Watatu hawa!!!

Na Ahmed Raajab, Raia Mwema, 8 Agosti 2012

YEYOTE atayejaribu kuitalii jamii ya Zanzibar ya leo haitomchukua muda kutambua kuwa katika medani yake ya kisiasa kuna kambi mbili kuu. Kambi hizo zinawakilisha ajenda mbili zinazouongoza mjadala mkubwa wa kisiasa unaoendelea Visiwani: ajenda ya Tanganyika na ajenda ya Zanzibar. Hii ndiyo hali halisi ilivyo na kila siku zikisonga mbele inazidi kuwa wazi.

Tulipotanabahi kuwa hii ndiyo hali ilivyo na kuanza kuieleza katika kurasa za jarida hili kuna waliotuona kuwa ni wazushi, maadui, wasaliti na wachochezi. Walitupakaza kila aina ya uovu na kutusingizia mambo ya ajabuajabu.

Leo hakuna anayethubutu kukana kwamba hizo kambi mbili kweli zipo na kwamba ile ya ajenda ya Zanzibar ndiyo iliyo kubwa tena kubwa mno. Wala hakuna anayethubutu kukana kwamba kambi hiyo imewaunganisha wengi wa Wazanzibari bila ya kujali itikadi zao za kisiasa wala za kichama.

Hebu tuwatupie macho wanachama walio maarufu wa CCM/Zanzibar waliojitokeza wazi na kujitambulisha wamo kwenye kambi ipi kati ya hizo mbili. Hassan Nassor Moyo, mmoja wa wajumbe wa Baraza la Mapinduzi la awali lililoundwa mwaka 1964 na aliyewahi kuwa waziri katika serikali za Zanzibar na Muungano, anaiunga mkono ajenda ya Zanzibar na amechomoza kuwa kama kiongozi wa kambi hiyo.

Mwengine mwenye msimamo kama huo ni Mansour Yusuf Himidi, Waziri asiye na wizara maalumu katika serikali ya Zanzibar. Huyu ni kijana lakini ni mkereketwa wa CCM na baba yake Brigadia Yusuf Himidi alikuwa mmoja wa waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar. Baada ya Mapinduzi kufanikiwa yeye ndiye aliyeteuliwa awe mkuu wa jeshi jipya la Zanzibar na mjumbe wa Baraza la awali la Mapinduzi.

Walio katika kambi hii wanadai pawepo Muungano wa mataifa mawili yenye serikali mbili yatayoungana kwa Mkataba.

Kwa upande mwingine ndani ya hiyohiyo CCM/Zanzibar mwandishi wa habari wa zamani na mjumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM Ali Ameir anaiunga mkono kwa nguvu ajenda ya Tanganyika ya kutaka Muungano uendelee kama ulivyo minghairi ya kutiwa viraka vya hapa na pale.

Kwa hili anaungwa mkono na Shamsi Vuai Nahodha, waziri wa ulinzi katika serikali ya Muungano. Lakini hata yeye Nahodha anataka mabadiliko. Kwa mfano, anataka mambo ya mafuta na gesi asili yarudi Zanzibar.

Nahodha alianza kupata umaarufu katika siasa za Zanzibar alipoteuliwa waziri kiongozi na rais mstaafu Amani Abeid Karume.

Katika kambi ya kina Ameir na Nahodha ya Wazanzibari wachache wanaounga mkono ajenda ya kuwa na taifa moja lenye serikali mbili yumo pia Salmin Awadh ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na mjumbe wa kamati Kuu ya CCM.

Labda Awadh na wenzake wanahisi hawana hila ila kuiunga mkono hadharani sera ya CCM kwa vile wanachelea kulitilia mchanga tonge lao na wanaziona nyadhifa walizo nazo katika CCM kuwa ni zenye umuhimu mkubwa kushinda uzalendo wao wa Kizanzibari.

Moyo ameibuka kuwa shujaa wa Wazanzibari kwa ujasiri aliouonyesha katika kuupigania huo uzalendo wa Kizanzibari. Hadi sasa hakuchomoza kiongozi yeyote wa ngazi ya juu ndani ya CCM mwenye hadhi, haiba na hekima kama za Moyo na mwenye kuiunga mkono hadharani ajenda ya kuwa na serikali mbili katika taifa moja.

Kwa nini kina Ameir wakapaparika baada ya akina Moyo kujitokeza wazi na kutetea Muungano wa mataifa mawili yenye serikali mbili? Ni dhahiri kwamba walipoliona wimbi la wautakao Muungano wa Mkataba kina Ameir waliingiwa na hatihati, wahka na daghadagha. Walichojaribu kufanya baada ya hapo ni kutumia kila hila kuigwaza ajenda ya uzalendo wa Kizanzibari. Hatua ya mwanzo waliyoichukuwa ni kumlenga Moyo na kujaribu kumvunjia heshima yake.

Lililo wazi na kuthibitishwa na historia ni kwamba hakuna hata mmoja ndani ya kambi ya kina Ali Ameir anayeweza kufua dafu akilinganishwa na Moyo. Hakuna anayeweza kuzifikia sifa za Moyo katika harakati za kuwapigania wafanyakazi, katika harakati za chama cha Afro-Shirazi wakati wa kupigania uhuru na katika Mapinduzi ya mwaka 1964.

Kadhalika, mchango adhimu wa Moyo kwa hali ya utulivu uliopo sasa Zanzibar umekwishaingia katika kumbukumbu za historia ya Zanzibar na hakuna anayeweza kuufuta. Hili la mwisho tu linamfanya anapozungumza awe anasikilizwa kwani sauti yake imegeuka na kuwa sauti ya uadilifu.

Kinyume na wanasiasa wa jana wanaojaribu kumponda na kumchafualia jina lake, sisi wengine tunamkumbuka Moyo kuwa katika safu ya mbele ya wanaharakati wenye fikra za kimaendeleo hapa Zanzibar tangu tuko wadogo na yeye akiwa kijana. Uzalendo wake hauna shaka, imani yake ya Umajumui wa Kiafrika wa kutaka Bara la Afrika liungane pia haina dosari.

Hivi sasa ameibuka kuwa mwanasiasa mzingativu mwenye kutumia busara kuepusha hasara. Kama tulivyokwishadokeza ni yeye aliye mbele miongoni mwa waliojitolea kuilea hali iliyopo sasa Visiwani ya umoja wa kitaifa, hali iliyoleta utulivu na amani.

Ukweli uliopo ni kwamba kwa hili Wazanzibari wanamuunga mkono Moyo na wengi wao pia wanamuunga mkono kuhusu aina ya Muungano anaoutetea. Nahodha na Ameir hawana kaumu kubwa inayowafuata. Kwa Wazanzibari suala la Muungano ni suala la uzalendo na utiifu wa kitaifa.

Kutokana na maoni ya Wazanzibari yaliyokwishatolewa hadi sasa mbele ya Tume ya Katiba tunaona kwamba wenye kuunga mkono mfumo wa Muungano kama ulivyo sasa ni wachache. Walio viongozi wa kisiasa miongoni mwao hawawezi kubadili fikra za wananchi wenzao.

Ukweli mwingine uliopo ni kwamba Wazanzibari wengi wanasema kuwa hili si suala la chama. Si suala la CCM wala si la CUF. Ni suala la nchi. Ndiyo maana watu wakawa wanaulizwa maoni yao kwenye shehia na si kwenye matawi ya vyama vyao.

Tunaishi katika nyakati ambamo kila mtu ana haki ya kimsingi ya kusema atakalo bila ya kubughudhiwa. Kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake na kuyasambaza atakavyo. Kwa sababu hiyo ndiyo maana daima tutaiunga mkono haki ya kina Ali Ameir na wenzake kutoa maoni yao kwa uhuru bila ya wao kubughudhiwa.

Hata hivyo, Wazanzibari wenzao nao wana kila haki ya kuyapinga maoni hayo iwapo wanayaona kuwa ni maoni finyu na yasiyo na maslahi kwa Wazanzibari, hata kwa wao akina Ameir wenyewe.

Nilipokuwa nikiizingatia hii kadhia ya kina Ali Ameir na Moyo nimekuwa nikijiuliza: Wangesemaje kina Nahodha na Ameir lau Moyo angetamka kwamba anataka taifa moja lenye serikali mbili au taifa moja lenye serikali moja? Wangesema pia kuwa Moyo si Mzanzibari?

Kwa hakika, hii ni mara ya mwanzo kusikia Moyo akiambiwa kuwa si Mzanzibari. Siku zote tukimjua kuwa ni Mzanzibari kama tulivyo wengine ambao mababu au mababa zetu wamezaliwa kwingine na sisi wenyewe vitovu vyetu kuzikwa katika ardhi ya Zanzibar.

Moyo ni mzalendo na labda lililodhihiri sasa ni kwamba yeye ana uchungu zaidi wa Zanzibar kushinda kina Ameir wenye kujaribu kumkebehi.

Zile zama za kuwatandika bakora ya kisiasa au ya chama watu wenye mawazo huru sasa hazipo tena. Wenye kudhania kuwa zama hizo zinaweza kurudi wanaota ndoto za mchana. Jamii katika Tanzania nzima imepevuka vya kutosha kuweza kutambua haki za kimsingi za kila mtu na kuweza kuzitumia taasisi zilizopo kuzitetea haki hizo katika ulingo wa sheria.

Wanaojitutumua kichama kuwapinga wenye mawazo kama ya Moyo au ya Mansour Himidi wanapoteza bure nguvu zao kwani kwa kadri nionavyo hakuna mtu hapa anayekisikiliza chama. Si cha CCM si cha CUF. Nionavyo ni kuwa Wazanzibari wanaliona suala hili kuwa ni suala la ukombozi na si la malumbano ya kichama.

Wenye kutaka Muungano wa Mkataba hawapingi dhana ya Muungano. Wanachodai, kwa hoja na sababu wazitoazo, ni kuwa na Muungano mbadala. Lakini hata wale wasioutaka Muungano wana haki ya kusema hivyo na haki hiyo imeshadidiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Jaji Joseph Warioba.

Kuna uwezekano kwamba kina Ali Ameir wanaweza kuleta balaa hapa Zanzibar kwani kwa kuzusha mgawanyiko wa kisiasa ndani ya Zanzibar huenda wakaivuruga hali ya amani na utulivu iliyopo Visiwani. Ninaamini kuwa wanafanya hayo kwa akili zao wakitumai kwamba chokochoko zao zitaweza kuwababaisha na kuwapembeja wananchi na kuwafanya waache kuijadili katiba na badala yake wawe wanawajadili watu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.