Balozi Ali Karume

Nimeisoma vizuri na kwa makini makala ya Bwana Njelu Kasaka yenye anwani:  Sera ya kupokezana urais haitufai nchini  juu ya sera ya kupokezana urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kinachonishangaza ni kwa nini mtu mashuhuri katika jamii yetu anakataa hali halisi ambayo tunayo kikatiba, na imetupatia marais wanne tofauti?

Sera ya kupokezana urais inatufaa nchini, na ndio maana tukabadili katiba yetu na kuweka vipindi vya urais. Iwapo hatutaki urais wa kupokezana, basi turudi kule kule enzi ya zamani ambapo rais akitawala, aendelee kutawala mpaka afe, ilimradi awe anachaguliwa kwa kura kila baada ya kipindi muafaka.

Kwani Mwalimu Julius Nyerere si alitawala kwa miaka 20 na akaamua kuacha kutawala kwa hiyari yake ? Angeamua kututawala, kwa muono wangu, Mwalimu Nyerere angetawala mpaka kifo chake mwaka 1999. Angetutawala maisha yake.

Sera ya kupokezana urais ni nzuri na lazima. Nasema lazima ibakie katika katiba mpya; rais akae madarakani kwa sio zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano, iwapo atapata ridhaa ya wananchi na kuchaguliwa.

Tatizo linakuja pale rais anapomaliza muda wake, na mchakato wa kutafuta rais mpya unaanza. Vyama vya siasa hutafuta watu mashuhuri wagombee urais kwa niaba ya vyama vyao, na katika hivyo vyama, hatukosi kuona makundi yanopendelea mtu wao.

Hilo sio geni katika siasa. Kila chama hujaribu kumpata mgombea anokubaliwa na viongozi wote wa chama, lakini hilo hushindikana na inabidi mgombea apatikane kwa kura za wajumbe husika katika chama. Ndio maana wagombea huwa wengi hapo mwanzo na baadae hupatikana mgombea mmoja kutokana na nguvu za kundi lake kwenye chama.

Chama kinapozingatia nani apewe ridhaa ya kuteuliwa, mambo mengi huangaliwa. Katika hayo ni pamoja na kuzingatia rais aliyemaliza muda wake alikuwa ni mtu wa rika gani. Madai ya Mwalimu kwamba rais anaweza kuwa Mkiristo na akafuatiwa na Mkiristo kwenye urais, au akiwa Muislamu anaweza kufuatiwa na Muislamu mwenzake, ni nadharia tu, lakini katika hali halisi, wazee wa chama hushauri (bila ya kutangaza) kwamba bora rais anomaliza muda akiwa Muislamu, afuatiwe na rais wa dini nyengine; na huko ndio kupokezana. Sasa tatizo liko wapi?

Njelu Kasaka ataridhika ikiwa rais wa 2015 atakuwa Muislamu hata akitoka Bara?

Njelu Kasaka

Sidhani kwamba mwandishi wa makala hii ataridhika na rais mpya ifikapo 2015 atoke bara na awe Muislamu, ilimradi katimiza sifa alizozieleza. Ikiwezekana, awe Mkiristo mwenye sifa zinotegemewa ili jamii yote ishiriki katika kukamata wadhifa huo wa juu.

Hakuna anobishana na hitimisho kwamba “Rais achaguliwe kwa kuzingatia uwezo wake, elimu yake, uadilifu wake…” ila la uzuri wa sera zake halipo, maana tunataka rais shupavu katika kutekeleza sera na ilani ya chama chake ambacho kinaweza kumdhibiti iwapo atatamani madaraka ya udikteta.

Rais jendaheka hafai, na ndio maana kwenye urais haifai kuwa na mgombea huru, hilo likome kwenye ubunge na nyadhifa nyengine. Rais ni vyema apitie kwenye chama chake ambako anawajibika kisera. Wapiga kura mara nyingi hupigia kura vyama kwa kupendezwa na sera kupitia ilani ya chama.

Hiyo huwa ni ahadi ya utekelezaji, na ahadi ni deni. Bora chama kisimamie utekelezaji wa hizo ahadi. “Uzoefu ni sifa ya nyongeza lakini si lazima sana” uzoefu wa kitu gani? Mgombea urais gani anodai kwamba anao uzoefu wa kuwa rais, kaupata wapi?

“Mifano imezagaa ya wanasiasa wenye uzoefu wa miaka mingi wakishindwa kuongoza vizuri wanapopata nafasi.” Hao mimi nawaogopa, maana wana uzoefu wa kutenda kwa mbinu za kale na hawawezi kujirekebisha kwenye mbinu za kisasa, hutegemea sala ili Mungu awajalie wapate matokeo mema. Ukipanda mdanzi, tabu kuchuma machungwa. Dunia ya leo, watu wanataka “Change” hata ikiwa saa nyengine, hawaijui maana yake.

“Uwezo binafsi na ubora wa sera ndio viwe msingi wa kuamua nani apewe uongozi wa nchi”. Kweli kabisa, lakini katika nchi yenye jamii ya watu wa aina nyingi ki rika, kabila, dini, jinsia, kanda, eneo nk, sio vyema uongozi wa juu kama urais ushikwe na Wakristo tu au Waislamu tu, ilimradi wamekidhi sifa zinazotegemewa.

Kuwe na sera ya makusudi ya kupokezana urais, ilimradi watoshika wadhifa huo wawe na sifa zinotegemewa. We are a diversified community, and leadership should reflect that diversity. Tunahitaji kuepuka ukiritimba wa kutawaliwa na watu wa dini, kabila, rika, jinsia, kanda au imla moja.

Kwa nini Muungano wetu “mzuri” unakimbiwa na wengine?

Mwalimu Julius Nyerere, mmoja wa waasisi wa Muungano.

Sasa twendeni kwenye taswira au mfumo wa kijamii, kisiasa na kiuchumi ambao unaifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa tofauti na nchi nyengine, hasa kwenye bara la Afrika. Mara nyingi tumetolewa mifano kwamba nchi yetu ndio nchi ya pekee ya muungano kwenye bara la Afrika. Nchi zetu, baada ya uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar, ziliungana na kubaki katika muungano kwa sababu nyingi sana, lakini sababu muhimu ni kwamba mfumo wa muungano wa serikali mbili umewezesha Zanzibar kujisikia kwamba bado wanao uhuru wao na wanajitawala wenyewe kupitia serikali yao. Kuna rais, Baraza la Wawakilishi na Mahakama ya kujitegemea. Uhuru huo umehakikishwa kwenye nyanja zote isipokuwa mambo ya nje, ulinzi, mambo ya ndani, usalama wa taifa na sarafu za fedha. Katika Afrika, hakuna nchi hata moja ilotamani kujiunga na muungano wetu kwa sababu ya mapungufu yake.

Marekani wana msemo kwamba “If you have a good thing going, everybody will want to be a part of the act”. Ikiwa kweli muungano wetu ni “A gravy train”, mbona nchi nyengine za jirani hazijawahi hata kututembelea na kuangalia mfumo wa huu muungano, na hakuna nchi hata moja inotaka kujiunga na sisi? Ukweli ni kwamba nchi zote zilowahi kuungana kwenye bara la Afrika, sasa zimetengana na juzi tu tumesikia south Sudan kujitenga na Tanzania ikawa nchi ya mwanzo kutambua jamhuri mpya ya south Sudan. Hii inamaanisha kwamba kwenye nchi za kiafrika mtengano ni bora kuliko muungano?

Mapungufu ya Muungano

Abeid Karume, mmoja wa waasisi wa Muungano.

Tunahitaji kuangalia upya muundo wa muungano wetu na ndio maana Watanzania wengi wamekaribisha zoezi la katiba mpya ili mapungufu yaliyopo, yashughulikiwe kikamilifu. Moja katika hayo mapungufu ni imani ya baadhi ya Watanzania wenzetu, hasa kutoka Bara, wanoamini kwamba wajibu wetu ni kujenga taifa moja lenye nchi moja na baadae, serikali moja. Wanolivalia njuga hilo ni wale wanoamini kwamba kutokana na wingi wao, wataimeza Zanzibar na kuifanya mkoa.

Hilo halikubaliki kwa sababu Wazanzibari kutokana na uchache wao, wanaogopa kumezwa na walo wengi. Na siasa ya dimokrasia hutegemea kura, na walo wengi huwashinda walio kidogo. “Let the minority have their say, and the majority will have their way” haikubaliki na Wazanzibari kwa sababu wao ni minority na pasipokuwa na safeguards za kunusuru interests za Wazanzibari, basi watatawaliwa na Watanganyika maisha. Ndio maana Mwalimu Nyerere alikataa mfumo wa serikali moja kwa kuhofia hisia ya Wazanzibari kwamba wamemezwa.

Safu ya Uongozi katika Muungano

Ali Hassan Mwinyi, Raisi wa Awamu wa Pili wa Muungano wa Tanzania. Mzanzibari mwenye asili ya Kisarawe, Tanzania Bara.

Katika muungano wa aina yoyote, safu ya uongozi, hasa safu ya juu, ni lazima ibebe viongozi kutoka sehemu zote za Muungano. Yale madai kwamba Wazanzibari wengi ni kidato cha nne tu na hawana uwezo wa kuongoza, ni hisia ambazo zimepitwa na wakati. Kuna Wazanzibari wengi tu ambao wanakidhi sifa zinotegemewa na ni wajibu kuwapa nafasi za uongozi katika Muungano.

Hilo ni pamoja na wadhifa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Kufanya hivyo hakutogawa nchi yetu, bali kutokufanya hivyo na kuruhusu marais wote watoke upande mmoja wa Muungano, ndiko kutogawa nchi maana Wazanzibari wamejenga hisia kwamba wao ni second class citizens katika nchi yao wenyewe.

Ni kweli kwamba katika nchi ambayo si ya muungano, kuna hatari ya kugawa zamu ya uongozi kwa makundi tofauti. Mfano mbaya tumeuona huko Lebanon. Lakini nchi yetu ni ya muungano, na katiba ya sasa inasema kwamba iwapo rais anatoka upande mmoja, makamo wake atoke upande mwengine and vice versa.

Tumekwenda nalo hilo kwa miaka mingi, tatizo liko wapi? Wanodai kwamba rais wa muungano atoke popote tu ilimradi anazo sifa zinotegemewa, wengi wanatoka bara, na wanahisi kwamba kutokana na wingi wao wataweza kutawala wenzao. Ni kweli kabisa kwamba iwapo haitachukuliwa juhudi ya kupokezana uongozi wa juu, basi wote watatoka bara kutokana na wingi wao.

Madai ya kwambaMmzanzibari anaweza kuchaguliwa kuwa rais wetu ilimradi awe anazo sifa zinotegemewa sio madai sahihi. Wapiga kura wengi huchagua chama, lakini pia huchagua mtu. Iwapo vyama vya siasa havitolazimishwa kuweka mgombea urais kutoka Zanzibar, pale ifikapo zamu yao, basi chama kitoweka Mzanzibari kitahatarisha ushindi wake. Wapiga kura wetu wengi huangalia mtu, na bado wapo wapigakura wenye hamu ya kumchagua Nyerere au chama chake. Ukimuuliza umepigia kura chama gani, anakujibu kwamba kapigia kura chama cha Nyerere. Sioni vipi mgombea urais kutoka Zanzibar ataweza kufaulu iwapo vyama vengine vimeweka mgombea kutoka Bara?

Mara nyingi huwa na wasi wasi juu ya kuona uongozi kwenye nyanja ya urais ukikamatwa na mtu wa dini moja au jinsia moja kwa hofu kwamba watu wa dini au jinsia nyengine wanaweza kulalamika. Hilo halijapata kutokea kwa sababu nchi yetu ni ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na sio muungano wa wanawake na wanaume, au Wakristo na Waislamu.

Tungekuwa tumeingia kwenye muungano wa kidini au kijinsia, basi walioungana wangekuwa na haki ya kujitambulisha ili na wao wapate zamu katika kuongoza. Nayasema haya kwa sababu ni imani yangu kwamba zamu ya uongozi sio lazima ifuate dini, kabila au jinsia, lakini ni bora ifuate utaifa; nikikusudia kwamba mataifa mawili huru yakiungana pande zote zitadai kushiriki kikamilifu kwenye uongozi, na hilo tabu kulikamilisha iwapo hakuna zamu ya uongozi.

Uhalali ya Hoja ya Mpokezano Urais kupitia Mifano Hai

Tony Blair, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza kutoka England, ambaye baada ya kuondoka alimpisha Gordon Brown kutokea Scotland.

Hivi sasa, tumedhamiria kuingia katika Shirikisho la Afrika Mashariki. Ndio kwanza tumeanza na suala la mwanzo lilikuwa la uongozi. Tulikubaliana kwamba mtendaji mkuu au Secretary General atoke kwenye member states kwa zamu. Walianza Kenya wakafuatiwa na Uganda na Tanzania. Ilipofika zamu ya Rwanda, kuna baadhi ya viongozi walishauri kwamba duru ya uongozi ianze upya kuanzia Kenya. Walidai kwamba Rwanda na Burundi walikuwa ni associate members tu na wasitoe mtendaji mkuu.

Rais wa Rwanda, kwa ushupavu mkubwa, alidai kwamba Rwanda walikuwa fullfleged member na walistahili kutoa kiongozi wa juu. Tuliwaunga mkono na mashirikiano yetu hayakutetereka. Nani anadai kwamba Secretary General wa East African Community anaweza kutoka popote ilimradi awe na sifa zinotegemewa? Maradhi hayo tunayo sisi watanzania maana kwenye kazi kama hizo tunaamini kwamba hakuna mzanzibari mwenye uwezo wa kuiwakilisha nchi yetu.

Hivi karibuni askari wa kijeshi wa Tanzania walipelekwa Comores (Ngazija) kwenda kumuondoa Col. Bacar kwenye madaraka ya urais wa Anjouan. Bahati nzuri hatukupoteza watu wetu katika zoezi hilo. Lakini niliambiwa kwamba huyo muasi wa Anjuan, alitaka kuvunja katiba ya nchi inayoitwa “Union of the Comoros” inayosema kwamba marais wa nchi hiyo iliyoungana kwa visiwa, watachaguliwa kwa zamu, kipindi kimoja kimoja kwa kila kisiwa, bila ya kujali ukubwa wake au idadi ya wakaazi. Jee, katiba hiyo inotowa zamu katika uongozi hatimae itawasarambatisha watu wa Comores? Ikiwa jibu ni ndio, kwanini sisi, nchi ya muungano, tusothamini umuhimu wa zamu ya urais, tupeleke jeshi na kuhatarisha maisha yao, kutetea sera ambayo baadhi yetu wanadai kwamba haifai? What is good for the Comoros, of which we are willing to die for, must be good for our country.

Turejee tena nyumbani na kutembelea baadhi ya matatizo ya muungano wetu. Sina nia ya kujitolea kutoa dawa ya kutibu matatizo ya huu Muungano. Maana ya muungano ni kwamba iwapo mnashirikiana katika kuendesha nchi mbili ambazo ziliwahi kuwa huru kabisa na kujitegemea, lazima matatizo yatatokea. Tumeliona hilo kwenye muungano wa nchi nyengine kama England, Scotland, Wales na Northern Ireland.

Wenye kuleta malalamiko zaidi ni watu wa Scotland. Sababu ziko nyingi, lakini sababu kubwa ni ya kihistoria wakikumbuka kwamba kuna wakati Scotland ilikuwa nchi huru inojitegemea na walipigana vita vingi kufikia hali hiyo. Na kuna wakati katika historia mfalme wao James II, alikuwa pia James I wa England baada ya ufalme kurejeshwa kufuatia kifo cha Oliver Cromwell. Wanadai kwamba wamechoka kutawaliwa na England na kuibiwa mafuta yao ya North Sea, ambayo yanatoka kwenye eneo la Scotland.

Kwa miaka mingi, ulitumika umahiri wa kisiasa kutoa uongozi wa zamu kwenye wadhifa wa Waziri Mkuu. Inasemekana kwamba baada ya Anthony Eden kujiuzulu baada ya kashfa ya Suez, Butler aliomba chama chake kimpe ridhaa awe Waziri Mkuu mpya. Mzozo uliendelea mpaka chama kikaamua kwamba apewe Harold McMillan. Butler alipouliza sababu ya hilo, aliambiwa kwamba mawaziri wakuu waliotangulia, Churchill na Eden, walitoka England na afadhali anayefuata atoke Scotland. Na kweli walifuatia McMillan na Alec Douglas Home, wote kutoka Scotland. Kinachotakiwa ni political engineering, na hiyo huipati mpaka uipate political architecture iliyokua madhubuti.

Katika historia ya UK ya hivi karibuni tumeona kwamba Waziri Mkuu Tony Blair alitoka England na akampisha mwenzake Gordon Brown kutoka Scotland.

Marais wote wa Muungano wangetoka Zanzibar, Muungano huu usingefika miaka 48

Amani Karume, Rais wa Awamu ya Sita wa Zanzibar.

Uongozi wa nchi ziloungana hauna budi kuwa na zamu hasa ikiwa tuna nia ya kupunguza malalamiko ya kuelemewa na kukoseshwa pumzi. Wacheni tupumuwe ni kwa pande zote mbili. Marais wote wa Tanzania wangetoka Zanzibar, huu muungano usingetimiza miaka 48.

Hata hao marais wote wangetoka Zanzibar na wangekuwa na sifa zinazotegemewa, Wabara wasingekubali, na hata mimi mzanzibari nisingekubali. Ningeshauri urais wende kwa zamu. Hata mjukuu wangu siku moja nilimuuliza juu ya kupokezana marais na nikamuuliza kwani kuna ubaya gani ikiwa marais wote wa muungano watatoka Tanganyika? Alijibu…”I don’t know; but it just doesn’t seem right” Ndio next generation hiyo.

Marekani wameweza kuhimili matatizo mengi walipoanza kuungana na hasa walipoanza na madola 13. Wengi wa waanzilishi wa taifa jipya la muungano, walitokea Dominion of Virginia. Rais wa kwanza alipochagua makamo wake, alishauriwa asimchague Thomas Jefferson, ingawa alikuwa na sifa zote. Alimchagua John Adams kutoka Massachusetts ili alete uwiano. Alipoamua kuacha urais, wengi walimpendekeza Adams awe rais na alipomaliza ndio Jefferson akapewa urais akiwa rais wa tatu.

Mifano hiyo iko mingi, na sisi Watanzania ni lazima tujifunze kwa wenzetu. Urais bora wende kwa zamu sio kwa makundi, dini, kabila, kanda au jinsia. Hao sio waliounganisha nchi, wamejikuta tu wanaishi kwenye jamii moja. Walounganisha nchi zao, wanategemea kwamba uongozi hasa kwenye safu ya urais utakwenda kwa zamu.

Mwalimu Nyerere, katika historia yetu, alisimamia hilo kwenye uchaguzi wa rais wa muungano wa 1985. Wengi wanaamini kwamba kama sio usimamizi huo, rais angetoka Bara, maana kwa wakati huo, ndiko kulikokuwa na magwiji waloamini kwamba wao peke yao ndio wangefaa kutawala kwa sababu walitoka “from the right place, with the right name”, an exaggerated sense of entitlement.

Labda ndio maana yakazuka ya G55 na serikali ya Tanganyika pengine ni kwa sababu baadhi yao waliona kichefuchefu kutawaliwa na Mzanzibari. Walisahau Kisarawe.

Mwaka 1995, tuliingia tena kwenye zoezi la kumtafuta rais wa muungano. Kati ya watu takriban 13 waliotaka kutuongoza kwenye wadhifa huo, kulikuwa hakuna Mzanzibari hata mmoja aliyejitokeza. Wazanzibari wawili waliulizwa kama wangetaka kushiriki katika zoezi hilo na wote walikataa wakitoa sababu moja tu: “Rais anayetoka madarakani ametokea Zanzibar na sio vyema rais atakaefuata pia atokee Zanzibar!”

Mmoja kati ya hao, ambaye alifikiriwa kuwania urais mwaka 1985, inadaiwa kwamba hata Nyerere alitamka kwamba mwachieni agombee hakutokua tatizo kinadharia. Lakini mtajwa, kwa uungwana wake, alikataa na kusema labda atajaribu rais wa muungano kutoka Bara atapomaliza muda wake.

Sote tunayajua yaliyotokea mwaka 2005. Wagombea wengi kutoka pande zote za Muungano walijitokeza, lakini uongozi wa nchi, akiwemo rais wa muungano na yule wa Zanzibar, hawakuona umuhimu wa kumpata rais wa muungano kutoka Zanzibar. Viongozi wengi walidai kwamba “Katiba haisemi hivyo” Ndio maana, kwa muono wangu, Wazanzibari wengi wangependelea Katiba mpya itamke wazi kwenye hilo, ili sura ya Muungano wetu itambulike kimataifa kwamba ni “equitble union”. Equitable to all the citizens of the United Republic of Tanzania.

Mfumo wa Muungano ubadiike kwa kuwa umeshachosha

Mifumo ya muungano iko mingi, na ni muhimu, tena muhimu sana kwa muungano wetu uwe wa haki na uonekane kwamba ni wa haki. Vyenginevyo, tunawapa fursa watu waliochoka na hisia za kutawaliwa na upande mmoja, kuukacha mfumo huu wa “Unionism” na kujaribu kupendekeza mifumo mingine. Wapo watu, kama mimi, wanotaka muungano wenye usawa kwa raia wote, na sio muungano ambao rais akitoka upande mmoja, basi anapendelea watu kutoka kwao kwenye ajira na terms of service.

Sitegemei kwamba rais akitoka Zanzibar, na yeye atapendelea wazanzibari wenzake kwenye ajira. Katiba yetu haimzui Mzanzibari kuwa Jaji Mkuu, na mmoja alifikia wadhifa huo. Alifikia kutokana na sifa zinotegemewa. Wapo Wazanzibari wengi wenye sifa kemkem, lakini wanakoseshwa ajira kwa sababu tu rais wa muungano katoka upande mmoja. Hayo yakiendelea, na watu mashuhuri kutoka Tanganyika wakianza kung’ang’ana kwamba urais usiwe na zamu baina ya Wazanzibari na Watanganyika, itajengeka hisia kwamba kuna mbinu za Zanzibar kutawaliwa.

Wazanzibari wanokumbuka historia yao, kama watu wa Scotland, hawatakubali kutawaliwa na hisia kwamba wao hawafai kushika wadhifa mkubwa kabisa kwenye taifa letu. Watakumbuka kwamba waliondowa utawala wa Kireno, wa Kiingereza na wa Kiarabu, na haiyumkin wao kubatizwa na hisia kwamba bado wanatawaliwa. Hisia kama hiyo ni sawa na maradhi yasiyopona, maradhi ya kuchafua mawazo.

Pia, wenye kutaka muungano huu udhoofike, wanapata nguvu ya kudai kwamba kutokana na mfumo huu, ni bora tuivunje Katiba na tuingie kwenye Mkataba. Kila mtu aliyekuwa mtaalamu wa mambo ya siasa anajuwa kwamba ushauri huo ni mbinu tu za kuvunja muungano.

Muungano wa Katiba si wa Mkataba

Nchi ziloungana hutengeneza Katiba; mambo ya Mkataba yanahusu mahusiano ya raia katika nchi, na mara nyingi tunasikia kesi mahakamani za raia kushtakiwa kwa kuvunja Mkataba. Huwezi kujenga taifa la kisasa liloungana kwa kutegemea Mkataba ambao upande mmoja unaweza kutoa notice ya miezi mitatu, au muda muafaka kutoka kwenye huo Mkataba. Tahadharini, chonde chonde ujiti na macho. Lakini yote haya, hupewa nguvu na watu ambao kwa kujua au kutambuwa, hufanya kusudi kutoa ushauri wa kikatiba ambao utapendelea upande mmoja, hasa katika ushirika wa kuongoza nchi.

Tumepata fursa adhimu ya kurekebisha katiba, ili kuiboresha. Mimi siamini kwamba nchi yetu inahitachi katiba mpya, ila katiba nyengine itakayokuwa na maslahi ya watu wote kutoka pande zote za muungano. Mambo ya kimsingi katika katiba mpya yatabaki vile vile kama yalivyo kwenye katiba ya sasa. Kwani nani anafikiria kwamba nchi yetu iendeshwe na Mfalme badala ya Rais anayechaguliwa na wananchi wake kwenye uchaguzi huru na wa haki?

Mambo ya kimsingi yatabaki vile vile, isipokuwa vipengele vinoudhi vifutwe. Vipengele hivyo ndio chimbuko la matatizo na Kero za Muungano. Moja ya vipengele hivyo ni pamoja na kipengele kinosema kwamba Rais wa Muungano atachaguliwa kiholela bila ya kujali anatokea wapi katika huo Muungano. Nchi zetu ni nchi za Muungano na katika muungano, nchi husika zipewe fursa ya kikatiba kushiriki kwenye uongozi kwenye ngazi zote, pamoja na urais wa Muungano. Sera ya kupokezana urais ndio sera bora kwa nchi yetu.

One thought on “Sera ya kupokezana urais haitufai nchini? Jibu la Balozi Karume kwa Njelu Kasaka”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.