Prof. Isa Shivji

Na Abbas Muhunzi

Sikubaliani asilan na maneno ya Profesa Issa Shivji kuwa iwapo Muungano utavunjika Wazanzibari ndio watakaoathirika sana. Kwanza suala la Wazanzibari kuwa wako wengi wanafanya biashara Bara na kwamba ukivunjika Muungano watafukuzwa hivi ni vitisho vya watembea barabarani kuliko falsafa ya kiprofesa. Ukiangalia kwa kipimo cha ‘asilimia’ na sio idadi, basi wenye asili ya Tanganyika walioko Zanzibar ni wengi zaidi kuliko wenye asili ya Zanzibar walioko Tanganyika.

Biashara leo duniani imeunganishwa na mfumo wa utandawazi kuliko siasa na ndio maana Wakongo, Warwanda, Wazambia, Wangazija, Wachina nk. wako wengi Tanganyika na wala hakuna Muungano kati ya nchi watokazo na Tanganyika. Watu wanapofanya biashara hujinufaisha wao wenyewe pamoja na kunufaisha uchumi wa nchi wanayofanya biashara na ndio maana nchi zetu bila kuogopa kutawaliwa tena zinazialika nchi zote duania kuja kufanya biashara.

Kama itatokea Muungano uvunjike na Wazanzibari wafukuzwe Bara huu ni umbogo wa kisiasa ambao naamini Bara hawawezi kuufanya kutokana na hadhi waliojiwekea duniani kwa kuheshimu haki za binadamu na amani. Ndio maana nchi hili ilikubali hata kuwapa hifadhi wakimbizi wa nchi nyengine na leo wanatafutiwa uraia pamoja na kwamba nchi zao hazina tena kadhia zilizowakimbiza.

Hapa hapana tena nafasi wa kuwaelimisha Wazanzibari kuhusu historia ya Muungano na faida zake kwani wasiojuwa historia ya Muungano kama mimi basi wana uzoefu wa kutosha wa faida na hasara za Muungano kwani ndio wanaishi ndani ya Muungano wenyewe. Leo kwa mfano ushuru wa forodha ulisawazishwa kwa matakwa ya Tanganyika na Wafadhili na ikaundwa Mamlaka ya Mapato ya Tanzana (TRA) na Ofisi ya Zanzibar inaongozwa na Msaidizi Kamishna na wafanyakazi wote wanaajiriwa na Muungano na wanalipwa mshahara na Muungano na wanapangiwa kazi na Muungano.

Sheria ya forodha ya nchini na kimataifa inasema mzigo ukiingizwa katika bandari yoyote ya nchi utachukuliwa umeingia nchini. Kama Tanzania ni nchi moja kwa Profesa ulivyotusomesha, inakuwaje leo mizigo ikilipiwa ushuru Zanzibar na ikipelekwa Bara inazuiwa na kutakiwa kulipiwa ushuru upya kama haujaingia nchini?

Hivi sasa kuna magari zaidi ya 400 kutoka Zanzibar iyamezuiwa Bara na maofisa tu Serikali! Huu ni ushahidi kuwa mazingiza ya nchi zetu hayaruhusu kuwa na mfumo wa uendeshaji wa pomoja lakini yanaruhusu kuwa na mfumo mashirikiano tu kihaki.

Kusema kuwa kuwe na Rais mmoja na Waziri Mkuu mmoja na kutoka pande mbili ndio kuimeza Zanzibar kinyemela na sikutarajia Profesa alietokea Zanzibar angependekeza uhusuda huu wa wazi. Profesa aliebobea kwa sheria na historia atakumbuka kuwa Mwenye Kigoda aliwahi kuwaita Kenya Nyanga’u.

Hii ndio sehemu ya historia wasioijuwa wengi wetu na anayo nafasi nzuri ya kuwasomesha Watanzania. Leo tuko tayari kuzichapa na Malawi kwa Ziwa tu lakini hatuoni umuhimu wa Bahari na ardhi ya Zanzibar. Kama wanaotaka kuvunjika kwa Muungano wana tamaa za kibinafsi, na wale wanaotaka Zanzibar itoweke basi wanatamaa kubwa zaidi kwani wanataka kuhakikisha kuwa Zanzibar inamaliza historia yake, utamaduni wake na dini zake.

Hii ndio tamaa mbaya zaidi duniani kuliko ya suala la kibiashara alilolielezea Profesa Shivji. Mimi si miongoni mwa wanaotaka kuvunjika Muungano na hakuna mwanasiasa aliyewahi kutoa maoni kuuvunja Muungano hadi sasa, lakini tunachotaka ni Muungano utakaowapa uhuru wananchi wa pande mbili kujiamulia mambo yao ya kiuchumi na kijamii na yale yanayowatia khofu watu duniani yaani ya kuchafuka AMANI yapakie katika Muungano kwani sote tunataka tuishi kiusalama.

Haya hayataki KATIBA yanataka MKATABA ili iwe rahisi kiutekelezaji. Naamini Profesa kwa kushauri Serikali moja ndio hasa anafanya kazi iliyoacha na Mwalim Nyerere na pengine ndio maana akakabidhiwa KIGODA. Ajuwe ni Mwalimu alietufikisha katika mtafaruku huu ambao hatuko tayari tena kuuendeleza.

3 thoughts on “Profesa Shivji na hoja za mitengoni”

 1. Sikatai kuwa kuna mambo hayako sawa katika Muungano, kiasi kwamba Zanzibar inaathirika kutokana na mfumo na uendeshaji wa Muungano, kwa hivyo iko haja ya kurekebisha kero na kasoro za Muungano.

  Jambo ambalo sikubaliani nalo ni kusema kuwa hakuna uwezekano wa Wazanzibari kufukuzwa Bara na Watanganyika kufukuzwa Zanzibar. Wakenya, Wazambia, Wachina n.k. hawafukuzwi kwa sababu hakuna Muungano wa TZ na nchi hizo wala hatuna uhusiano nao wa kisiasa. Tukumbuke kuwa siasa ni mchezo mchafu.

  Tusiisahau historia yetu wenyewe ya CCM na CUF na Unguja na Pemba. Tuliwezaje kuchomeana nyumba moto, kumwagiana tindikali, kususiana kwenye mazishi, kutonunua katika viduka uchwara na kukatana mapanga na kuuana kwa sababu ya tafauti za kisiasa, tuje kushindwa kufanya kama hayo Muungano ukivunjika?

  Bado Muungano haujavunjika tayari tunasikia kelele za kuwa “vichogo warejee kwao” je ukivunjika itakuwaje? Tunadhani haya yanayofanywa sasa Zanzibar dhidi ya Watanganyika, wenzetu kule watakuja kukaa kimya wasifanye kama hayo na zaidi ya hayo Muungano ukivunjika?

  Sisemi Muungano udumu au uvunjike, ninachosema na nina hakika nacho, ni kuwa yanayoweza kutokea kama Muungano utavunjika kimunkari kama inavyotakiwa ifanyike sasa, yanaweza kuwa zaidi ya haya tunayoyaona au kuyafikiria sasa. Langu jicho!

 2. Suluhu ya Suala zima la Muungano ni MKATABA TU hakuna jengine litakaloweza kuchambua na kuonesha upi mchele na pumba .
  kwa sababu kuna baadhi ya watu wengi huwa wanafuata mkondo tu lakini sio wepesi wa kuona hali halisi .lakini tutakapokuwa na Muungano wa MKATABA basi ndugu zetu wa bara na Visiwani wataweza kuona hali halisi ya mapungufu ,faida au hasara ya M,uungano wetu.
  Tutakapo lazimisha mambo katika dunia hii ya Utandawazi Mwelekeo utakuwa mbaya.
  Haya ni maoni yangu Mtanzania halisi.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.