kuonyesha faida waliopata wengi wa wananchi wa Tanganyika na wa Zanzibar kutokana na kuwapo kwa Muungano katika kipindi cha miaka 48 iliyopita.

Pili, ukweli wa mambo ni kwamba uchumi wa Tanganyika na ule wa Zanzibar hazikuunganishwa ingawa kuna sarafu moja na mfumo mmoja wa utozaji kodi na ushuru.

Ukitembelea soko la Zanzibar utaona kwamba kuna bidhaa nyingi zitokazo China na hata Ghuba ya Arabuni kuliko bidhaa zitokazo Bara. Kwa upande wa Bara nako hakuna biashara ya maana inayofanywa kati yake na Zanzibar.

Takriban biashara ya pande mbili inahusisha biashara ya nje. Kwa mfano, kuku hapa Zanzibar wanatoka Brazil, maziwa yanatoka Arabuni, kahawa inatoka Brazil na Kenya na chai inatoka huko huko Kenya ingawa Tanzania Bara ni taifa lenye kusafirisha kahawa na chai.

Shivji anapendekeza ubadilishwe muundo wa uongozi kwa kuwekwa rais mmoja na waziri mkuu mmoja ambapo kati yao hao mmoja atakuwa anatoka Tanzania Bara na mwengine Zanzibar. Ni haki yake kupendekeza alivyopendekeza. Lakini ikiwa yeye ana haki ya kupendekeza hivyo kwa nini anawanyima wengine haki ya kupendekeza mfumo wa aina yoyote wa Muungano ikiwa wa katiba au wa mkataba, haki ambayo wanapewa Wazanzibari na katiba zote mbili za Tanzania na Zanzibar?

Watanzania wote wanahakikishiwa haki hiyo kwa mujibu wa sheria zinazohusika na mchakato mzima wa kutafuta katiba mpya ya Tanzania na mwongozo uliotolewa na Jaji Joseph Warioba kwamba wananchi wana haki ya kutoa mapendekezo yoyote yale wayatakayo hata ikiwa ni ya kutaka Muungano uvunjwe. Sasa tumsikilize nani: Shivji au Warioba?

Kwa hakika wanaotaka Muungano wa Mkataba hawasemi kuwa wanataka kuuvunja Muungano. Wanachosema ni kuwa wanataka kuuimarisha na kuufanya uwe na maana kwa kuugeuza badala ya kuwa wa kikatiba na kuufanya uwe wa mkataba.

Wanachodai ni mfumo mbadala wa Muungano, mfumo ambao utakuwa kivutio cha kuzivutia nchi nyingine za Kiafrika zijiunge nao kwa moyo wa umajumui wa Kiafrika.

Kuhusu mada hii Shivji anakosea anapodai kwamba chama kimoja Zanzibar (anakusudia chama cha CUF) ‘kinapandikiza’ pendekezo la Muungano wa Mkataba. Huu ni upotoshaji wa ukweli. Misimamo rasmi ya vyote viwili vikuu Zanzibar inajulikana. CCM ina msimamo wa kutaka mfumo wa sasa wa serikali mbili uendelezwe ila ufanyiwe marekebisho; CUF ina msimamo wa kutaka pawepo serikali tatu.

Dai la kutaka Muungano wa Mkataba ni dai linalosukumwa na wananchi kwa jumla bila ya kujali misimamo ya vyama vyao na linaungwa mkono na hata baadhi ya viongozi wa vyama hivyo lakini si msimamo wa chama chochote hapa Zanzibar. Na wala si kweli kwamba wenye kuutetea Muungano wa Mkataba hawakueleza waziwazi maana yake. Wameeleza kwa kina.

Jingine la kushangaza alilosema Shivji ni kwamba wanaotaka Muungano wa mkataba wana ajenda ya siri. Lakini iweje ya siri ilhali zoezi zima la kuratibu maoni ya Wazanzibari na ya Watanganyika linaendelea kwa uwazi na utulivu?

Isitoshe si siri kwamba hadi sasa wengi wa wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakitoa maoni ya kupendekeza mfumo mbadala wa Muungano wa kutaka pawe na Muungano wa mkataba baada ya kuona madhara yaliyoipata nchi yao hasa katika sekta za uchumi na ustawi wa kijamii.

Bila ya shaka kwa vile Shivji si Mzanzibari haishangazi kuona kuwa hana uchungu na Zanzibar. Lakini kwa vile anasifika kwa kipaje chake cha uchambuzi katika taaluma ihusiyo katiba tunamtarajia kwamba angalau ataendelea kulitendea haki suala hili kama ilivyokuwa tabia yake.

Ama mimi ninambembeleza Shivji alifanyie taamuli suala hili kwa kukisoma tena kitabu chake kwa makini. Lakini kwa namna alivyobadili maoni yake nachelea asije akageuka na kukirarua rarua kitabu chake mwenyewe.

__________________________________________________________________________________________________________

Makala hii ya Ahmed Rajab ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 15 Julai 2012 kwa jina la Shivji anapogongana na Shivji.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.